Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,421
Kama unatamani kufanikiwa katika uhusiano wa kijamii, ni muhimu ukakubali ukweli kwamba si kila mtu atakupenda, si kila mtu atavutiwa na ujio wako na hasa kwa mara ya kwanza. Kila mtu anacho kifurushi cha sifa za vitu anavyopenda na asivyopenda ambavyo alivitengeneza siku nyingi.Usidhani una haja ya kujilaumu kama uliyeshindwa iwapo inaonekana mtu fulani hakupendi au havutiwi nawe.
Kama kuna mtu anayekuchukia, sababu ya kukuchukia huko huenda ikawa na uhusiano mdogo na wewe ama huenda isiwe inahusiana kabisa na wewe. Huenda mtu huyo anakuchukia kutokana na kudhani unamuogopa ama kumkwepa, kuona haya ama kuonekana kutokuwa tayari kukaa naye na kuzungumza naye ama kutokuwa katika kiwango kimoja na yeye. Kwa kifupi huenda wewe na mtu huyo, ni watu tofauti msioweza kwenda pamoja hivi sasa.
Usijisikie vibaya na kuanza kujiweka kando na kuwa mpweke kwa kudhani kwamba dosari zako ni kubwa kuliko sifa zako. Kwa kweli, huenda baadhi ya hizo dosari zikawa na mvuto mkubwa kwa watu wengine. Unaweza kuwa umenenepeana sana, lakini ukawa na tabasamu la kuvutia na furaha katika maisha yako. Wapo watu ambao mwili wako huo mkubwa unaweza kuwavutia ama wanaweza wasiuone ama kuonekana kero kwao. Unaweza kuwa na hali mbovumbovu au afya nyondenyonde, lakini ukawa na uwezo mkubwa katika kusakata dansi na mkweli kwa marafiki zako. Ukweli ni kwamba wapo watu wanaotafuta watu wakweli ama watakaowapatia furaha, wema au waungwana na hivyo wewe kuwa na sifa za kujenga nao urafiki.
Ikiwa una shaka kwamba wewe si mzuri wa kutosha wa sura na umbo kuweza kuwavutia marafiki wapya, hasa kwa wanawake. Lazima uelewe kwamba si kila mtu anatafuta uzuri wa sura kwa marafiki zake. Jifunze kupumzisha akili yako. Badala ya kujifunga kwenye mapungufu yako, weka mkazo kwenye sifa zako bora mbele ya watu. Boresha zaidi sifa nzuri ulizo nazo kwani hizo ndizo wale wanaozipenda zitawavuta kuwa karibu na wewe na si vinginevyo.