Fahamu mbinu mbalimbali za kuongeza mauzo ya biashara yako

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Jana tuliona kwamba mzunguko wa fedha ndio damu ya biashara yako. Kama mzunguko huu usipokuwa vizuri basi biashara yako itadhurika. Na kama mzunguko huu utasimama basi biashara nayo itakufa. Tuliona baadhi ya njia za kuhakikisha mzunguko wako wa fedha upo vizuri.

Leo tutaangalia eneo muhimu sana la kuhakikisha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako unakuwa mzuri. Eneo hili ni mauzo. Mauzo ndio yanaleta fedha kwenye biashara yako na hivyo kama ukiongeza mauzo maana yake unaongeza fedha zinazoingia. Japokuwa hili halimaanishi kwamba ukiongeza mauzo umeongeza faida, la. Tutaangalia kwenye makala zijazo jinsi ya kuhakikisha unapata faida ya kukutosha. Leo tuangalie kwanza kuhusu mauzo ya biashara yako na jinsi ya kuyaongeza.

Kabla hatujaona mbinu tano ambazo unaweza kuzitumia kuongeza mauzo kwenye biashara yako naomba nijibu swali muhimu sana ambalo unaweza kuwa unajiuliza, je inawezekana mauzo ya biashara yangu kuongezeka? Jibu ni ndio, haijalishi biashara yako ipo kwenye hatua gani, bado una nafasi ya kuongeza mauzo zaidi ya unayofanya sasa. Kikubwa ni kujua mbinu sahihi za kutumia ili uweze kuongeza mauzo yako.

Kwa kuwa tuko sawa sasa ya kwamba mauzo ya biashara yako yanaweza kuongezeka, sasa unayaongezaje? Hapa ndio zinakuja mbinu tano muhimu unazoweza kutumia kuongeza mauzo yako.

Mbinu ya kwanza: Uza bidhaa zinazoendana kwa pamoja

Mteja anapokuja kununua bidhaa kwako, tayari amejipanga atanunua bidhaa au huduma fulani. Unaweza kumuuzia bidhaa hiyo na akaondoka, unakuwa umepata mauzo ya kile alichotaka na mambo yanaishi hapo. Ila ukiwa mfanyabiashara mjanja unaweza kumuuzia ile bidhaa anayotaka na pia ukamjulisha kwamba kuna bidhaa nyingine ambayo inaweza kutumika kama hiyo. Au kama zikitumika pamoja basi zitaboresha maisha yake kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano kama mtu amenunua nguo muuzie na viatu, na begi la nguo. Kama mtu amenunua kompyuta, mwambie kuna vitu muhimu anahitaji kununua ambavyo vitafanya matumizi ya kompyuta yake kuwa mazuri. Kwa mfano kuweza kuhifadhi data zake sehemu tofauti ili zisipotee kompyuta inapopotea. Kama mtu akinunua kitabu kimoja mwoneshe na vitabu vingine ambavyo vitampatia maarifa zaidi.

Kwenye biashara yoyote unayofanya, kuna bidhaa nyingi unazoweza kuuza kwa pamoja. Fanyia kazi hili.

Mbinu ya pili: Uza bidhaa yenye uhitaji mkubwa

Ni rahisi mtu kununua tiba kuliko kununua kinga. Ndivyo binadamu tulivyo, kama hakuna tatizo kubwa linalotusumbua basi hatuhangaiki kutafuta suluhisho.

Ni kazi yako kama mfanyabiashara kuangalia biashara yako vizuri na kuangalia matatizo ya watu, ni matatizo gani ambayo yanawaumiza na wanatafuta sana suluhisho. Kisha wapatie suluhisho la matatizo yao kupitia biashara yako.

Kwa mbinu hii utapata wateja wengi ambao wana matatizo na wanatafuta suluhisho la matatizo yao.

Mbinu ya tatu: Toa punguzo na weka muda wa kuisha kwa punguzo hilo

Tengeneza aina yoyote ya ofa kwenye biashara yako ila weka muda maalumu ambapo ofa hii itakuwepo. Sio lazima ofa yenyewe iwe kubwa na ya kuathiri biashara yako. Kikubwa ni kutengeneza mazingira ya utofauti kwenye biashara yako ambayo yatamvutia mteja kununua zaidi.

Na unapoweka tarehe ya mwisho wa ofa yako na ukawa unawakumbusha wateja mara kwa mara kwamba ofa inakwisha watasukumwa kufanya maamuzi haraka kabla nafasi hiyo haijaisha.

Mbinu ya nne: Weka bei zako vizuri

Bei zako inaweza kuwa sababu ya watu kununua au ikawa kikwazo cha watu kununua. Sio mara zote ukiweka bei ndogo ndio unapata wateja wengi, kuna wakati ukiweka bei kubwa ndio unapata wateja bora zaidi.

Kwa kuwa hili la bei linahitaji mbinu zake pia, tutalijadili kwa undani kwenye makala inayofuata.

Mbinu ya tano: Boresha huduma unazotoa kwa wateja wako

Hakuna kitu ambacho kila mtu anapenda kama kupata huduma bora, kama kuona anajaliwa na kama kuona kwamba yeye ni muhimu. Ukijenga biashara yako kwenye misingi hii ya kumjali na kumpatia huduma nzuri mteja wako, mteja ataridhika na hataweza kukaa kimya. Atawaambia wengi zaidi na hivyo utakuwa na wateja wengi na mauzo yako kuongezeka.

Wateja ulionao sasa ni sehemu nzuri sana ya kukuza biashara yako kwa sababu ni wao ambao wataisema biashara yako vizuri. Na pia wanaweza kuwa sehemu ya kuiua biashara yako kama watapata huduma mbovu na kuanza kuisema biashara yako vibaya.

Fanyia kazi mbinu hizi tano na utaona mabadiliko makubwa kwenye mauzo yako.

===========



Haijalishi huduma au bidhaa yako ni kubwa kiasi gani, biashara yako haitazalisha pesa kama wateja hawatakuwa tayari kununua bidhaa au huduma yako. Hakuna wateja, hakuna biashara.

Tatizo la kukosa wateja hukabili sana biashara ndogo, na hata kusababisha biashara hizo kufa. Siyo kwamba wateja hawapendi kununua bidhaa za biashara hizi, bali tatizo kubwa ni mbinu duni za kujitangaza na masoko.

Katika makala hii nitakueleza mbinu 10 rahisi na za gharama nafuu ambazo unaweza kuzitekeleza na ukaongeza au kuvutia wateja zaidi kwenye biashara yako.

1. Lugha nzuri
Katika mambo yanayowapotezea wafanyabiashara wengi wateja ni lugha mbaya kwa wateja. Hakuna mteja anayependa kupokelewa au kujibiwa vibaya. Hakikisha unazungumza na wateja wako kwa namna bora ambayo wataona unawajali, unawathamini na kuwaheshimu.
Mimi mwenyewe ninapenda kwenda kwenye biashara ambayo wahusika wana lugha nzuri; huwa nawashauri pia rafiki zangu kwenda kwenye biashara za aina hiyo. Hivyo hakikisha unatumia mbinu hii ili kuongeza wateja.

2. Huduma au bidhaa za bure

Wateja wengi wanapenda vitu vya bure au zawadi. Siyo lazima ufanye jambo kubwa la bure ili kuwavutia wateja; hata jambo dogo tu linaweza kuwavutia sana. Ili kuwavutia wateja unaweza kutoa huduma au vitu vya bure kama vile kalamu, mifuko, shajara (diary) au hata maji ya kunywa. Kwa njia hii utawavutia wateja wengi zaidi.

3. Punguzo
Punguzo ni njia bora sana ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara na kupata wateja. Ikiwa mwenzako anauza sabuni kwa shilingi 2,100, wewe uza 2,050. Unaweza usipate faida kubwa kwenye bidhaa moja lakini utapata faida kubwa kwenye mauzo ya jumla. Kwa mfano ikiwa faida kwenye sabuni hapo juu ni sh. 100, muuzaji wa kwanza akauza sabuni 5 kwa sh. 2,100 atapata faida ya sh. 500. Lakini wewe ukauza sabuni 20 kwa sh. 2,050 utapata faida ya sh. 1,000. Je huoni kuwa umeuza na kupata faida zaidi kutokana na kuvutia wateja wengi kupitia punguzo? Weka punguzo sasa.

