SoC02 Elimu ya mtoto wa Kitanzania

SoC02 Elimu ya mtoto wa Kitanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Peterking1

New Member
Joined
Jul 27, 2022
Posts
3
Reaction score
1
ELIMU YA MTOTO WA KITANZANIA

Na Julius Peter

Ni asubuhi tulivu ikiwa ni saa 12:00 ya asubuhi hii, natoka kwenye makazi yangu na kuelekea barabara kuu ili kuweza kupata usafiri wa kuelekea katika shughuli zangu za kila siku. Kwa mwendo wa dakika chache najikuta tayari nimefika katika kitu cha magari ya umma maarufu daladala. Nikiwa hapo nakutana na kundi kubwa la watu wazima wakisubiri usafiri huo wa umma na huku pia kundi kubwa la wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wakiwa hapo.

Mara daladala unafika kituoni hapo na kondakta akipiga kelele za kutangaza uelekeo wa safari. Watu wazima kwa msongamano mkubwa tunagombea kuingia huku wanafunzi nao wakijaribu kujipenyeza. Mara inasikika sauti ya kondakta akisema "wanafunzi sipakii, ninao wengi sana humu". Mlango unafungwa na dereva akiondoa gari huku idadi kubwa ya wanafunzi wakibaki pale kituoni.

Kwa haraka najaribu kuwa itakuwaje kwa wale wanafunzi waliobaki pale kituoni? Je, watapata gari la kuwafikisha shuleni? Je, watawahi vipindi shuleni? Lakini je pia watarudi nyumbani kwa wakati? Hapa ndio najaribu kupiga picha ya elimu inayotolewa kwa watoto wa kitanzania toka tulipopata uhuru mpaka sasa.

Katika hali ya kawaida, elimu inayotolewa kwa watoto wa kitanzania ina changamoto kubwa. Tena hasa ile elimu inayotolewa na kusimamiwa na serikali, yaani shule za serikali maarufu kama "kayumba". Upande huu ni elimu wa shule za serikali zina changamoto kubwa bado kiasi hazimsaidii mtoto wa kitanzania kuweza kupata japo uwezo wa kukabiliana na dunia ya sasa.

Kuna mambo mengi bado yamekuwa ni mwiba kwa mtoto wa kitanzania kufurahia shule na kuipenda ili tu aweze kufanya vizuri. Mambo kama usafiri, miundombinu ya shule, mitaala ya elimu inayotolewa, mada zinazofundishwa, lugha inayotumika kufundishia, kwa njia moja ama nyingine vimekuwa ni uzio kwa mtoto wa kitanzania kutoweza kutoka katika kupambana na hali ya maisha ya dunia huko nje.

Ikiwa watoto wa kitanzania (walio wengi) ambao wanasoma katika shule hizi za serikali hawawezi kupata usafiri kwa urahisi wa kuwapeleka na kuwarudisha majumbani kama vile inavyofanyika kwa shule binafsi zinazomilikiwa na taasisi ama na watu binafsi. Je, wanaweza kweli kukabili ushindani wa kimasomo ndani ya nchi yao, nchi moja yenye amani, upendo na uzalendo wa kipekee hapa duniani. Hapa ndio unapoanza kuona tabaka lililopo kati ya watoto wa wenye uwezo na watoto wa masikini.

Lakini pia vipi kuhusu huko shuleni wanakofika tena kwa kuchelewa. Idadi ya wanafunzi katika darasa husika, idadi ya wanafunzi zaidi ya 40 katika darasa moja na mwalimu mmoja wa somo husika katika shule, ni uzio mwingine wa kumfanya mtoto wa kitanzania asione mwanga ulio wazi katika kupata elimu. Bado miundombinu ya shule haitoshelezi kumfanya mtoto wa kitanzania aweze kuwa katika hali ya ushindani wa kielimu japo kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki hasa kwa shule za msingi na sekondari.

