SoC02 Elimu nchini ikombolewe kwanza ili iweze kumkomboa Mtanzania

SoC02 Elimu nchini ikombolewe kwanza ili iweze kumkomboa Mtanzania

Stories of Change - 2022 Competition

ReTHMI

Senior Member
Joined
Jul 17, 2022
Posts
181
Reaction score
323
1658773373178.png
Elimu hutumika kumkomboa mtu kifikra, kimwili, kijamii na hata kiroho. Lakini uimara wa namna elimu itolewavyo huweza kumkomboa au kumdidimiza zaidi mtu. Elimu ya Tanzania bado ina mapungufu mengi sana yanayoifanya ilegelege katika ukombozi wa mtanzania. Ni vyema kuikomboa kwanza kwa kuyapunguza/kuyaondoa mapungufu hayo.

Kwanini elimu ikombolewe?
Elimu ikikombolewa tutaepukana na matatizo haya kwenye jamii za watanzania;
  • Ukosefu wa ajira kwa idadi kubwa ya wahitimu​
  • Vyuo kuzalisha wahitimu wasio na ujuzi wa kutosha​
  • Idadi ndogo ya wataalamu katika sekta mbalimbali​
  • Wahitimu kuhitimu katika umri mkubwa​
  • Ukuaji mdogo wa sayansi na teknolojia​
  • Umaskini uliokithiri kwenye jamii​
  • Ushiriki mdogo wa wananchi katika mambo mbalimbali ya kitaifa na kijamii​
  • Changamoto ndogondogo kwenye jamii kama ukosefu wa maji safi na salama na njia dhaifu katika kilimo na ufugaji​
Matatizo haya huchangia kwa kikubwa katika ukuaji mdogo wa uchumi wa mtu mmojammoja na uchumi wa taifa kiujumla. Pia huleta changamoto kubwa sana katika upatikanaji wa serikali yenye viongozi bora walio mstari wa mbele katika kutatua matatizo ya nchi na jamii anayoishi mwananchi.

Nini kifanyike ili kuikomboa elimu?
Ili kuimarisha elimu inahitajika ushirikiano mkubwa baina ya serikali na wananchi utakaosaidia kujua ni changamoto gani zilizopo kwenye mtaala na mfumo wa elimu na njia zipi zitumike kumaliza changamoto hizi. Zifuatazo ni baadhi ya njia zitakazoweza kuimarisha elimu ya Tanzania kiujumla;

1. Kuwekeza fedha ya kutosha katika elimu.
Baadhi ya shule nyingi nchini zina changamoto ya idadi ndogo ya madarasa, meza na viti ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo kwenye shule hizo. Hali hii hupelekea msongamano mkubwa darasani kitu ambacho kinamfanya mwalimu ashindwe kufanikisha malengo yake ya ufundishaji kwa kila mwanafunzi. Shule nyingine zina ukosefu wa vitabu kitu ambacho kinampa ugumu mwanafunzi katika kujifunza zaidi. Ukosefu wa maabara na vitendea kazi vingine humfanya mwanafunzi kushindwa kujifunza kwa vitendo hali inayopelekea kuzalishwa kwa wahitimu wasio na ujuzi wa kutosha.

Ni vyema serikali ikitoa kiasi kizuri cha pesa kwenye sekta ya elimu ili kusaidia kuboresha miundombinu ya shule nchini pamoja na kuhakikisha kila shule ina vitendea kazi vya kutosha katika kufundishia. Pia iajiri waalimu wa kutosha na kuwalipa malipo mazuri ili kuhakikisha idadi ya wanafunzi shuleni inaendana na idadi ya waalimu na malipo yanawaondolea ugumu wa maisha waalimu.

Pia serikali ihakikishe inapambana kuhakikisha inafuta dhana ya kua taaluma ya ualimu ni watu waliofeli au wenye ufaulu mdogo. Iwekeze kwenye kuzaliza waalimu kutokana na wanafunzi bora zaidi. Nchi ya Finland ambayo mfumo wake wa elimu una viwango vya juu vya ubora duniani, waalimu wenye elimu ya chini nchini humo wana shahada ya ualimu (Barchelor Degree) ambao hufundisha elimu ya awali, wengi wa waalimu nchini humo wana kiwango cha elimu cha shahada ya uzamili (Masters).

Tanzania inaweza kuiga kutoka Finland na kuacha kutoa nafasi kwa wanafunzi waliopata ufaulu mdogo kusomea ualimu. Ikumbukwe mwalimu ndiye anayezalisha taaluma zote kwenye jamii, kwaiyo mwalimu akiwa na uwezo mdogo basi itegemewe atazalisha wahitimu wenye ujuzi mdogo.

