SoC02 Elimu Bora ilenge kutimiza mambo manne kwa mwanadamu

SoC02 Elimu Bora ilenge kutimiza mambo manne kwa mwanadamu

Stories of Change - 2022 Competition

PrMujuni

New Member
Joined
Aug 3, 2022
Posts
1
Reaction score
2
ELIMU BORA ILENGE KUTIMIZA MAMBO MANNE KWA MWANADAMU.

Na PrMujuni

ELIMU BORA inahitajika sana na kila siku inaimbwa na wanaharakati wa kisiasa na kijamii. Leo nakuja na wazo kuwa ELIMU yoyote iliyo Bora inapaswa kutimiza malengo makuu manne kwa mwanadamu. Nitatumia msitari wa Biblia kufafanua hili maana hiki ndicho Kitabu cha kale kuliko vitabu vyote kwa Imani yangu.

Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Luka 2:52 kwa Mujibu wa fungu hili mambo yaliyomkuza Yesu yalikuwa manne yaani

1. Hekima
2. Kimo
3.Kumpendeza Mungu
4. Kuwapendeza wanadamu


HEKIMA
Kulingana na Wikipedia, kamusi elezo huru inasema Hekima ni hali bora ya mtu katika kutambua ukweli wa binadamu, vitu, matukio na mazingira mbalimbali hata kuchagua vizuri la kufanya. Hivyo Hekima ni uwezo wa kutumia maarifa uliyonayo kwa namna inayokubalika kuchagua na kufanya vitu sahihi kulingana na kanuni na sheria zilizopo.Hivyo ELIMU BORA ni lazima ilenge kukuza hekima ya watoto yaani upanuzi wa maarifa na matumizi yake katika maisha halisi. Hii inawezekana pale tutakapobadilika na kugundua kuwa wanadamu wameumbwa tofauti kwa hekima za Mwenyezi Mungu na hivyo haina haja ya kumfundisha Tembo, twiga, Nyani na Sungura kwa namna Ile Ile na kuwapima kwa mtihani mmoja wa aliyefaulu ni yule aliyepanda hadi juu ya mti wakati una uhakika kuwa Tembo, twiga na Sungura hawawezi kupanda mti kama Nyani.

KIMO
Kimo ni ukuaji wa kimwili na viungo vyake. ELIMU ya kweli ilenge kutambua na kuwaelezea watoto masuala ya makuzi ya viungo vyake vya mwili. Mapema watoto wafundishwe majina halisi ya via vya uzazi na utofauti wa via vya uzazi vya kike na kiume na masuala ya ngono na hatari zake.na pia kuelezwa umuhimu wa maeneo yanayoitwa SEHEMU ZA SIRI na kwamba maeneo hayo ni nyeti sana kwamba hakuna mtu anayetakiwa kuwagusa au kuwashika maeneo hayo na kwamba huo ni uharifu mkubwa mpaka wanapoingia katika ndoa hivyo wao wasiwafanyie wengine wala wasikubali kufanyiwa Chochote na mtu mwingine na kama ikitokea wafanyeje. Jamii ifundishwe namna ya kumtambua mtoto aliye katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya kikatili. Hii itasaidia kupunguza masuala ya ulawiti na ngono za utotoni na athari za ngono na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.

AKIMPENDEZA MUNGU
Hii inalenga kukuza Imani ya watoto kwa Mwenyezi Mungu. Moja kati ya vitu hatari katika jamii yetu ni kuwa na ELIMU isiyohusisha masuala ya dini katika makuzi ya mtoto. Kwa mujibu wa sheria za nchi, Serikali haina dini ila watu wake wana dini. Masuala ya dini mashuleni hayatiliwi mkazo sana. Ni hiari watoto kwenda kwenye vipindi vya dini au la. Na hata wale wanaojitajidi kuhudhuria vipindi na masomo ya dini, masomo hayo japo yanatungiwa mtihani wa taifa ila hayana maana kwa Masomo ya mbeleni. Niliwahi kusikia vyuo vinapotangaza nafasi za kujiunga navyo mfano vyuo vya Afya, wanasema "mhitimu awe na D katika masomo ya sayansi na D ya somo lolote isipokuwa somo la dini." Hii maana yake inawafanya wanafunzi wasio umuhimu wa masomo ya dini mashuleni. Na hivyo tunazalisha watu wasio na hofu ya Mungu na kama hawana hofu ya Mungu maana yake hawa watakuwa ni wafanyakazi wasio na maadili ya kazi maana hawana hofu ya Mungu. Hii inapelekea kuwa na watu wala rushwa, mafisadi, wanaotetea vyeo hata kwa kuumwa wanaoonekana kuhatarisha vyeo vyao. Ni muhimu masomo ya dini kutiliwa mkazo mashuleni kama yalivyo masomo mengine.

AKIWAPENDEZA WANADAMU
Wanadamu ndio jamii. Kila mwanafunzi afunzwe mapema kuwa elimu anayoipata inapaswa kuleta matarajio chanya kwenye jamii yake. Aelewe wazi atafanya kazi kwa ajili ya watu hivyo afanye kazi Kwa uzalendo wa nchi yake na watu wake.

ELIMU ilenge kuleta manufaa kwa jamii sio manufaa ya mtu binafsi. Ieleweke wazi kuwa daktari na wauguzi wapo kwa vile kuna wagonjwa. Mfanyabiashara yupo kwa vile kuna wateja. Hivyo hizi kazi zote tulizonazo ni kwa ajili ya watu wengine, tunapaswa kuwaheshimu na kuwahudumia kwa upendo na kuwajali maana hao ndio kama waajiri wetu.


HITIMISHO
ELIMU ya kweli ilenge kutimiza maeneo hayo manne kwa maisha ya mwanadamu, kukosekana kwa kipengele Chochote kati ya hivyo vinne hufanya mwanadamu kupungua.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom