SoC02 Elimu ya sasa kwa vizazi vijavyo

SoC02 Elimu ya sasa kwa vizazi vijavyo

Stories of Change - 2022 Competition

Msafiri 2018

New Member
Joined
Jan 18, 2018
Posts
2
Reaction score
0
Elimu ni sekta muhimu sana katika nchi, hutazamwa pia kama ni sehemu inayozalisha wabeba maamuzi wenye taaluma mbalimbali na inapotokea kuonekana kuwa na changamoto, mapitio mapya yanayoweza kuchanganua mwenendo wa kielimu katika taifa.

Mataifa ambayo yanajitabanaisha kuwa na elimu bora yamekuwa yakiweka mipango na kuifanyia kazi katika kipindi cha miaka mitano au chini ya hapo.

Ukuaji wa sayansi na teknolojia ulimwenguni ni kati ya vyanzo vikubwa vya mabadiliko ya elimu ukiachana na siasa ambapo ndio maamuzi mengi yanafanyika. Elimu ya nadharia inayopewa kipaumbele kuliko vitendo zaidi jambo ambalo ni hatari sana kwa Dunia ya sasa ni moja ya changamoto.

Hapa nitagusia mambo matano makuu ya kufanyia kazi ili elimu na wanaoelimishwa waweze kuwa bora zaidi hapa nchini Tanzania.

Elimu kwa vitendo, inabidi iwe kipaumbele cha kwanza katika kufundisha, kwani itaongeza chachu ya upatikanaji na ukuaji wa stadi za maisha,si kwamba hakuna taasisi za elimu ambazo zinafanyia kazi ufundishaji kwa vitendo la hasha!,swali ni kwamba ni kwa ubora upi? vigezo vinafuatwa? takwimu zinasemaje katika hao ambao wamepita kwenye mafunzo ya aina hayo kuanzia elimu ya awali mpaka chuo? .

Katika mahojiano yangu na Waziri wa Elimu wa Ureno Prof Coao Costa baada ya kongamano la elimu la Schools 2030, alibainisha kuwa ufundishaji Bora na wenye lengo la kutengeneza wajenga nchi wa taifa unapaswa kuchochewa na walimu wenye ari ya kufundisha, kukubaliana na mabadiliko yanatokea ama kuikumba Dunia.

Ufundishaji kwa kulinganisha na yale yanayofanyika kwenye jamii za wanafunzi zitawaibua katika kuwa na shauku zaidi. Huenda walimu wakawa hawana uelewa wa kina kutengeneza darasa la kiubunifu na ushirikishwaji wa wanafunzi, majukwaa ya elimu na serikali ni muhimu kusaidia katika kuanzishwa kwake katika kuwaendeleza walimu.

Katika kipindi chote mwanafunzi anaposoma shauku yake inamalizwa na viboko na pia kukanywa ili tu akione anachokiuliza au kukifanya hakifai na kuhesabiwa ni utovu wa nidhamu kumbe ni jambo la kulipigilia msumari na kumsaidia mwanafunzi.

Msingi wa ufundishaji kwa vitendo hauanzi mashuleni tu Bali majumbani pia msisitizo huu inapaswa kuangaliwa, kwanini nimezungumzia majumbani huku ndipo tunapokaribishwa katika Dunia ya sasa,lugha zetu za kwanza tunazifahamia huko na pia tunapoamini kuwa tutasikilizwa vizuri kuliko sehemu yoyote.

Hoja yangu ya pili ambayo inapaswa kutiliwa mkazo katika elimu yetu ni Ushirikiano baina ya wanafunzi kwa wanafunzi (Peer to peer learning) kwenye kubadilishana mawazo hasa wakiwa kwenye makundi, wanafunzi wanapokuwa pamoja wengi wao hufahamu changamoto zinazowakumba wenzao kwenye masomo, jamii wanamoishi na hata kwenye michezo. Njia hii sio tu itawafanya wawe na uwelewano baina yao,pia watajifunza na kujenga umoja hata pale ambapo watakuwa na wakati mgumu wa kutatua tatizo.

Vile vile itarahisisha katika kutengeneza taifa la wasulusha matatizo ya kwenye jamii wanazoishi, pia watakapofika hatua za juu kielimu kama chuo watakuwa ni wenye ushirikiano.Utaratibu kama huu nimeushuhudia kwenye kongamano la kielimu la Schools2030 ambapo wengi waliohudhuria ni walimu pamoja na wadau wa elimu kutoka Tanzania na wengine wa nchi mbalimbali.

Inapotumika njia hii itaweza kusaidia wanafunzi katika kuongeza maarifa tofauti na yale anayoyapata mwalimu anapofundisha darasani tu, kulinganisha ujuzi kwenye majadiliano wanayoyafanya, ufanyaji kazi wa maarifa na mwisho kupokea majibu yenye lengo la kuwajenga.

Ndani ya majadiliano katika makundi, pia kuwepo na usisitizaji wa usomaji wa kina kwa wanafunzi ili wasitegemee chanzo kimoja cha maarifa kwenye kuwapa jawabu sahii.

Elimu ya masuala ya fedha na ujasiliamali, pengine inatumika katika shule mbalimbali ama kufanyiwa kazi na wadau wa elimu na wenye uelewa wa masuala haya ya kifedha, lakini tunapoanza katika ngazi ya chini ya elimu kuwafundisha watoto kuhusu masuala ya kifedha itawajengea kufahamu kwa undani na hata kwa uchache juu ya uwekezaji, uwekaji akiba, upokeaji faida na hata elimu ya hisa.

Naamini katika mawazo haya, kwasababu elimu ya fedha au ujasiliamali haipaswi kumkuta mtu akiwa na miaka 17 na kuendelea, ni kama vile tunavyosisitiza masomo ya lugha na hii inapaswa kupewa chapuo la kutosha zaidi kuna msemo wa kiswahili unaosema kuwa ‘Hakuna aijuaye kesho’ sasa tutakaposisitiza kwenye hili inaweza kuleta jamii inayopenda kufanya biashara na masuala mengine.

Njia ya ufundishaji nayo izingatiwe, walimu wabuni njia za kuwafanya wanafunzi kuwa na miradi ya kiubunifu ambayo pengine ndio wataweza kuifanyia kazi kivitendo zaidi na sio kuishia kwenye njia moja tu ya kinadharia.Njia ya pili ambayo nimeielezea hapo awali inaweza kuunganishwa na hii hasa kwa wanafunzi kujifunza, ushirikiano wa pamoja.

Mbobezi wa uchumi kutoka nchini Marekani ananukuliwa akisema “Tatizo mojawapo kati ya kizazi cha leo na uchumi ni ukosefu wa elimu na ujuzi wa masuala ya fedha.”

Jambo la nne na la muhimu kwenye makala yangu ni Teknolojia, hii ni ya kupewa kipaumbele katika Dunia ya sasa, hatuwezi kuikimbia na tutakapojaribu hivyo basi tutabaki nyuma zaidi, teknolojia kama Uhalisia ghushi (Augmented Reality) na Uhalisia pepe (Virtual Reality) ni za msingi sana kwenye masomo ya sayansi na hata ya kihistoria.

Njia mojawapo ya kuipa nguvu teknolojia ni kuwekeza katika vitendea kazi kama kompyuta mpakato vifaa vingine vya umuhimu.

Anatomy_kgroup.jpeg

Watoto wakisoma biolojia kwa njia ya Uhalisia ghushi 'Augemented Reality' (Chanzo India Today)

Jambo la tano ni kwamba,katika ngazi ya chini kwa kweli tunahitaji mfumo wa elimu ambao unawasaidia watoto kutambua kile wanachofanya vizuri na kwa usahihi, mtindo wa sasa wa elimu nchini unamchagulia mwanafunzi nini anapaswa kukifanya na sio kutokana na mapenzi yake, muda umefika sasa, walimu, wazazi, serikali na jamii kutafuta njia ya kuwasaidia na kuwaongezea tutafute mfumo wa kile wanachofanya vizuri na utaalam katika hilo.

Napenda mfano wa herufi ‘T’ au Mti, wenyewe una matawi ambayo ni kama ujuzi wa mambo mengi iwe ya kiujasiliamali, uandishi, upigaji picha, mpira n.k, huku ile ‘I’ ndio iwe inashikilia maarifa ambayo mtu anayafahamu kwa undani zaidi na ndio kitu ambacho amesomea na kuwa mbobezi kwa njia hii itasaidia pia kwenye suala la ajira.

Hitimisho langu la makala haya ni kwamba ili haya yaweze kutekelezeka inahitajika mabadiliko ya elimu na yanapaswa kutiliwa mkwazo ili kufanikisha na kupata elimu bora, watainiwa wenye vigezo na hata kuwa na jamii iliyo elimika na yenye ujuzi wa kutosha.

Uchocheaji wa mabadiliko ya elimu uambatanishwe na malengo ya muda mfupi na mrefu ili kuwa na tathimini ya pamoja kuwa tumefikia wapi na je tunawezaji kufanya mabadiliko zaidi kwa mustakabali wa elimu yetu.
 
Upvote 0
Karibuni wanafamilia wa JamiiForum mnaweza kutoa maoni juu ya andiko nililoandika, itakua vizuri tubadilishane mawazo, asanteni sana.
 
Back
Top Bottom