SoC02 Elimu

Stories of Change - 2022 Competition

Hopper lyfer

New Member
Joined
Aug 31, 2022
Posts
4
Reaction score
4
Elimu ni ile hali ya kusambaa kwa maarifa,akili,ubunifu,uwezo na ujuzi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwengine, au kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine. Pia Elimu ni msingi mkuu wa maendeleo katika kila shughuli husika katika nchi yetu, kwani kupitia elimu tunaweza kupata wataalamu wa mambo mbalimbali kama madaktari, wahandisi, viongozi bora, walimu, marubani, wanasheria.​

Sekta ya elimu katika nchi yetu ni moja ya sekta adhimu na muhimu katika nchi yetu. Tangia tupate uhuru mwaka 1961 mpaka sasa,Serikali imezidi kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu kwa kuweka mitaala mbalimbali ya elimu,kujenga shule katika kila kata, kuweka sera mbalimbali za kusaidia kukuza elimu,uboreshwaji wa miundombinu kama shule na vyuo, utoaji wa ajira kwa walimu na wakufunzi,utoaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Licha ya juhudi zilizofanywa na serikali, bado sekta ya elimu inakumbwa na changamoto zifuatazo÷

Uhaba wa vitu vya kujifunzia na kufundishia kama vile vitabu rafiki kwa wanafunzi na kwa walimu,upungufu wa madawati,hali ambayo inapelekea wanafunzi kusoma kwa shida na kuleta matokeo mabaya katika sekta ya elimu. Mfano wanafunzi wengi kutumia kitabu kimoja kujifunzia au kukaa wengi kwenye dawati moja na hata kukaa chini, hali hii hutokea Zaidi kwa shule za vijijini na hata maeneo ya mjini, hii ni kutokana na kuwepo kwa shule nyingi Zaidi za serikali ambazo zinashindwa kuwekewa bajeti nzuri za fedha katika kuhakikisha zinaondokana na changamoto hizo.



Mazingira mabovu na miundombinu chakavu kwa kujifunzia, Mfano uhaba wa madarasa ya kusomea, madarasa chakavu, uhaba wa mabomba ya maji safi na salama maeneo ya kujifunzia, kutokuwepo kwa umeme maeneo ya shule, upungufu wa matundu ya choo katika shule nyingi hali ambayo imepelekea watoto kujisaidia vichakani na kuwa hatarini katika kupata magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindi.



Upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi,Hii ni moja ya changamoto kubwa kwa kila shule hususani za serikali kutokana na kuwa na walimu wachache katika masomo ya sayansi na kupelekea wanafunzi wengi kufanya vibaya katika masomo hayo, mfano mwalimu mmoja wa hesabu anaweza kufundisha madarasa Zaidi ya manne kwa siku na kupelekea kushindwa kufundisha vizuri jinsi vile inavyoitajika kufundisha ili wanafunzi waweze kuelewa kutokana na uchovu mwalimu anaoupata kwa kufundisha madarasa mengi.


Maslahi hafifu kwa walimu,Hii ni kutokana na mishahara midogo wanayopewa walimu na usawa katika mishahara kati ya walimu wa masomo ya Sanaa na wa masomo ya sayansi imepelekea walimu kutoa elimu ambayo ya kiwango cha chini wanapofundisha na hii imepelekea matokeo hafifu hususani kwa masomo ya sayansi. Mfano mwalimu wa sayansi mmoja amepangiwa kufundisha juu ya kiwango anachotakiwa kufundisha kwa siku kutokana na uhaba wa walimu wa sayansi katika shule nyingi za Tanzania , hii ni tofauti kwa walimu wa masomo ya Sanaa ambayo wapo wengi katika shule na mwisho wa siku walimu hao wanapokea mishahara sawa, kitu ambacho siyo sahihi na kinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la kipekee sana.

Ukosefu wa teknolojia mashuleni, Mfano matumizi ya kompyuta, imepelekea wanafunzi kutoendana na hali ya sasa ya teknolojia na imepelekea wanafunzi wengi kutokuwa na ujuzi wa maswala ya teknolojia katika masomo na kufanya elimu yetu izidi kuwa chini ukilinganisha na elimu zinazotolewa na mashule ya nchi zilizoendelea kama marekani, uingereza, China.

Elimu inayotolewa kutohusiana au kutoendana na maisha yetu ya kila siku,Elimu inayotolewa katika shule nyingi za nchi yetu ni elimu ambayo haimuandai mwanafunzi aweze kukabiliana na mazingira kutokana na elimu hiyo kuwa ya nadharia( kukariri )tu na si vitendo. Mfano mwanafunzi anaweza kumaliza mpaka chuo lakini asiwe na uwezo wa kufanya elimu yake iwe msaada kwa jamii inayomzunguka mfano mwanafunzi aliyesomea uhandisi anajikuta hawezi kutumia elimu aliyoipata katika kujenga majengo, barabara, madaraja na ndomana kazi nyingi zinazohusu uhandisi wanapewa watu kutoka mataifa mengine kama China, Marekani.

Ukosefu wa sera bora katika sekta ya elimu,Hii imepelekea sekta ya elimu kuwa dhaifu,Sera zilizopo katika mfumo wa elimu hazitoshelezi kukidhi kiu ya mafanikio katika sekta ya elimu kwani bado zinaonekana kuwa dhaifu na zilizopitwa na wakati, Mfano wa sera hizo ni kama vile, mitaala mibovu ya elimu kwa kuwa haimuandai mwanafunzi kuwa bora katika kuyatumia mazingira yanayomzunguka vizuri kutokana na elimu aliyokuwa ni ya nadharia Zaidi kuliko vitendo, na hii inapelekea vijana kutoweza kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo yao ya vyuo vikuu na kuwafanya kuwa tegemezi kwa familia zao na taifa kwa ujumla.Licha ya mapungufu na changamoto zinazoikumba sekta ya elimu, zifuatazo ni njia ambazo zinaweza kutumuka katika kuboresha sekta ya elimu.

Kutoa vifaa toshelezi vya kujifunzia na kufundishia,Mfano kuhakikisha vitabu vya kutosha vinapatikana mashuleni na katika sekta zote za elimu,pia ukarabati wa majengo na ujengaji wa shule,vyuo na majengo ya elimu, Pia utengenezaji wa majengo ya kufanyia masomo kwa vitendo, mfano ujengaji wa maabara za kutosha katika taasisi hizo za elimu. Kwa kufanya hivi tunaweza kuongeza uwezo wa wanafunzi kukabiliana na mazingira na pia ufaulu katika sekta ya elimu itaongezeka.



Utoaji wa ajira kwa walimu na wakufunzi wa masomo ya sayansi,Hii itasaidia kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi katika mashule,vyuo pamoja na taasisi zote za elimu.Ongezeko la walimu wa sayansi itapelekea ufaulu mzuri katika masomo hayo na kuleta matunda chanya katika nchi yetu.

Uanzishwaji wa tehama katika masomo,Kutokana na mambo ya utandawazi kuongezeka imefanya dunia kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine katika maswala ya teknolojia.Hivyo serikali na wadau wengine wa elimu hawana budi kuanzisha matumizi ya tehama mashuleni na katika taasisi zote za elimu kwa kuanzisha njia bora na za kisasa za kujifunzia na kufundishia, kwa mfano Matumizi ya kompyuta, projekta katika kujifunzia. Kwa kufanya hivi tutapelekea mfumo wetu wa elimu kuwa bora Zaidi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.



Uboreshwaji wa maslahi ya walimu na wakufunzi,Katika kufanya sekta ya elimu kuwa bora na yenye tija kwa taifa, serikaali na wadau wa elimu hawana budi kuboresha maslahi ya walimu na wakufunzi kwa kuwaongezea mishahara, kuwapunguzia tozo mbalimbali na pia kuhakikisha maslahi yao yanalindwa wakati wote wa utumishi wao na baada ya kustaafu kwao.

Uanzishwaji wa sera bora na imara katika sekta ya elimu,Sera zitakazoazishwa ziwe na maslahi chanya katika sekta ya elimu kwa kuweka mitaala bora ya elimu itakayowezesha kufanya wanafunzi waweze kuendana na kukabiliana na mazingira kwa kuwafanya kuwa wabunifu katika kutumia elimu waliyonayo katika kuleta maendeleo chanya katika nchi yetu.

Kutoa mafunzo bora na yenye tija kwa walimu na wakufunzi,Juhudi kubwa zinahitajika kufanyika hususani kwa walimu na wakufunzi mbalimbali ambao ndiyo msingi wa elimu kwa kuwapa mafunzo bora yatakayowaimarisha vilivyo katika utoaji bora wa elimu kwa wanafunzi.

Kwa ujumla serikali na wadau wa elimu wanahitajika kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwa kupunguza idadi ya madarasa na kutoa elimu itakayoendana na mazingira na yenye tija kwa wanafunzi na taifa kwa ujumla kwa kutompotezea muda wa kukaa shuleni mwanafunzi muda mrefu ambapo angetumia muda huo kujenga taifa kwa kufanya shughuli za kumletea kipato.

CHANZO CHA PICHA: GOOGLE
 
Upvote 4
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…