SoC01 Dunia katika uzani sawa

Stories of Change - 2021 Competition

Mulokozi GG

Member
Joined
Jul 14, 2021
Posts
34
Reaction score
44
Utaratibu wowote duniani tunaoufuata binadamu katika kuhusiana, ni matokeo ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja katika kutafuta njia zitakazo rahisisha uwepo wetu katika maisha yetu hapa duniani huku tukinufaika na kila kilichopo. Kwa kujua au kwa kutokujua watu wengi wamekuwa wakifuata baadhi ya taratibu zilizo anzishwa kama njia pekee inayoweza kuwafanya waendelee kuwepo katika ulimwengu huu(hawawezi kulaumiwa ni asili ya akili yetu kila kinachoifikia na tukakikubali kama ukweli inakilinda bila kujali uhalisia wake).

Ifahamike wazi kuwa utaratibu/mifumo yoyote iliyowahi kuanzishwa na vizazi vilivyopita ililenga kuboresha maisha ya vizazi vilivyokuwepo na vitakavyofuatia kwa namna moja ama nyingine. Kamwe mifumo husika siyo na haikukusudiwa kuwa njia ya mwisho inayopaswa kufuatwa ili binadamu waishi katika dunia hii.

Sababu kubwa iliyo na inayo sababisha mfumo wowote usiwe njia pekee ya kufuatwa ili kuishi katika ulimwengu huu ni ; Kutokamilika kwa uelewa wa binadamu juu ya uumbaji. Hii inasababisha kila utaratibu unaoanzishwa utengenezwe na uendane na idadi, uwezo pamoja na uelewa wa kizazi husika. Hii inadhihirisha ukweli kuwa hakuna mfumo wowote uliowahi kutengenezwa au kuanzishwa ambao ni kamili na uliosawa asilimia mia moja. Sababu kama haujui kwa asilimia mia moja kesho kuna nini, ni dhahiri ulicho kithamini jana kinaweza kisikufae leo na kinacho kufaa leo kikakuponza kesho.

Licha ya ufinyu wa uelewa wetu kama binadamu katika huu Ulimwengu, haituzuii kuboresha na kutengeneza utaratibu mzuri na uliosawa kwa wote ndani ya kizazi kilichopo na kijacho ili sote tuweze kunufaika na ngazi ya uelewa tulioufikia kama binadamu. Licha ya ukweli kuwa ni vigumu watu wote kuishi maisha sawa, ni uhalisia kuwa tunaweza kutengeneza mazingira sawa kwa wote. Kila aliye kwenye mazingira hayo akawa na nafasi sawa ya kunufaika na kupata kilicho bora kutoka kwenye jamii yake. Haya mazingira sahihi ni uzani sawa kwa wote wa kuiweka dunia yetu.

Kutokana na aina ya maisha ndani ya jamii zetu elimu, uchumi, imani na siasa(uongozi) ni mihimili muhimu inayohitaji maboresho ili kuiweka dunia yetu katika uzani sawa kulingana na idadi, uwezo pamoja na uelewa tulioufikia kama binadamu. Yafuatayo ni maelezo kwa ufupi ya hii mihimili;

Elimu ; neno elimu kwenye andiko hili lieleweka kama, Ujuzi na matumizi yake katika kuongoza, kutumia na kuhusiana na vitu au watu katika mazingira. Hivyo mtu yeyote ni mwenye elimu kama anao ujuzi na anautumia ujuzi huo kuongoza, kuhusiana au kutumia kitu chochote katika jamii inayomzunguka bila kujali ujuzi huo aliupata wapi na kwa njia gani. Njia inayotumika kutoa elimu ya kisasa(formal education) ilianza katika miaka ya mwanzo ya kipindi cha mapinduzi ya viwanda, ikiwa na lengo la kuzalisha wafanyakazi ili kuendeleza viwanda.

Elimu hii haikuwa na lengo la kupunguza wala kuondoa ujinga kama elimu nyingine za kale, bali ililenga kutengeneza tabaka la watu watakaotumikia na kuendeleza viwanda. Sababu ilikuwa ni zao la uhitaji, elimu hii imesaidia kusambaza baadhi ya maarifa na kukuza uelewa wa binadamu kwa kasi kwa pamoja na kwa kiasi kikubwa kuliko elimu nyingine yoyote katika historia ya binadamu. Hata hivyo ongezeko la wafanyakazi wasio na kazi (wahitimu wasio na ajira) ni ishara tosha kuwa elimu hii inahitaji maboresho ili kuendana na hali, idadi, uwezo na uelewa wa kizazi kilichopo na kijacho.

Katika kizazi chetu elimu ya msingi ilenge kumfanya mtu ajitambue(self determination), kiwango cha mtu kujitambua uwe ndio msingi kabla ya kupewa elimu nyingine yeyote. Mfano elimu jinsi akili inavyo fanya kazi , pamoja na elimu ya hisia zinavyozalishwa, zinavyofanya kazi na jinsi zinavyoweza kutawaliwa au kuongozwa (Emotion intelligence). Baada ya msingi imara katika elimu hii mtu ndiyo apewe ujuzi mwingine maalumu kulingana na mahitaji yake pamoja na jamii inayomzunguka. Tanzania na duniani kote hakuna tatizo la ajira, tatizo ni elimu na elimu siyo tatizo, tatizo ni aina ya elimu.

Uchumi ; neno uchumi kwenye andiko hili lieleweke kama, muundo au hali ya usimamiaji na utumiaji wa rasilimali katika maisha ndani ya eneo au Nchi. Uchumi kama mhimili ni matokeo ya ujuzi na matumizi yake ndani ya jamii husika, hakuna jamii inaweza kuwa na uchumi imara zaidi ya ujuzi ulio ndani ya jamii au taifa husika. Katika jamii sababu mojawapo ya muhimu inayo changia katika kuinua, kukuza na kuendeleza uchumi ni njia inayo tumika kubadilishana huduma ndani ya jamii husika. Katika njia hii pekee watu wanaweza kusaidiwa, kukatishwa tamaa, kuhamasishwa, kupendelewa au kunyonywa kwa kujua au kwa kutokujua.

Kwenye historia ya binadamu njia kadhaa zimetumika kwenye ubadilishanaji wa huduma au bidhaa kabla hatujafikia mfumo huu wa noti na sarafu. Ni mfumo huu peke yake unaowafanya wengi bila wao kujua kuwatumikia wachache. Jamii yetu bila kujua inaendelea na mfumo huu unaozidi kurefusha nafasi na daraja la kutoka kwenye umasikini.

Ili kuweka uzani sawa ni muhimu njia ya kubadilishana huduma kama ilivyo noti na sarafu(pesa) sasahivi, iwe na thamani ndani yake. Hii italifanya tabaka lenye mamlaka juu ya njia ya kubadilishana huduma lifanye kazi pia ili kuipa au kupata thamani ya kuweka ndani ya njia ya kubadilishana huduma.

Imani ; uhakika juu ya jambo au kitu fulani. Kwenye hali ambayo ni vigumu kuielezea kwa maneno, kila binadamu akifikia kiwango fulani cha uelewa huanza kuhisi uwepo wa Nguvu iliyo kubwa zaidi yake. Bahati mbaya sana licha ya kuhisiwa na kila aliye fikia hatua fulani ya uelewa, Nguvu hii huwa haijioneshi na haiwi bayana kwa mtu husika. Hivyo mtu hutegemea uelewa na maarifa yaliyo kwenye jamii inayomzunguka kama njia ya haraka ya kuielewa Nguvu anayoihisi. Kwa kutambua hili vizazi vilivyopita vilianzisha njia au utaratibu tofauti tofauti kulingana na jamii husika ili kuelewa na kunufaika na Nguvu hiyo. Utaratibu huu ndio ulibadilishwa na kuwa msingi na chanzo cha dini, mila na ibada mbalimbali zilizopo kwenye jamii zetu.

Katika mifumo tuliyo nayo iliyoanzishwa kuendana na kulingana na kizazi kilicho kuwepo, ni wazi baadhi ya mambo yameanza kwenda tofauti siyo tu kwa wanaofuata dini, mila au ibada husika bali hata kwa wanaoziongoza. Sina shaka kuwa ingekuwa siyo dini, mila pamoja na mafundisho yanayo endana na hayo maisha yetu binadamu yasingekuwa na tofauti sana na maisha ya Simba au Wanyama wengine walanyama porini. Hivyo mafundisho hayo yametusaidia kuuishi ubinadamu kama binadamu. Pia mapungufu kwenye mafundisho na utaratibu huo ni moja ya chanzo kilicho na kinacho chochea baadhi ya tabia na tamaduni ndani ya jamii ambazo ni vigumu kuzielezea. Kwani akili ya binadamu hupendelea kufanya yale yanayozuiwa kufanywa kuliko yale yanayo elekezwa kufanywa.

