Ewe Mjasiriamali/Mfanyabiashara zingatia haya kabla ya kuanza biashara/wazo la biashara!

Joined
Jun 28, 2017
Posts
72
Reaction score
124
Ewe Mjasiriamali/Mfanyabiashara zingatia haya kabla ya kuanza biashara/wazo la biashara!

Habari zenu

Kumekuwa na ongezeko la watu kuingia katika ujasiriamali/kufanya biashara hasa katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi za kibiashara. Hili ni jambo jema kwani watu wanatoka katika fikra za kuamini ya kwamba hauwezi kufanikiwa katika maisha bali mpaka uajiriwe. Hili si kweli, mafanikio yanapatikana hata nje ya kuajiriwa.

Pamoja na hili la watu kutamani kuingia katika kujiajiri, kuna tatizo ambalo kama wana jamii tunapaswa kushauriana na kusaidiana kutatua changamoto hizo. Ukiangalia kwa haraka haraka utaona karibu kila baada ya muda mfupi maswali haya yamekuwa yanaletwa sana barazani , mfano kama haya

1. Nina mtaji wa kiasi Fulani, mfano mil 1-6; naweza kufanya biashara gani?

2. Tunaopanga kuacha kazi na kujiajiri, tunapanga nini cha kufanya?

3. Kiwanda gani kidogo naweza kuanzisha kwa gharama ya kiasi Fulani, n.k

Kimtazamo wa maswali au maelezo yote hapo utaona ni kwamba kuna mambo ya msingi na maono ambayo mtu anapaswa kuyapa nafasi kabla ya kufikia maswali/maelezo hayo hapo juu

Mambo hayo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kuamua kuanzisha biashara/kuwa mjasiriamali baadhi yake ni haya:

1. Wazo la biashara

Fanya upembuzi yakinifu wa mawazo ya kibiashara unayoona yanafaa na mwisho kabisa chukua wazo lililo bora kabisa. Katika dunia ya leo, hakuna biashara ambayo haijafanywa hili lazima ulitambue. Muhimu kwako sasa ni kuhakikisha wazo lako unaliboresha hadi linakuwa la kipekee kabisa japo aina ya biashara hiyo ipo tayari sokoni. Jiulize maswali haya ndani ya wazo lako la biashara uliloona ni bora na la kipekee

§ Nini lengo la hii biashara?

§ Je nitajitofautisha vipi na biashara inayofanana na wazo langu ambayo tayari ipo sokoni?

§ Je ni maboresho gani au ugunduzi gani ntauongeza katika kujitofautisha?

Hili utakuja kuona kabla hujauliza wazo la biashara ya kufanya anza wewe mwenyewe kujiuliza biashara ipi unaona utaimudu kwa namna yoyote ile

2. Vikwazo katika biashara unayotaka kuianza

Fanya tafakuri jadidi juu ya mambo ambayo unaona yanaweza kukukwamisha kuifanya biashara. Hii ina maana jitahidi kufanya uchunguzi kwa kuwauliza wajasiriamali au wafanyabiashara wa biashara unayoiwaza kuifanya au ifanana nayo.

Angalia sasa je vikwazo hivyo umejipanga vipi kimkakati kukabiliana na changamoto hizo. Vilevile wazo lako unalilinda vipi kimkakati kuhakikisha wazo lako hata kama mtu akilikopi atashindwa kufanikiwa kwa sababu ya namna ya utekelezaji wake kuwa na mikakati madhubuti

3. Soko gani unalenga

Wazo lako la biashara liangalie ni soko gani hasa linalenga. Bidhaa uizalishayo jitahidi ikusaidie kuulinda na kuukuza mtaji. Buni biashara ambayo itagusa sehemu kubwa ya jamii kwa namna zifuatazo:-

Aina ya pesa. Tambua watu wa kipato cha chini pesa zao ni za ‘coin’ , hivyo bidhaa ambayo utazalisha na kuiuza kuanzia sh 100/= hadi 500/= utaona itaigusa jamii kubwa ya watu wa kipato cha chini na cha kati kuliko kubuni biashara ambayo bidhaa zake zitakuwa bei juu

