Hapa kijijini mjadala umekuwa ukiendelea kuhusu wanyama jamii ya Punda namna ya ulaji wa mimea, mfano "mhindi" ambao umeng'atwa na punda huwa hauoti tena, tofauti na unapong'atwa na wanyama wengine kama ng'ombe, kondoo au mbuzi, na wanakijiji wamefika mbali zaidi na kusema labda wanyama aina ya punda yamkini watakuwa na sumu, hivyo endapo watang'ata mmea huo basi huathirika na sumu, hivyo kutokuendelea kuchipua tena.
- Tunachokijua
- Mimea ni aina ya viumbe hai inayojumuisha viumbe wa kawaida kama vile miti, mimea ya shambani, nyasi, mizabibu, pamoja na mimea mingine mingi. Mimea hubadilisha maji na kabonidayoksaidi kuwa oksijeni inayovutwa na wanyama. Hata hivyo mimea ina uhusiano wa moja kwa moja na wanyama mfano katika uzalianaji ambapo wanyama husaidia upevushaji wa mimea huku pia ikitumika kama chanzo cha chakula kwa wanyama.
Kumekuwapo na hoja kuwa ulaji sehemu ya mimea na mnyama kama punda, tofauti na wanyama wengine husababisha mimea hiyo kushindwa kuendelea kukua.
Je uhalisia wa hoja hiyo ni upi?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa si kweli kwamba ulaji wa mimea kwa mnyama punda husababisha kusimama kwa ukuaji wa mimiea hiyo.
Wanyama wote (herbivores) wanaweza kula mmea mzima au sehemu kubwa kiasi cha kuua mmea huo, wengine hula sehemu tu ya mmea, na hivyo mmea unaweza kupona na kuendelea kukua.
Hali ya wanyama kula mimea kupita kiasi kunaweza kubadilisha umbo la mmea kabisa, na urejeshaji wake unaweza kuchukua muda zaidi pia kunaweza kuua na kuharibu kabisa mmea.
Wanyama wanaokula mimea ambao wanajulikana herbivores, huathiri viungo vya mimea kama vile majani, mashina, mizizi, na maua wanapokula mimea. Ikiwa mmea unapoteza sehemu ya tishu zake hai, inaweza kuwa na changamoto ya kunyonya maji na virutubisho, jambo ambalo hufanya mmea kuwa dhaifu. Katika baadhi ya matukio, hupunguza uwezo wa mmea kujitengenezea chakula chake (photosynthesis), kukua, kuzaliana, na hata kuendelea kuishi. Hii ina maana kwamba wanyama kula mimea kunaweza kudhibiti wingi wa mimea katika mazingira.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la Ecology, wanasayansi walionesha katika jaribio kwa kuharibu baadhi ya mimea kulianzisha mfululizo wa matukio ya kimolekuli ambayo yaliwasababisha mimea hiyo kukua kwa ukubwa zaidi na kuzalisha mbegu nyingi zaidi pamoja na kujenga kinga za kemikali kwa wakati mmoja pamoja na kuokoa maisha ya mmea. Vilevile mimea huweza kujiimarisha zaidi kutokana na sehemu yake kuliwa na wanyama na hivyo kuendelea kukua.