Date::2/16/2009 (
Mwananchi Read News )
Bukoba: DC aungwa mkono kwa walimu kuchapwa viboko
*Polisi wazima mpango wa waalim kuandamana kulaani adhabu hiyo
Na Lilian Lugakingira
Walimu mkoani hapa walikuwa wamepanga kuandamana jana lakini maandamano hayo hayakufanyika kutokana na kutopata kibali cha Jeshi la Polisi, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa Chama cha Walimu cha Kagera, Dauda Bilikesi.
Bilikesi alisema kuwa walimu walikuwa wamepanga kufanya maandamano ya amani kulaani kitendo cha mkuu huyo wa wilaya ya Bukoba cha kuwachapa walimu viboko, na kuwa kunyimwa kibali cha kufanya hivyo ni kunyimwa haki yao ya kujieleza na kutoa hisia zao.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zimesema kuwa, walimu hao walinyimwa kibali kutokana na kuhofia kuvunjika kwa amani. Hata hivyo, kamanda wa polisi mkoani hapa, Henry Salewi hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Wakati walimu wakishindwa kuandamana, wakazi wa wilaya ya Bukoba wanamuona DC Mnali kuwa alifanya kitendo sahihi cha kuchapa walimu viboko, wakidai kuwa utoro, uchelewaji na uzembe umezidi.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema kuwa adhabu aliyoitoa rais kwa mkuu huyo haistahili, wakisema kuwa walimu hao walistahili adhabu hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu.
Wakazi hao waliitupia lawama serikali iliyopitisha utaratibu wa walimu kupewa mikopo ambao wamesema umechangia kwa asilimia kubwa walimu kukiuka maadili ya kazi yao, ikiwemo kufanya biashara saa za kazi na kushindwa kufundisha.
Helleni Lianda, mkazi wa kata Kashai katika manispaa ya Bukoba, alisema kuwa wapo baadhi ya walimu ambao wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi na taratibu za kazi, lakini walimu walio wengi wamejiingiza katika biashara na kuwa wanapaswa kuchagua moja, kama kuingia madarasani kufundisha au kufanya biashara.
"Ni haki yao kupigwa viboko; wanafanya biashara saa za kufundisha; wanafika kazini wakiwa wamechelewa; wanapiga soga kazini badala ya kufundisha. Mimi sioni sababu ya kumwadhibu DC eti kwa sababu kawapiga walimu, ni haki yao," alisema Lianda.
Naye Beatrice Mshumbusi, mkazi wa kata Hamugembe, alisema walimu walistahili kuchapwa viboko, akidai kuwa wamekuwa kero hasa kutokana na vitendo vyao vya kulewa saa za kazi, hali inayosababisha wengi wao kuwa wachafu kupindukia.
Mbali na asilimia kubwa ya watu waliohojiwa kuonekana kumuunga mkono mkuu huyo wa wilaya, wapo baadhi ambao wamesema kitendo cha kuwachapa viboko walimu sio cha kiungwana maana zipo taratibu za kumwajibisha mtumishi wa serikali anayeenda kinyume na taratibu za kazi, sio kumchapa viboko.
Baadhi ya wazazi walisema wanaandaa maandamano kupinga kitendo cha kumwajibisha mkuu wa wilaya ya Bukoba kwa sababu ya kuwapiga walimu viboko.Mzazi mmoja wa Hamugembe aliyejitambulisha kwa jina la Athuman alisema kuwa endapo Jeshi la Polisi litatoa kibali kwa walimu hao kuandamana kuunga mkono uamuzi wa Rais Kikwete, na wazazi wataandamana kupinga hatua hiyo.
Tuma maoni kwa Mhariri