Waititu kurudi Gerezani: Mahakama Kuu yathibitisha kifungo na yafungua tena mlango wa Mashtaka ya utakatishaji fedha

Waititu kurudi Gerezani: Mahakama Kuu yathibitisha kifungo na yafungua tena mlango wa Mashtaka ya utakatishaji fedha

Wakaguongo

Member
Joined
Sep 23, 2026
Posts
95
Reaction score
38
1792436424090.png

Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu, maarufu Baba yao, mkewe Susan Wangari Ndungu na washirika wao wamepata pigo tena baada ya Mahakama Kuu kuthibitisha hukumu zao katika rufaa iliyohusiana na ufisadi wa mkataba wa barabara wa shilingi milioni 588.

Katika uamuzi uliotolewa Oktoba 14, 2026, Jaji Rose Ougo alithibitisha hukumu na adhabu zilizokuwa zimetolewa dhidi ya Waititu na wenzake kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na ufisadi. Waititu alihukumiwa kifungo cha miaka 12 au kulipa faini ya milioni 52.749. Aidha alipigwa marufuku kugombea au kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa miaka 10.

Wengine waliohusika ni aliyekuwa Afisa Mkuu wa Barabara, Uchukuzi, Ujenzi wa Umma na Huduma za Kiambu, Luka Mwangi Wahinya, pamoja na Charles Chege Mbuthia ambaye ni Mkurugenzi wa Testimony Enterprises Limited.

Kesi hiyo ilitokana na uchunguzi ulioanzishwa mwaka 2019 kufuatia madai kwamba Serikali ya Kaunti ya Kiambu ilikuwa imetoa kwa njia isiyo halali mkataba wa milioni 588 kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited.

Mkataba huo wa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ulihusisha kuboresha barabara za changarawe kuwa barabara za lami katika maeneo ya Thika, Limuru, Gatundu North, Juja na Ruiru. Waititu na washirika wake walipatikana na hatia Februari 12, 2025, kwa makosa yaliyohusisha mgongano wa maslahi, na matumizi mabaya ya mamlaka ikiwemo aratibu zisizo halali za ununuzi.

Mali ya milioni 131.2 pia iliamriwa kutaifishwa:
Katika kesi tofauti ya mali isiyoelezeka, mahakama pia iliagiza mali zenye thamani ya takriban milioni 131.2 zinazohusishwa na Waititu na washirika wake kutaifishwa mnamo Desemba 2025. Mali hizo zilijumuisha majengo ya Thindigua, mashine ya Caterpillar, magari na mali nyingine zinazohusishwa na washukiwa na kampuni zinazohusiana nao. Aidha Tume ya Kupambana na Ufisadi(EACC) pia ina kesi tofauti ya madai ya kurejesha milioni 170 kutoka kwa Waititu na Testimony Enterprises Limited, ambayo bado inasubiri uamuzi.

Hatua inayofuata sasa:
Kwa mujibu wa EACC, suala la hukumu kuhusu makosa ya utakatishaji pesa limepangwa kusikilizwa kwa ajili ya kupunguza adhabu na kutoa hukumu Oktoba 19, 2026.

Hii ina maana kwamba uamuzi wa hivi karibuni umeimarisha hukumu zilizokuwepo, huku hatua ya hukumu kuhusu makosa ya utakatishaji pesa ikisubiriwa.

Je, kesi kama hii inaonyesha kuwa viongozi wanaohusishwa na ufisadi wanaweza kuwajibishwa hata baada ya kuondoka madarakani?

Kwa nini kesi za ufisadi wa fedha za umma huchukua miaka mingi kabla ya kufikia hatua za mwisho?

Lakini, kwa kufuatilia hili la Waititu, Je hukumu kali na kurejeshwa kwa mali ni njia bora zaidi ya kupambana na ufisadi kuliko kuwafunga wahusika pekee? Wewe unaonaje? Kwa sasa, Baba Yao anarudi gerezani.

1792436456139.png
 
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetangaza kuendelea na juhudi za kurejesha KSh170 milioni kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu uliodumisha hatia yake katika kesi ya ufisadi na kurejesha mashtaka ya utakatishaji fedha.

Katika taarifa ya Oktoba 15, 2026, EACC imekaribisha uamuzi wa Jaji Rose Ougo uliodumisha hukumu dhidi ya Waititu, mkewe Susan Wangari Ndung'u na washtakiwa wengine waliohusishwa na sakata la kandarasi ya ujenzi wa barabara katika Kaunti ya Kiambu.

Kesi hiyo ilitokana na uchunguzi ulioanzishwa mwaka 2019 kuhusu utoaji wa kandarasi ya KSh588 milioni kwa ajili ya kuboresha barabara za changarawe kuwa za lami katika maeneo mbalimbali ya Kiambu katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Waititu na washtakiwa wenzake walipatikana na hatia Februari 2025 kwa makosa yaliyohusisha mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa taratibu za ununuzi wa umma.

Katika uamuzi wa hivi karibuni, Mahakama Kuu pia ilibatilisha uamuzi wa mahakama ya chini uliokuwa umewaondolea baadhi ya washtakiwa mashtaka ya utakatishaji fedha. Kesi hiyo imepangwa kurejea mahakamani Oktoba 19, 2026, kwa ajili ya kusikiliza hoja za kupunguza adhabu na kutoa hukumu husika.

Kwa mujibu wa EACC, kesi tofauti ya madai ya kurejesha KSh170 milioni dhidi ya Waititu na kampuni inayohusishwa na sakata hilo bado inaendelea mahakamani. Tume hiyo inadai fedha hizo ni mapato yaliyotokana na ufisadi katika kandarasi ya barabara.

Hata hivyo, fedha hizo bado hazijarejeshwa, kwani mahakama haijatoa uamuzi wa mwisho kuhusu kesi hiyo ya madai.

Katika kesi nyingine iliyohusu mali ambazo chanzo chake hakikuelezwa, mahakama iliamuru kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya takribani KSh131.2 milioni mnamo Desemba 2025, zikiwemo mali za Thindigua, mashine ya Caterpillar na magari mawili.

Hatua hizi zinaibua mjadala kuhusu juhudi za kurejesha mali za umma zilizopatikana kupitia ufisadi na iwapo hukumu dhidi ya viongozi wa zamani zinaweza kusaidia kupunguza matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
 

Attachments

  • integrity-centre-eacc.jpg (1).webp
    integrity-centre-eacc.jpg (1).webp
    57.6 KB · Views: 18
  • ferdinand waititu jail.jpg.webp
    ferdinand waititu jail.jpg.webp
    50.5 KB · Views: 13
Back
Top Bottom