Mzunguko. Faida nyingine ya bidhaa za bei za chini ni pamoja na kukupa mzunguko mkubwa wa bidhaa zako sokoni. Japo faida si kubwa lakini kwa ukubwa na uharaka wa mzunguko utaona faida inayopatikana ni kubwa

Mfumo wa uuzaji bidhaa. Uza bidhaa uzalishazo kwa kuanzia chini na kupanda juu ie retail to wholesale business. Kumuuzia mtu wa reja reja na hata mtumiaji wa mwisho itakusaidia kuitangaza bidhaa yako na vile vile faida nyingine hutauza kwa mkopo kwani utamuuzia kiwango anachomudu kulipa tu. Kuuza katika maduka ya jumla kwa biashara inayoanza tatizo lake ni katika malipo na vile vile maduka ya jumla ni kama stoo ya bidhaa nyingi na ambazo mnunuzi siku zote huenda kununua alichozoea na anachokifahamu. Sasa kwa wewe mwenye bidhaa mpya mpaka izoeleweke inachukua muda

Kutangaza katika media ni jambo jema lakini gharama zake zipo juu hivyo tumia njia mbadala kuingia na kulishika soko

4. Je una Mtandao?

Katika biashara yoyote kuianzisha, suala la msingi ‘capital’ sio jambo la kwanza ili uianzishe biashara. Jambo la kwanza ni wazo la biashara na jingine muhimu ni mtandao. Tambua nani unaweza kumuuzia katika hao unaofahamiana nao. Mfano unakuta mjasiriamali au mfanyabishara yupo katika makundi zaidi ya matatu ya kijamii lakini hanufaiki nayo kisa anaona aibu kuitangaza bidhaa yake halali. Jitahidi hao watu unaoanza kuwauzia kujenga nao mtandao ambao watakupata kirahisi na utawapata kirahisi katika kuwafuatilia toka ulivyowauzia kwa mara ya kwanza na kuendelea

5. Jenga Moyo wa Imani na Subira kufikia Mafanikio

Tambua wazi kuingia katika ujasiriamali au biashara kunahitaji kuwa na imani ya dhati kupambana na changamoto na uwe na zaidi ya uvumilivu ie uwe na subira kufikia mafanikio. Changamoto za kibiashara zisikukatishe tamaa au kukurudisha nyuma bali iwe chachu ya mapambano kuelekea katika mafanikio. Siku zote mwanzo wa jambo ni mgumu lakini ukiwa na nia thabiti na malengo utatoboa

6. Andika mchanganuo wako wa biashara

Andika mchanganuo wa kibiashara wa wazo lako. Baada ya hapo waweza kuuboresha kwa kupeleka kwa wataalam wa masuala ya biashara wakakuandikia katika namna iliyo nzuri na nyepesi kutekelezeka



7. Amua na Jipime Utayari wako

Amua na vilevile jitathmini utayari wako wa kufanya biashara au kuwa mjasiriamali. Usifuate mkumbo. Kwa mfano mtu umezoea maisha ya kuajiriwa, hutishwi lakini ni lazima ujitathmini na kangalia utayari wako na umejipanga vipi kimaandalizi kuacha kuajiriwa na kuingia maisha ya kujiajiri

8. Chagua Aina na Muundo wa Biashara yako

Aina na muundo wa biashara yako ni muhimu sana kwani itakusaidia namna ya kuiendesha biashara husika. Inapendeza kama unafanya biashara ya uzalishaji tafuta watu wa kuiuza na wewe ubaki mzalishaji tu kwani utaweza kuthibiti ubora wa bidhaa sokoni, wakati huohuo ukitoa presha ya kufikia malengo ya mauzo kwa muuzaji wa bidhaa zako

Haya ni baadhi ya mambo muhimu kuyatafakari. Uwanja upowazi kwa wabobezi wa masuala ya ujasiriamali na biashara kuongeza zaidi na kurekebisha mahala palipo na mapungufu

karibuni
 
asante sana, mimi naomba nisaidiwe kuhusu kuandika business plan
 
Kucharanga business plan na kui develop ukafanya na market survey sio kitu cha overnight
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…