Fahamu Hati Nne zinazotolewa na CAG

Fahamu Hati Nne zinazotolewa na CAG

beth

JF-Expert Member
Joined
Aug 19, 2012
Posts
3,880
Reaction score
6,368
Hati za Ukaguzi ni maoni ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu hesabu za Taasisi inayokaguliwa. Maoni haya yanalenga kuonyesha kama hesabu zilizokaguliwa zimeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kihasibu vya kimataifa (IPSAs) na matamko yanayotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA)
Inatarajiwa kuwa, uwajibikaji wa taasisi na vitengo vya umma unafanikiwa zaidi pale ambapo utendaji na matumizi ya taasisi za umma zinazingatia viwango vya kihesabu vya kimataifa na matamko ya NBAA. Uzingatiaji wa viwango hivi unaziba mianya ya ubadhirifu kwenye matumizi ya umma na athari zake kwa upatikanaji huduma kwa wananchi

Aina ya Hati Zinazotolewa na CAG

Katika ukaguzi wa taasisi za Umma, CAG hutoa hati zifuatazo;

1) Hati inayoridhisha (hati safi): Hati hii inatolewa wakati Mkaguzi anaporidhika kuwa hesabu za mkaguliwa zimetayarishwa kwa usahihi na kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu na vile vinavyotolewa na Bodi ya NBAA. Hati safi inamaanisha kuwa, hesabu zinaonyesha kwa usahihi hali halisi ya kifedha na utendaji wa taasisi iliyokaguliwa

2) Hati Yenye Mashaka: Hati hii hutolewa pale mkaguzi anapokutana na mazingira ya kuwepo kwa makosa ya msingi ya kiuhasibu yanayohusu mapato, matumizi au rasilimali za shirika linalokaguliwa. Hati yenye mashaka inamaanisha kuwa, hesabu zinaonyesha kwa usahihi hali halisi ya kifedha na utendaji wa taasisi iliyokaguliwa, isipokuwa tu katika maeneo machache ambayo mkaguzi ameyatilia mashaka

3) Hati Isiyoridhisha: Hati hii inatolewa pale Mkaguzi anapoona kuwa, taarifa za fedha na rasilimali za mkaguliwa kwa kiasi kikubwa zina makosa ya msingi ya kiuhasibu na kiutendaji pamoja na kuwepo na usimamizi mbovu wa mifumo ya udhibiti ya ndani. Hati isiyoridhisha inamaanisha kuwa, hesabu zilizokaguliwa sio sahihi na hivyo, hazionyeshi usahihi wa hali halisi ya kifedha na utendaji wa taasisi iliyokaguliwa

4) Kushindwa kutoa Hati (Hati Mbaya): Hati hii hutolewa pale ambapo mkaguzi anapojiridhisha kuwa mkaguliwa hana kumbukumbu za fedha na rasilimali zinazotosheleza kutengeneza taarifa za mahesabu ya taasisi pamoja na kuwepo udhaifu mkubwa wa usimamizi wa mifumo ya udhibiti ya ndani. Kulingana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiyo inayozungumziwa kama, hati mbaya ya ukaguzi

WAJIBU Institute
 
Back
Top Bottom