Hapa ndio ninapopiga jicho langu kwenye mitaala ya elimu. Mitaala inayoandaliwa ni kama mitaala ya zima moto kwani kila mtawala ama kiongozi wa eneo la elimu anapoingia anakuja na taratibu zake. Kwa kipindi kifupi tu utakuwa mabadiliko yanafanyika mara kwa mara kiasi kwamba mtu anashindwa kujua ninj hasa uelekeo wa elimu hii kwa mtoto wa kitanzania. Leo utasikia watawala wanasifia ujenzi wa madarasa katika nchi nzima, lakini hawaangalii mitaala inavyoandaliwa kama inaendana na mahitaji ya nchi na mahitaji ya dunia ilivyo.

Ukija kwenye lugha ya kufundishia nako unakutana na uzio mwingine tena huu unapelekea matabaka kati ya wanafunzi wanaosoma shule ya serikali na wanaosoma shule binafsi. Kwani kwa shule za serikali huko darasa la awali mpaka la saba watumia lugha ya kiswahili na kingereza ni somo tu; ili hali kwa zile shule binafsi wanatumia lugha ya kingereza kufundishia na kiswahili kinabaki kama somo tu. Hawa wote hatimaye humaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza. Hawa wote wanakutana kule huyu anajua kiswahili sana na yule anajua kingereza sana la lugha ya kufundishia ni kingereza. Wanafunzi wengi toka shule za serikali huofia sana lugha ya kufundishia wanapoingia kidato cha kwanza na hapo hupelekea hofu na anguko la ndani la kuleta ushindani.

Hapa ndio najiuliza kwa nini iwe hivi? Hapa ndipo unapoona tabaka la kufanya vizuri darasani. Ni kama vile kuna kundi fulani linaandaliwa kuwa watu waliofanikiwa kwa wingi na kundi lingine la wachache ni kama wanaandaliwa kuwa watu hali ya maisha ya kati. Kwa nini tuegemee tu kwenye juhudi ya mwanafunzi husikq badala ya kumuandalia miundombinu itakayomsadia kumsukuma mbele zaidi. Imefika wakati sasa ni vyema serikali ikafanya maamuzi stahiki aidha kutumia lugha ya kiswahili ama kwa kingereza kwa shule zote iwe ni binafsi ama za serikali.

Lakini pia ni vyema kuangalia upya mitaala ya kutolea elimu. Ichambuliwe upya na kuangaliwa kama inajitosheleza zaidi katika kuhakikisha mtoto wa kitanzania anaapomaliza shule ya msingi ama sekondari anatapa mwanga wa kuyaishi maisha yanayomkabili.

Hali ya usafiri ya watoto wa shule za selikali itazamwe pia ili kusaidia watoto hawa kufika shuleni pamepa na kurudi majumbani mwao mapema pia. Tena hili lifanyike japo kwa kila njia kuwepo na magari makubwa japo matano yatakayoweza kubeba wanafunzi tu.

Pia mada zinazofundishwa mashuleni ziangaliwe kama zinafaa katika dunia ya sasa yenye kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mada ziwe rafiki ili japo watoto wetu waweze kuwa wavumbuzi wa mambo mbali mbali ya kimaendeleo. Naamini kuwq ikiwa serikali itakaa chini na kuamua sasa elimu inayotolewa kwa watoto wa kitanzania iwe bora, hilo halitawashinda. Nasema hivi kwa sababu ni kama kuna mahali kuna kusita hivi kuchukua hatua na maamuzi.

Mwisho kabisa ni vyema sana maslahi ya walimu yaboreshwe. Ni kweli nchi nyingi za Afrika zina hali ya uchumi usio imara sana, lakini pamoja na hayo katika hali hiyo hiyo walimu wapewe vipaumbele vya maslahi. Ninaamini ikiwa misingi itafumuliwa na kuangaliwa upya katika maeneo yote ya kutolea elimu, basi elimu ya Tanzania siku moja itafanya Tanzania kuwa nchi tajiri yenye uchumi wa juu zaidi.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom