SoC02 Elimu ya malezi na makuzi ya mtoto

SoC02 Elimu ya malezi na makuzi ya mtoto

Stories of Change - 2022 Competition

Adam Memba

New Member
Joined
Jul 26, 2022
Posts
1
Reaction score
1
Kwanza kabisa ningependa kushukuru kwa fursa hii adhimu katika jukwaa la uandishi wa STORY OF CHANGE 2022. Kwa upande wangu nitajikita katika Nyanja ya elimu, na kwa namna ya pekee nitajielekeza katika elimu ya malezi na makuzi ya mtoto jambo ambalo kwa hali ilivyo kwa sasa ya zama za utandawazi hakuna atakayepinga nikisema kundi hili lipo hatarini sana kuliko wakati mwingine wowote pengine. Ili kupata picha halisi ya jambo lenyewe tujiulize swali hili:

Je, ni mzazi au mlezi gani ambaye anaweza kuwa huru bila wasiwasi na kuendelea na shughuli zake huku akiwa amemuacha mwanae kwa jirani,dada wa kazi au mtu wa ukoo?

Ikiwa ndivyo tatizo ni nini?

Sasa tujadili suala hilo kwa kina.

Mtoto ni nani?

Haki zake ni zipi?

Sasa kwanini tuzungumzie kwa kina kuhusu elimu ya malezi na makuzi kwa mtoto?
Ni vema nikajibu maswali haya kwa umakini upana wake kuanzia Nyanja za kimataifa (kidunia),kitaifa na kijamii(ngazi ya familia) ili tuone umuhimu na uzito wa elimu ya malezi na makuzi ya kundi hili lililo katika hatari kubwa.

Mtoto ni nani?

Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na mkataba wa kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 inasema"mtoto ni kila binadamu aliye chini ya umriwa miaka 18.” Kwa kutambua ubinadamu wao ndiyo sababu sheria inawatambua na kuhakikisha yafuatayo kwao: wana haki sawa na wengine,wanapaswa kuwa na sauti(wasikilizwe)na kupatiwa ulinzi-yaani mazingira salama ya kuishi pasipo kuhatarishwa kwa namna yoyote ile.

Hii ndiyo sababu mnamo Novemba,1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mkataba wa haki za mtoto na nchi yetu ilikubali mkataba huu Julai 10, 1991. Huyo ndiyo mtoto anavyotambuliwa duniani kisheria.

Haki zake ni zipi? Huenda kila mtu angeweza kutaja orodha ndefu ya haki zinazomuhusu mtoto kulingana na uelewa wake kuzihusu ikiwa angeulizwa swali hili na huenda ikawa yupo sahihi kwa asilimia kubwa sana, lakini hapa ningependa kuorodhesha baadhi ya haki za msingi.

 Kupatiwa elimu
 Kupatiwa ulinzi/kulindwa
 Haki ya kumiliki mali/kurithi
 Kusikilizwa/kushirikishwa
 Kutokubaguliwa kwa muonekano au jinsi yake.
 Malezi bora ili kusaidia ukuaji wa kiakili na kimwili.
 Kupata muda wa kucheza na kupumzika.

Lengo la uwepo wa haki hizi ni kuhakikisha kwamba mtoto anakua katika mazingira salama yanayomjenga kuwa mtu mzima anayetegemeka siku za usoni, kuwa baba au mama bora na viongozi bora kwa jamii na taifa kwa ujumla na hata kupunguza matukio ya ukatili au ikiwezekana kuondoa kabisa aina ya watu wasiojali utu wa mtu katika jamii na kufanya dunia kuwa mahali salama kwa kuishi.

Sasa kwanini tuzungumzie kwa kina kuhusu elimu ya malezi na makuzi kwa mtoto?
Katika kujibu swali hili muhimu kabisa ningependa kutumia mifano halisi ya eneo au jamii inayonizunguka na ninayoshirikiana nayo kwenye shughuli za kila siku. Ukweli ni kwamba ni watu wachache sana wenye mwamko na mtazamo chanya kuhusu elimu ya malezi na makuzi kwa mtoto na wazazi na walezi hili ni jukumu lenu la kwanza.

