Fahamu kuhusu mwanamuziki Ludwig van Beethoven

Fahamu kuhusu mwanamuziki Ludwig van Beethoven

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Posts
76,107
Reaction score
160,001
Huenda ungependa kufahamu kuhusu mwanamuziki wa kale Ludwig van Beethoven. Hayumkini ndiye mwanamuziki nguli wa wakati wote wa miondoko ya klasiki (classical music).

Alizaliwa Ujerumani Disemba 17 mwaka 1770, na alianza kufanya muziki akiwa na umri wa miaka 5. Alikuwa na baba mkali kimalezi na walimu wa muziki wenye kaliba sawa na baba yake ambao walimpangia mazoezi marefu na magumu ya muziki, wakati mwingine kama adhabu, mambo ambayo yalimtoa machozi Beethoven.

Kuna wakati fulani mwalimu wake wa muziki kwa jina Tobias Pfeiffer alikuwa na tatizo la kukosa usingizi. Kwa kuwa muda mwingi mwalimu huyu alikuwa macho basi akawa anamburuza Beethoven akiwa amelemewa na usingizi majira ya saa tisa za usiku, na kumpeleka kwenye kinanda kufanya mazoezi. Wakati huu Beethoven alikuwa mtoto mdogo wa miaka 7 tu.

Walimu wake walitaka afanye muziki katika tamaduni na kanuni za wakati ule lakini Beethoven alitaka kuongeza vionjo vyake mwenyewe na kuwa mbunifu zaidi. Kwa hiyo, akiwa peke yake akawa anakwenda kwenye kinanda na kucheza nota zake za muziki alizotunga huku akiwa amejawa hasira na wakati huo huo furaha kwamba alikuwa akicheza muziki aupendao.

Hatimaye akawa mwanamuziki na mtunzi mahiri ambaye tungo zake hata leo hii ikiwa imepita miaka zaidi ya 200 bado zinahusudiwa duniani kote na wapenzi wa miondoko ya klasiko.

Angali bado kinda, Beethoven akawa tayari mashuhuri kwenye fani yake, lakini, ghafla akiwa na umri wa miaka 21 akaanza kupoteza uwezo wa kusikia.

Hali hii ilimfanya akawa na msongo mkubwa wa mawazo kwamba angefanya vipi na kufurahia muziki kama hangeweza kusikia. Katika barua zake nyingi alizowaandikia marafiki zake aliwaeleza kwamba tatizo hilo lilimfanya atamani kujiua, lakini akaapa kwamba hatafanya hivyo na ataishi kwa ajili ya muziki wake.

Mwaka 1814, akiwa na umri wa miaka 44, akapoteza kabisa uwezo wa kusikia na akaishi katika upweke akiwa na “kitabu cha mazungumzo” na kalamu pembeni yake, kwa ajili ya ambao walitaka kuzungumza naye. Aliongea kwa sauti kubwa na kucheza kinanda kwa spidi kali sana kiasi kwamba watu wakahisi huenda alikuwa amewehuka.

Hata hivyo baadhi ya watu matajiri huko London, Uingereza wakampa kazi ya kuandika muziki (symphony) ambao ulikuwa andiko lake la 9 na la mwisho, lakini pia mashuhuri kuliko yote yaliyotangulia. Alitunga andiko hilo namba 9 akiwa kiziwi kabisa, na hakuwahi kusikia hata nota moja ya andiko hiyo bali aliisikia kichwani mwake.

Kwenye uzinduzi wa andiko hilo, akasisitiza kwamba lazima yeye awe mwongozaji. Alikuwa hajafanya hivyo kwa karibu miaka 12, na kila mtu alikuwa na wasiwasi lakini wakamruhusu.

Tarehe 7 Mei 1824 Beethoven akapanda jukwaani huko Vienna Austria kuongoza uzinduzi. Video ambayo nimeambatanisha na andiko hili ni kipande toka katika sinema ya “Copying Beethoven”. Mwishoni mwa tamasha kama unavyoweza kuona, ameupa umati mgongo, hakuwa na hakika namna gani muziki wake ulikuwa umepokelewa, mpaka binti mmoja ambaye alikuwa akimsaidia alipokwenda jukwaani na kumgeuza kutazama walioko ukumbuni kuona namna ambayo walikuwa wameipokea kazi yake. Alilia.

Hili lilikuwa tamasha lake la mwisho, na aliaga dunia miaka mitatu baadaye. Tungo yake hii ambayo pia inaitwa “Ode to Joy” (Tungo ya Furaha) hivi sasa ni wimbo rasmi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU). Karatasi halisi ambazo Beethoven ameandika nota za tungo hii zimehifadhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Mwandishi wa makala hii ni january Makamba
 
Safi sana January Makamba, kama kazi zako zote za uwaziri zinafanywa na mtukufu ni vizuri wewe ukaendelea kutushushia nondo. Juzi kati ulikuja na story wa wali ng'ombe kule Dodoma, bado naikumbuka pia story ya kukosa ada kule Marekani na leo ni classical music
 
Huyu Ndo Nyimbo Zake Compter Ukinunua Unazikuta Zipo?
 
Back
Top Bottom