4. Shindano
Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo uweze kuendesha shindano. Unaweza kuendesha shindano lenye zawadi ndogo kama vile vocha, kalamu, mikoba, shajara au hata vinywaji.
Kwa njia ya kuweka shindano watu wengi watavutiwa kununua bidhaa au huduma zako ili wawe washindi. Unaweza pia kuweka bidhaa au huduma zako kama kitu cha kushindaniwa badala ya zawadi nyingine.

5. Anzisha tovuti au blog
Watu wengi hawafahamu umuhimu wa tovuti au blog. Wengi hufikiri kuwa ni mahali pakuweka matangazo ya watu wengine ili wakulipe.Ukweli ni kuwa blog au tovuti ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza wateja kwa njia ya kutangaza biashara yako.Ukiwa una blog nzuri yenye watembeleaji wa kutosha, unaweza kuitumia kutangaza na kuuza bidhaa zako wewe mwenyewe na ukajipatia pesa nyingi.

6. Tumia mitandao ya kijamii
Kama ilivyo kwa blog na tovuti, vivyo hivyo mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa kuzalisha pesa nyingi. Ikiwa unataka kuongeza wateja, basi wafahamishe watu kupitia mitandao ya kijamii juu ya huduma au bidhaa zako. Hakikisha wanazielewa na kuweza kuzifikia kwa urahisi.

7. Matangazo

Biashara nyingi hupuuza nafasi ya kujitangaza ili kuongeza wateja na hatimae kupata faida zaidi. Siyo lazima utumie njia za gharama kubwa kujitangaza kwani zipo njia nyingi sana.
Unaweza kutumia mitandao (rejea mbinu ya 5 na 6), vifungashio, saini ya barua pepe (email signature), card ya utambulisho wa biashara (busness card), vipeperushi n.k.

8. Toa misaada
Je umeshawahi kujiuliza kwanini biashara na kampuni nyingi hutoa misaada mbalimbali? Je ni kwa kuwa wana pesa za ziada au wanawapenda sana wale wanaowasaidia?
Ni wazi kuwa hii ni mbinu nzuri sana ya kujitangaza na wala si vinginevyo. Kwa njia ya kutoa misaada wateja huongezeka zaidi kwani watu huifaahamu biashara husika, pia huichukulia kama biashara inayowajali zaidi. Kumbuka siyo lazima utoe misaada mikubwa au ya pesa nyingi. Unaweza kutoa hata bidhaa zako au huduma yako kama msaada kwa watu au taasisi fulani.

9. Lenga changamoto
Watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili itatue changamoto zao. Hivyo kuendesha biashara isiyolenga changamoto za wateja haitapata soko. Hebu fikiri mtu anaanzisha duka la kuuza dawa za Ebola Kenya au Tanzania, je atapata wateja kweli? Ni wazi kuwa hatapata wateja kwani tatizo la Ebola kwa Tanzania na Kenya ni dogo sana. Hivyo ili kuongeza wateja hakikisha unakuwa mbunifu na kulenga changamoto na mahitaji ya wateja.

10. Shirikiana na biashara au kampuni kubwa
Hebu fikiri kampuni kama Vodacom au Airtel wakikutaja kwenye matangazo yao kuwa wewe ni wakala wao; je unafahamu ni nini kitatokea? Moja kwa moja utafahamika zaidi pamoja na kile unachokifanya na utaongeza wateja zaidi. Kumbuka kushirikiana na kampuni au biashara nyingine kubwa hukufanya pia uaminike zaidi kwa wateja.

Hitimisho
Naamini sasa umeona jinsi unavyopoteza wateja na faida bila sababu yoyote ya msingi. Fanyia kazi mbinu jadiliwa hapo juu nawe kwa hakika utaweza kuongeza wateja na hatimaye kupata faida zaidi.

Michango ya wadau:
----
----
----
 
Ahsante kwa elimu uliyotoa hapa; naamini itanisaidia sana tena sana
 
Endapo una mtaji mdogo na unataka kuanza na kukuza biashara yako. Fanya yafuatayo;

1. JIPE MUDA, BIASHARA HAITAWEZA KUKUA HARAKA KAMA UNAVYOFIKIRI
Uzuri wa kuanza biashara na mtaji kidogo ni kwamba kila mtu anaweza kufanya hivyo. Lakini pia urahisi huu wa kuanza biashara kwa mtaji kidogo unafanya ukuaji wa biashara kuwa wa taratibu sana. Hivyo unapofanya biashara yoyote ambayo unaanza na mtaji kidogo ni muhimu ukajipa muda ili kuweza kukuza mtaji wako.

