Dr. Sigalla: Ushiriki wa Marie Stopes Tanzania katika Tuzo ya EJAT utasaidia kuondosha mitazamo potofu juu ya Afya ya Uzazi

Kayugumis

Senior Member
Joined
Jun 6, 2022
Posts
107
Reaction score
97

Dr. Geofrey Sigalla​

Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari (EJAT) 2022 zilizotolewa kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Jumamosi ya Julai 22, 2023 ambapo waandishi mbalimbali walifanikiwa kubeba tuzo kwenye vipengele tofauti.

Tuzo hizo ambazo ziliratibiwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kulikuwa na kipengele kipya cha Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi ambacho kimedhaminiwa na Marie Stopes Tanzania (MST).

MST imeshiriki ikiwa ni katika kuongeza wigo kwa Waandishi wa Habari kutumia kalamu zao kuelemisha jamii kuhusu masuala ya Afya ya Uzazi.

Kuongezwa kwa kipengele hicho cha Afya ya Uzazi kimetajwa kuwa ni sehemu ya kuongeza motisha kwa Wanahabari kuandika taarifa za masuala ya Afya ya Uzazi.

Walioshinda katika kipengele hicho ni;
1. Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi (Magazeti)
Zuhura Said (Zanzibar Leo)

2. Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi (Radio)
Peter Lugendo John (TBC Taifa)

3. Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi (TV)
Dafrosa Ngailo (Azam TV)

4. Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi (Mtandaoni)
Festo Charles Lumwe (Dar 24)

Dr. Geofrey Sigalla ambaye ni Mkurugenzi Mwandamizi wa Marie Stopes amesema MST inashirikiana na Baraza la Habari katika kuendelea kuweka msisitizo na kuchagiza msukumo wa utoaji wa habari zinazohusu Afya ya Uzazi.

Amesema “Hii ni pamoja na umuhimu uliopo katika masuala haya katika kuhakikisha tunakuwa na vizazi vyenye Afya, Taifa lenye ustawi na linalonufaika na idadi ya watu wake na vilevile kuepusha vifo vya akina mama vitokana na uzazi.”

Akielezea msukumo uliochangia MST kushiriki katika kutambua umuhimu wa Wanahabari amebainisha ni kutambua umuhimu wa Huduma za Afya ya Uzazi kama sehemu ya Haki muhimu zenye mchango kwa Jamii, akiongeza kuwa Wanahabari wanatoa mchango mkubwa katika kukuza uelewa na kuibua changamo zilizopo.

Amesema: “Kuondosha unyanyapaa katika huduma, Wanahabari wanahusika kuibua mijadala inayolenga kuondosha mitazamo hasi na potofu juu ya Afya ya Uzazi.

“Waandishi wa Habari wana mchango mkubwa katika kuchangia mabadiliko ya Kisera na Kisheria yenye lengo la kuweka mazingira mazuri ya kisera katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za taarifa za Afya ya Uzazi unakuwa na manufaa kwa wote.”

Amesisitiza Wanahabari wana jukumu kubwa la kuchambua na kuainisha changamoto za kimfumo kuweka wazi fursa na matokeo mazuri yanayopatikana kutokana na uwekezaji katika Huduma ya Afya ya Uzazi ambazo zinalenga kupunguza madhara yanayoikumba jamii.

Ameongeza Wanahabari wanachochea uwajibikaji katika eneo la Afya na hasa ya uzazi kwa kufuatilia ahadi na utekelezaji wa sera mbalimbali ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

Amesema “Tuungane kuwapongeza waandishi wote wa habari ambao wameamua kujikita katika kuifanya kazi hii na kuitendea haki kufika hapa.

“Nitoe wito kwa Waandishi wa Habari kuendelea kutoa kipaumbele katika kuangazia Habari zihusuzo Afya ya Uzazi Nchini ili kuendelea kutoa mchango mkubwa katika ustawi wa Jamii zetu.”

Ushirikiano wetu na Baraza la Habari Tanzania ni imani yetu kuwa mwakani waandishi wengi watashriki katika kuwasilisha kazi zetu katika kipengele hiki cha Afya ya Uzazi na hivyo kuongeza ushindani katika Habari za Afya ya Uzazi zenye umahiri na weledi unaotegemewa.

MCT WAELEZA SABABU ZA USHIRIKIANO NA MST
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga amesema “Tumeingia ushirikiano wa kukuza Uandishi wa Habari wa Uzazi salama za Afya Uzazi salama Nchini.

“Makubaliano yetu ni ya miaka miwili ambapo kwa pamoja tutakitangaza kipengele cha Afya ya Uzazi na Uzazi Salama ili kuwashawishi kuandika na kuandika kwa umahiri masuala hayo ambayo ni nyeti, hilo ni jambo muhimu kwa kuwa linahusiana na maisha moja kwa moja.

“Unapozungumzia Afya ya Uzazi unazunguzia maisha tangu mtu anapozaliwa, hivyo kwetu ni jambo muhimu sana, tumeshukuru sana kupata sapoti hii ya MCT katika EJAT.

“MST wanasapoti kipengele hicho kwa maana ya kutoa uwezeshaji wa kulipa washindi na mambo mengine yote yanayohusiana na suala hilo, pia tutashirikiana kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari ili kuwajengea uwezo wa kuandika kwa umahiri kuhusu suala la Afya ya Uzazi na Uzazi salama.”
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…