Sababu ya ukuaji wa haraka katika uelewa wa binadamu, kipindi hiki ni mda sahihi watu waelimishwe na waelewe kile wanacho kiamini au kuambiwa na siyo kuwaacha waendelee kuamini kila wasicho kielewa na wanacho ambiwa. Hivyo pale tusipo jua kama binadamu tukubali kuwa hatujui na siyo kuchukua kila dhana tusiyo ielewa na kuiamini, kitu kinacho endelea kutugawa katika makundi makundi. Katika hili itolewe elimu itakayo mfanya mtu binafsi ndani ya nafsi na kwenye maisha yake kukutana au kuzoea(experience) Nguvu iliyo ndani au nyuma ya Uumbaji, yeye kama yeye (practically and personally) na siyo kama ilivyo andikwa tu na kuishia kuamini maandishi. Mfano hapa Kati ya elimu nyingine nyingi, elimu ya yoga ipewe kipaumbele (zipo aina tofauti tofauti za yoga).

Siasa (uongozi) ; hiki ni kiungo cha muhimu sana katika jamii, kwani ndicho chombo kinacho amua kitu gani kisiwe au kiwe ndani ya jamii na kiweje. Siasa ikipuuzwa ikateleza basi jamii nzima imeteleza.

Maalumu Tanzania, mfumo wa uongozi tulio nao sasahivi (demokrasia) ni matokeo ya mifumo mbalimbali iliyopita. Sababu ya uhitaji na uelewa wa binadamu kwa ujumla,leo hii tupo katika mfumo wa uongozi wa watu kwa watu katika vyama vya kisiasa. Ukweli ulivyo kuwa kilicho kusaidia jana kinaweza kikakuponza kesho usipo kifanyia maboresho. Hivyo hivyo mfumo wa uongozi uliotusaidia baada ya ukoloni, unaweza ukatuponza mbeleni tusipoufanyia maboresho leo.

Sasa hivi uongozi umegawanyika katika makundi kulingana na itikadi za vyama vya kisiasa na siyo kutokana na mpango au malengo ya taifa, baadhi ya watu wanaongoza si kwa sababu wanauwezo wa kuongoza kwa ufasaha bali kwa sababu wanashabikia itikadi fulani. Mfumo huu ni hatari kwa Taifa na unatengeneza makundi kinzani ambayo athari zake ni kubwa na siyo rafiki kwa jamii yoyote inayotaka usawa na maendeleo ya kweli kwa wote.

Ni mda sahihi viongozi tuweke chini viburi(ego) tutengeneza serikali moja kulingana na uwezo wa watu bila kujali vyama vyao vya siasa, kwani sote lengo letu ni moja; kuleta maendeleo ndani ya jamii zetu. Mfano, Tanzania mbegu hii ya umoja imeishaanza kupandwa ; kwa kuteuliwa Mh. Queen Sendiga wa chama cha ADC kuwa mkuu wa mkoa pamoja na nafasi ya makamu wa Raisi wa Zanzibar kutoka upinzani. Hivyo ni jukumu letu sote kuilinda na kuiendeleza hii mbegu kabla hali haijawa tete na kutulazimisha kubadilika kwa lazima, nguvu na maumivu.

Kwa ujumla, elimu au ujuzi tulionao hudumaza au hukuza uchumi wetu unaoendana na imani zetu zinazosimamiwa na serikali zetu. Sisi ndiyo waamuzi wa haya yote penye uhitaji tufanye maboresho ambayo yatatengeneza mazingira sawa kwa binadamu wote ili kila mmoja awe na nafasi sawa kuwa kile anacho kitaka. Kama jamii yetu inao watu wanaotoa walivyo navyo ili watu wafikirie tofauti kupata hadithi za mabadiliko (stories of change), ni dhahili kuwa mabadiliko ni muhimu na yanaweza kutekelezwa ndani ya jamii zetu na kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa hali itakayoifanya dunia iwe katika uzani sawa.
 
Upvote 6
Sababu ya mipaka iliyo wekwa kama muongozo kwenye idadi ya maneno ya kutumia, nimejitahidi kuandika kwa ufupi bila kuathiri ujumbe kadiri nilivyo weza.

Hivyo pale utakapoona hauja elewa vizuri, uliza nielezee vizuri zaidi (usihitimishe kutokana na uelewa/mtazamo wako).

Au utakapo ona maelezo yamepungua, taja sehemu husika niongeze maelezo pamoja na mifano ili paeleweke zaidi.

Mwisho japo si kwa umuhimu, kama hauna swali na umeelewa andiko vizuri lipigie kura. Linaweza kuwa mbegu ya kuongeza zaidi usawa na mabadiliko bora kwenye jamii na Taifa letu kwa ujumla. Na!, Dunia ikaiga na kujifunza kutoka kwetu.

cosmic force.
πŸ™πŸΎπŸŒ³πŸŒ³...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…