Hii ni kutokana na matukio ya ukatili yanayoripotiwa kila siku kwenye vyombo vya habari na yale tunayojionea kwenye maeneo tunayoishi. Ili kuweka sawa jambo hili ningependa kutumia jedwali hili kufafanua ukatili wanaopitia watoto wenye umri kati ya 7 hadi 17 kulingana na utafiti wangu nilioufanya kwa kipindi cha miaka miwili(2021-2022).
Mshambuliaji Wasichana(wahanga) Wavulana(wahanga).

Jirani 30.2% 18.6%
Mtu asiyejulikana 35.0% 6.7%
Rafiki/mwanafunzi 12.3% 8.6%
Ndugu wa ukoo 20.1% 14.7%

Hii ni kwa eneo ninaloishi tu, je hali ipoje katika maeneo mengine? Bila shaka jibu tunalo kuwa hali ni mbaya sana. Na tusisahau idadi ya visa vya ukatili kwa watoto vinavyoripotiwa ni kidogo sana ikilinganishwa na vile visivyoripotiwa ambavyo vinamalizwa kifamilia au kienyeji bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Swali ni kwanini hali ipo hivi?

Jibu ni kwa sababu jamii haina uelewa sahihi juu ya malezi na makuzi kwa mtoto hali inayopelekea kundi hili kukosa ulinzi na kuishi kwa wasiwasi.

Tugeukie suala la elimu kwa ujumla: suala la elimu kwa jamii ni suala mtambuka, pamoja na jitihada za serikali kuboresha maeneo ya kufundisha na kujifunzia bado kuna maeneo yanayohitaji kutazamwa kwa jicho pevu hasa maeneo ya vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watoto wanaohitaji kupata elimu bora kama watoto wengine waishio katika maeneo ya mjini.

Ili kufanikisha hilo ninapendekeza utafiti ufanyike hasa kwa jamii za wafugaji ambao bado wanahitaji hamasa kubwa sana na elimu ya ziada ili kubadilisha mitazamo yao iliyojengwa kwa muda mrefu na mila, tamaduni, miiko na desturi zao zilizokita mizizi akilini mwao(change mindset).

Mfano kwa jamii za kimaasai ambazo ndizo mpaka sasa ninapoandika andiko hili sote tunakubaliana kwamba ndiyo jamii pekee inayodumisha mila, hata msanii wa kizazi kipya wa kimaasai hayati Mr Ebo aliwahi kuimba katika wimbo wake “mi Mmasai bwana”. Inapohusu elimu hali ipoje?

Sina hakika maeneo mengine ambako jamii hii inapatikana lakini hapa Morogoro kuna eneo linaitwa Maasai Ndama kata ya Msongozi wilaya ya Mvomero hali niliyoikuta huko wakati wa tafiti zangu inasikitisha kwani watoto wengi wenye umri wa kwenda shule hawana fursa hiyo kabisa matokeo yake umri unapita na hivyo kuna haja ya kuanzishwa kwa elimu ya watu wazima.

Sababu kubwa ni umbali wa shule ilipo, muamko wa jamii husika maana yake ni kwamba jamii haihusishwi kushiriki na kupanga mipango ya elimu na mwisho mapokeo yao hasa ukirudi nyuma kutazama mfumo wao wa kiutawala. Habari njema ni kwamba baada ya kugundua sababu taasi zisizo za kiserikali zilifanikiwa kuifikia jamii hii na kusaidia kupunguza changamoto hizo katika eneo hilo. Mpaka sasa naandika andiko hili kumejengwa shule shikizi(satellite school) na kutumia waalimu wa kujitolea kwa uthibitisho wa andiko hili nitaambatanisha picha ili kuonesha uhalisia wa jambo hili.

Mwisho kabisa rai yangu ni kwamba bado kuna umuhimu na uhitaji mkubwa katika jamii wa elimu katika Nyanja kuu mbili, (1). Elimu kuhusu malezi na makuzi kwa mtoto (2). Elimu ya msingi kwa watoto wa jamii zote hasa zile jamii ambazo hazina muamko mkubwa kuhusiana na elimu,lakini pia ili kufanikiwa kwa mambo haya mawili ni muhimu sana kuihusisha jamii katika kupanga na kushiriki miradi au mipango ya kimaendeleo katika jamii husika.

Ahsante

Imeandikwa na
ADAM STANFORD MEMBA.
Simu: 0754009033/0623824070.
Email:adammemba2@gmail.com

#Picha chini ni Kwa hisani yangu mwenyewe.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom