Fahamu mbinu mbalimbali za kuongeza mauzo ya biashara yako

Habari rafiki?
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hivyo ujanja siyo kuzikimbia changamoto, bali kukabiliana nazo na kuzishinda ili kuweza kusonga mbele zaidi. Hii ndiyo sababu kupitia AMKA MTANZANIA tuna kipengele cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia malengo makubwa tunayojiwekea kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunakwenda kupeana ushauri juu ya changamoto zinazowazuia watu kuanza biashara. Kwa zama hizi tunazoishi sasa, biashara ni kitu muhimu mno, iwe umeajiriwa au hujaajiriwa, unahitaji kuanzisha na kukuza biashara yako ili kuweza kujitengenezea uhuru wa kifedha. Na siyo lazima uache kazi yako ndiyo uanzishe biashara, kama ambavyo nimeeleza kwenye kitabu hiki; kukipata) unaweza kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa.

Imekuwa ndoto ya wengi kuanza biashara, lakini maswali ya awali kabisa ni nifanye biashara gani? Nianzie wapi? Nipate wapi mtaji? Nipate wapi soko la uhakika? Sasa leo kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kuangalia pa kuanzia, namna ya kupata soko, mtaji na hata jinsi ya kuikuza biashara yako. kabla hatujaingia kwenye ushauri wenyewe, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Mimi ni mpambaji, nadarizi ila nasumbuliwa na mtaji na soko na ni mfugaji mzuri wa kuku wa mayai ila kwa sasa nipo nipo tu sijui hata pakuanzia naomba ushauri wenu na msaada wenu. Amina S. A
Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayomsumbua msomaji mwenzetu, na nina hakika wapo wengi ambao wana changamoto kama hiyo. Swali ni je unatokaje hapo ulipo? Moja kwa moja tunakwenda kuangalia hatua unazoweza kuchukua, tukitumia mfano wa msomaji mwenzetu na mingine kwenye hali kama hizo.

HATUA YA KWANZA; Anzia hapo ulipo, hiyo ndiyo biashara uliyonayo tayari.

Kitu kimoja ambacho nataka kukuambia mwanzo kabisa ni kwamba hapo ulipo tayari una biashara, ni wewe kuijua na kuanza kuifanyia kazi. Je kuna kitu ambacho unapenda kufanya? Au kuna kitu ambacho una ujuzi nacho? Je kuna uzoefu wowote umepitia kwenye maisha yako ambao wengine hawajaupitia? Je kuna elimu uliyopata ambayo wengine hawana au wanaihitaji? Au je umeajiriwa au kuna watu walishakulipa kutokana na kitu ulichokifanya? Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote kati ya hayo hapo juu, basi tayari biashara unayo.

Kwa mfano wa msomaji mwenzetu hapo juu, ana ujuzi wa kupamba na wa kudarizi. Tayari ana biashara, tena nzuri sana ya kupamba na kudarizi. Kwa mwingine inawezekana ni ujuzi wa afya, au kilimo. Mwingine anaweza kuwa anapenda kuandika, mwingine kuimba. Mwingine anapenda kufuatilia michezo, au kutumia mitandao ya kijamii. Vyote hivi unaweza kuvigeuza na kuwa biashara.

HATUA YA PILI; Angalia ni nani mwenye uhitaji wa kile unachofanya au unachotaka kufanya.

Ukishajua kile ambacho unacho, ambacho ndiyo unakigeuza kuwa biashara yako, angalia ni watu gani watahitaji huduma au bidhaa yako. Angalia ni watu gani ambao wana shida au mahitaji ambayo wewe unaweza kuyatimiza kupitia kile ambacho unakifanya.

Kwa msomaji wetu aliyetuandikia, wateja wake ni watu wanaofanya sherehe mbalimbali kama harusi au mahafali. Wateja wake pia ni watu wanaopenda mavazi yaliyodariziwa.
Kama vitu unavyofanya wewe ni vingine, angalia watu gani wanaweza kunufaika navyo.

Kama unapenda kufuatilia michezo, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia yale unayofuatilia leo. kama unapenda kutumia mitandao ya kijamii, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia wewe kuwa kwenye mitandao ya kijamii. Kama unapenda kuandika, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika na kile unachoandika. Kila unachofanya, wapo watu ambao wanakitafuta kwa hamu, ni jukumu lako kuwajua na kuwafikishia kile unachofanya.

HATUA YA TATU; Wape watu kile unachotoa bila ya malipo.

Hapa ninachukulia kwamba unaanzia chini kabisa, ambayo ni sehemu nzuri sana kuanzia kwa sababu sasa hivi huna namna ambavyo unatengeneza kipato. Hivyo unaweza kutoa huduma zako kwa wengine bila hata ya kulipwa. Kama unachotoa ni bidhaa basi anza kutoa kwa bei ya chini sana, ambapo hupati faida yoyote. Lengo ni watu wakujue wewe ni nani kwanza, hapo ulipo sasa hakuna anayekujua na hata ukiwaambia kuna kikubwa unaweza kufanya hakuna anayeweza kukuamini, hivyo unahitaji kujijengea uaminifu.

Kwa msomaji mwenzetu aliyetuandikia hapa, anaweza kuanza kutoa huduma zake za upambaji bure kabisa. Angalia sherehe mbalimbali zinazofanyika pale unapoishi na omba kujitolea kupamba bure kabisa, wao wanunue tu mapambo. Au kama hizi hakuna, tafuta watu wanaofanya upambaji, ambao tayari wameshajijengea majina, waombe kujitolea kuwasaidia kazi bure kabisa, wasikulipe chochote. Lengo hapa ni wewe ujifunze, pamoja na kuwaonesha wengine kile ambacho unacho. Pia kwenye kudarizi hivyo hivyo, anza kudarizi vitu vya nyumbani kwako/kwenu na wasaidie watu kudarizi. Kadiri watu wanavyoona kazi zako ndivyo wanavyotaka kufanya kazi na wewe.

Kwa shughuli nyingine kama uandishi, tafuta njia ya kuwafikishia watu maandishi yako kwa bure kabisa. Anza kwa kuwa na blog, na andika mara kwa mara, kwa kuanza fanya kila siku, andika hata kwa siku mara mbili au mara tatu, andika sana, andika vitu ambavyo mtu akivifanyia kazi maisha yake yatakuwa bora.
Kama unachofanya ni kufuatilia michezo, anza kuwapatia watu uchambuzi wa ile michezo ambayo unafuatilia, toa historia za ile michezo ambayo unaifuatilia, hakikisha watu wanapotaka taarifa kuhusu michezo hiyo, wanakuja kwako kwanza.

Hatua hii ya tatu ni hatua muhimu kwani hapa ndipo watu wanapokujua na kuanza kuwatengenezea utegemezi. Wafanye watu wakutegemee wewe kupitia kile ambacho unawapatia. Kumbuka kwenye hatua hii hakuna faida yoyote unayotengeneza, unatengeneza jina kwanza.

HATUA YA NNE; Anza kutoza gharama kwa wale wanaotaka zaidi ya unachotoa.

Ukishatengeneza jina lako, na watu wakaanza kukutegemea kutokana na matokeo bora unayotoa, sasa unaweza kuanza kuwatoza watu kwa kile cha ziada wanachotaka uwafanyie. Ni wakati gani w akufanya hivi utaona tu inakuja yenyewe, watu wataanza kukuuliza wenyewe kama unaweza kuwasaidia kwenye mambo yao yanayohusika na unachofanya, na wao wenyewe watakuuliza wakulipe kiasi gani. Hii ndiyo hatua muhimu kwako kujenga msingi sahihi na imara wa kibiashara.

Kwa mfano ambao msomaji mwenzetu ametuandikia, hapa ndipo unapoanza kutoa huduma yako ya upambaji kwa gharama. Hapa umeshatengeneza jina lako, umeshashiriki kwenye sherehe nyingi na watu wameanza kuambiana kuhusu wewe. Hapa umeshawaangalia wengine wanaofanya wana mapungufu gani na wewe unakuja na suluhisho bora kabisa.

