Habari za mda wanaJF,
Swala la kuweka transmission/gearbox neutral gari linapoteremka au ku-coast kwenye mwendo ni jambo tata sana. Na kila ulingo una hoja zake. Ila kiutaalam mambo yanasema je?
Kuna sababu kadha za kukataza tabia hii. Kwanza ni kupungua kwa msukumo wa mafuta - fluid pressure. Unapoweka mfumo kwa neutral, mzunguko wa engine hupungua hadi idling - <800 rpm. Pump ya gearbox hutegemea mzunguko ule wa engine kutoa msukumo wa kufaa mahitaji ya gari - kasi, mzigo na mwendo. Msukumo unapokua hafifu hakuna nguvu ya kukamata zile gear na kwa hivyo clutch huachilia. Unaporegesha gear kwenye mwendo mawili hutokea, mfumo hung'ang'ania kukamata gear huku msukumo wa mafuta ukiwa bado hujafikia kiasi kinachotakikana; na Pili pale kwa clutch kuna mzunguko mkubwa hasaa kwa upande upasao kua UNAZUNGUSHWA na mwenzake aliyekamata mzunguko wa engine - kumbuka kasi ya engine iko chini ukilinganisha hapa.
La pili ni ukosefu wa mzunguko wa mafuta kwa minajili ya kupoesha, kulainisha na kusuuza mfumo. Ukosefu huu huadhiri mfumo kwa kuuzorotesha bure. Gearbox mingi nilizofungua hazikosi alama za joto kupindukia - rangi ya blue kwa vyuma. Kukosa mafuta pia huongeza kukulana kwa chuma na uongezeko wa joto. Kutosuzwa vizuri hasaa kwa transmission za automatic husababisha kuongezeka kwa uchafu na habari za kuziba kwa mfumo.
Mfumo wa gearbox huzingatia mtindo wa 'synchronization'. Hii ni usawazishaji wa kasi ya mzunguko katika vitu viwili; hii ina maana kimoja kitaongeza kasi na/au cha pili kitapunguza kasi hadi pale usawa utapatikana na muungano/ukamataji ufannyike bila mishtuko isiofaa. Hii ndio pia sababu kunatumika clutch lakini kwa pekee haikidhi mahitaji ya synchronization, mle ndani ya gearbox(manual) yale meno yana 'syncro' ambazo husawazisha kasi vikamilifu. Katika mfumo wa automatic, muundo wake na ubadili gear ni wa overlapping - yaani gear ya pili huingia kabla ya kwanza KUWACHILIA KABISA - hii ndio sababu gear huskika kujivuta pale ya pili 'inapochelewa kuingia'. Hapa basi, synchronization hufanyika kwa mtindo na utaratibu kulingana na kasi ya gari kwa mda; hivi ni kusema kasi ya engine ikipungua/mskumo wa mafuta, gear hushuka LAKINI kumbuka kuna speed sensor ambayo inatoa habari tofauti?!?! Hapa basi mfumo uchanganyikiwa na, ukazua code kama ni wa umeme na/au ukajikanganya upande wa valve body.
Sababu ya tatu na ya muhimu sana ni usalama wa gari barabarani au uhakika wa kuidhibiti pale. Tuchukue gari dogo la magurudumu manne kwa mfano wetu. Linapokua likitembea likiwa neutral, gari letu linasonga kwa magurudumu yasiohusiana ila kwa kufungiliwa kwenye gari letu; kila moja huru. Hii ni kumaanisha mguu mmoja au miguu ya upande mmoja ikikanyanga sehemu telezi, upande huo utaongeza kasi kuliko upande wa pili na hapo basi gari likapoteza mwelekeo. Gari likiwa na gear, miguu inayozungushwa - iwe ya nyuma, mbele au yote minne, imeungana kupitia zile shaft na mifumo ya diff, hadi kwa transmission/gearbox yenyewe hapo basi mmoja au miwili ikibadili (kupunguza au kuongeza) kasi, itabidi yote (miwili au minne) ibadili hapo hapo na kwa hivyo kuzuia kupoteza mwelekeo.
Madereva pengine wawewza uliza breki vipi? Kuna ushahidi tele kudhibitisha mifumo ya breki haikamati sawa hata kwa mguu mmoja matukio mawili!!! Hii ndio sababu kukavumbuliwa mifumo ya ABS, ASR, VSC n.k.