1658773612223.png
2. Kurekebisha/kubadili mfumo wa elimu
Mfumo wa elimu ya Tanzania ni janga kubwa sana katika kuhakikisha ubora wa elimu nchini. Tanzania ijifunze kwenye nchi nyingine kama Finland iliyo na ubora mkubwa katika sekta ya elimu duniani. Nchi iangalie ni nini kinawasaidia Finland kua vizuri kielimu, na ni vitu gani inaweza kuiga kutoka kwenye elimu yao vitakavyoweza kuboresha mfumo wa elimu ya Tanzania.
1658773708741.png
Katika kutengeneza mfumo mzuri wa elimu nchini vitu hivi viangaliwe kwa umakini wa hali ya juu;
  • Lugha ya kufundishia; Mfumo wa elimu ya Tanzania hutumia lugha ya kiswahili kwa upande wa shule za msingi na lugha ya kingereza kwa upande wa shule za sekondari katika ufundishaji. Hii ni changamoto kubwa sana inayomfanya mwanafunzi kuona masomo ni magumu pale anapokutana na lugha ya kingereza sekondari. Hii hupelekea wanafunzi wengi waliokua na uwezo mzuri kwenye shule ya msingi kukata tamaa na kupata ufaulu mdogo kwa upande wa sekondari.​
Ni vyema ikitumika lugha moja kufundishia kuanzia mtoto anapoanza shule ya msingi mpaka anapohitimu chuoni. Kama ni lugha ya kiswahili basi itumike kuanzia ngazi ya chini mpaka vyuoni katika kufundishia huku lugha ya kingereza ikifundishwa kama somo. Hivyohivyo kama nchi itaamua kutumia lugha ya kingereza basi itumike kufundishia kuanzia shule ya msingi mpaka vyuoni huku lugha ya kiswahili ikifundishwa kama somo. Hii itasaidia kuepusha mkanganyiko kwa wanafunzi kutokana na kubadilishiwa ghafla lugha ya ufundishaji.
  • Njia za ufundishaji; nchi ya Finland inaamini mwanafunzi anajifunza zaidi nje ya shule kuliko akiwa shuleni, hivyo wanafunzi hutumia muda mdogo shuleni. Finland hutumia chini ya saa 20 kwa wiki katika kufundisha ilihali Tanzania hutumia zaidi ya saa 30 kwa wiki katika ufundishaji ukiachana na masomo ya ziada. Mwanafunzi kutumia muda mwingi darasani hupelekea mambo yafuatayo;​
  • Mwanafunzi kushindwa kujifunza mambo muhimu kwenye jamii​
  • Kushindwa kutambua ubunifu na vipaji vya wanafunzi kupitia kazi za ziada shuleni​
  • Mwanafunzi kushindwa kufanyia kazi elimu yake kwenye jamii​
Pia njia za ufundishaji ziegemee zaidi kwenye ufundishaji wa vitendo kuliko nadharia. Ni kitendo cha kusikitisha sana kwa mwanafunzi anayesoma somo la kilimo Tanzania lakini haingii shambani kuonyeshwa kwa vitendo. Ufundishaji kwa njia ya vitendo utasaidia watu wengi kua na ujuzi mbalimbali hata pale wanapoishia katika ngazi ndogo za elimu.
  • Uhitaji wa soko la ajira; Idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni iendane na uhitaji wa wataalamu katika sekta mbalimbali. Kudahili wanafunzi wengi wa taaluma fulani bila kuzingatia uhitaji wa soko la ajira hupelekea kuongeza tatizo la ajira nchini. Tanzania inaweza kuliepuka hili kwa kuweka mikakati madhubuti katika mfumo wa elimu nchini.​
  • Uhalisia/uhitaji wa jamii ya mtanzania; Mtaala wa elimu ni vizuri ukiendana na mahitaji ya jamii husika kwani itasaidia wahitimu kuweza kupambana na changamoto mbalimbali kwenye jamii. Kuliko mwanafunzi kusoma masomo mengi yenye vitu vingi visivyo na manufaa kwenye jamii yake, ni bora kumpunguzia mzigo kwa kusoma vitu vichache vitakavyoisaidia jamii yake.​
Hivyo basi, ni vyema kuboresha elimu inayotolewa nchini kwa kujifunza kupitia nchi nyingine zinazofanya vizuri kwenye sekta ya elimu. Elimu ipelekee matamanio ya kujifunza zaidi kwa wanafunzi, na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kutosha kupambana na matatizo yaliopo kwenye jamii zao. Tanzania itengeneze mfumo wa elimu utakaoboresha maisha ya wananchi wake na sio huu mfumo uliopo wakati huu unaoongeza matatizo kwenye jamii kama ukosefu wa ajira kwa wahitimu na huduma mbovu kwenye jamii.
1658774281208.png
 
Upvote 22
Karibuni Wana JF kwa maoni na marekebisho
Ukivutiwa na andiko hili usisite kunipigia kura kwa kugusa alama ya
^ iliyopo mwishoni kabisa mwa andiko hili
 
Back
Top Bottom