Usiwe na tamaa ya kutaka kukuza biashara hii haraka, unaweza kuingia kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu zaidi. Endelea kufanya biashara yako huku ukijifunza zaidi na kuangalia kila fursa ambayo unaweza kuitumia kukuza biashara yako.

2. KUZA MTAJI WAKO TARATIBU
Kwa mtaji huo mdogo ambao umeanza nao biashara, endelea kuukuza kila siku. Usiendeshe biashara kwa kula kila kipato unachopata, badala yake tenga sehemu ya akiba irudi kwenye biashara yako.

Fanya hivi kwa nidhamu ya hali ya juu sana na unahakikisha kila unapopata faida sehemu inarudi kwenye biashara yako.

Pia endelea kuangalia kwa mazingira uliyonayo na kwa biashara unayofanya ni kwa jinsi gani unaweza kukuza mtaji wako zaidi. Kama utafikiria hili kila siku, hutakosa majibu ambayo yatakusaidia.

3. PUNGUZA GHARAMA ZA BIASHARA NA ZA MAISHA PIA
Kuwa kwenye biashara haimaanishi kwamba ndio una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na fedha za biashara hiyo, kwa sababu tu ni zako. Wewe sasa upo kwenye wakati mgumu wa kukuza biashara yako huku ukiwa huna njia nyingi za kufanya hivyo.

Hebu kwa sasa punguza kabisa gharama zako za kibiashara na za maisha pia. Kama kitu sio muhimu sana basi usikigharamie. Punguza matumizi yote ambayo ni ya anasa tu na sio kwa ukuaji wa biashara. Katika kupunguza gharama zako za biashara na maisha, jijengee nidhamu nzuri sana ya fedha. Usitumie fedha kiholela tu, kuwa na mahesabu na sababu kwa nini umetumia fedha fulani, hasa kwa matumizi ambayo sio ya kawaida.

4. ANGALIA WATU AMBAO UNAWEZA KUSHIRIKIANA NAO
Baada ya kuiendesha biashara yako vizuri na ukaona inaenda kwa faida, unaweza kuangalia watu ambao unaweza kushirikiana nao kwenye biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wanaweza kuwa na mtaji lakini hawana muda wa kufanya biashara.

Lakini pia watu hawa wanataka mtu ambaye wanaweza kumwamini. Hivyo kama unaweza kuaminika angalia watu unaoweza kushirikiana nao kibiashara.

Andaa mpango mzuri ambao utamshawishi mtu ni jinsi gani yeye atafaidika kama atawekeza kiasi kidogo kwenye biashara yako. Ikiwa unaendesha biashara yako kitaalamu itakuwa rahisi zaidi kushawishi watu kushirikiana na wewe.

5. RASIMISHA BIASHARA YAKO ILI KUJIWEKA KWENYE NAFASI NZURI YA KUPATA MKOPO
Hata kama biashara yako ni ndogo kiasi gani, irasimishe. Iendeshe kisheria kwa kuwa na namba ya mlipa kodi na hata leseni pia. Hivi vitakuwezesha wewe kutambulika na taasisi za kifedha pale utakapohitaji msaada zaidi wa kifedha.

Mkopo kwenye taasisi za kifedha ni chanzo muhimu ila usikimbilie kama bado hujaweza kuiendesha biashara yako kwa faida. Hakikisha umeiweka biashara yako vizuri kwanza na inajiendesha kwa faida ili unapochukua mkopo unajua unauweka wapi na kuendelea kupata faida zaidi.

Kuikuza biashara pale ambapo umeanza na mtaji kidogo ni kitu ambacho kinawezekana. Ila unahitaji kujitoa na kujenga nidhamu kubwa. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wafanyabiashara wengine, unahitaji kuwa mbunifu wa hali ya juu na pia unahitaji kujijengea uaminifu.

Ukishajua wewe biashara yako ni ndogo na inahitaji kukua, basi hakikisha kila mara unaumiza akili yako ifikirie njia zaidi za kuikuza. Na kama utaweza kufanya hivi basi utaziona fursa nyingi zilizokuzunguka za kuikuza biashara yako.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…