Kama ni uandishi watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwapa ushauri wa moja kwa moja, au kama kuna vitabu umeandika ambapo watu wanaweza kujifunza zaidi. Kama ni matumizi ya mitandao, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwatangazia biashara zao kupitia mitandao ya kijamii. Kama ni ufuatiliaji wa michezo, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwaelimisha zaidi kuhusu michezo hiyo, au kuwasaidia kutabiri michezo hiyo. Yapo mengi ambayo watu watahitaji kutoka kwako.
Unapofikia kwenye hatua hii ya nne, unahitaji kuwa umepitia biashara za wengine na kuona ni vitu gani unahitaji kufanya tofauti ili uwe bora zaidi ya wengine.


HATUA YA TANO; Kuza biashara yako.

Unapofika hatua hii ya tano sasa una biashara ambayo ina wateja, ambao wapo tayari kukulipa ili kupata bidhaa au huduma unayotoa. Hapa sasa ndiyo unaweza kusema una biashara, na unachohitaji kufanya hapa ni kuikuza biashara yako. unaweza kuona ndiyo sehemu rahisi, lakini ukweli ni kwamba hii ni sehemu ngumu, kwa sababu kila siku unahitaji kuja na mbinu mpya na bora za kukuza biashara yako.

Katika hatua hii ndiyo unaweza kuchukua mkopo wa kibiashara, kwenye hizo hatua nyingine za nyuma kamwe usichukue mkopo, utajipoteza. Chukua mkopo ukishakuwa na biashara ambayo tayari ina wateja wanaokulipa kwa kile unachofanya.
Hizi ndizo hatua tano muhimu ambazo mtu yeyote anaweza kuzitumia kutoka chini kabisa mpaka kufikia kumiliki biashara kubwa na yenye mafanikio.

Maswali ya haraka haraka na majibu yake;

Swali
; je hatua hizi tano ni rahisi?

Jibu; hapana siyo rahisi hata kidogo, unahitaji kuweka juhudi kubwa sana, unahitaji kujifunza kila siku, unahitaji kuacha uvivu na unahitaji kubadili maisha yako moja kwa moja.

Swali; itanichukua muda kiasi gani kuanzia hatua ya kwanza mpaka hatua ya tano?

Jibu; ukiweka juhudi vizuri, ukajifunza vyema na kufanyia kazi yale unayojifunza, itakuchukua mwaka mmoja mpaka miwili. Ukiwa mzembe itakuchukua muda mrefu zaidi na hivyo utakata tamaa haraka. Ukitaka kufanya haraka zaidi ya hapo utashindwa kabisa.

Fanyia kazi hatua hizi tano kwenye biashara unayotaka kuanzisha kwenye maisha yako, na utajijengea biashara kubwa na yenye mafanikio. Muhimu ni uwe mvumilivu na ujitoe sana kwenye kile unachofanya. Usikate tamaa na jifunze kwa wengine ambao wamefanikiwa kwenye kile unachoanza kufanya wewe.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea ,
 
Kama wewe ni mjasiriamali au mfanyabiashara unaehangaika kupata wateja kutokana na ushindani basi naomba unisikilize kwa umakini sana, kwani katika makala hii nataka nikuonyeshe mbinu ambayo itakusaidia:-

  1. Kuua ushindani kwenye soko lako na
  2. Kuwafanya wateja wavutiwe kuja kununua bidhaa/huduma unayotoa kutoka kwako badala ya washindani wako.

Tofauti ya stretejia (mbinu) hizi mbili inatokana na mfano ambao ametoa wa mapapa wenye kutafuta samaki.

Anasema mfanyabiashara ni kama papa mwenye kutafuta eneo lenye samaki samaki kwa ajili ya kula. Na samaki ni mteja wa mfanyabiashara yule.

Papa huyo akigundua eneo lenye samaki na kuanza kula wale samaki, baada ya muda fulani atapita papa mwengine kuja kula samaki katika eneo lile.

Na baada ya muda atakuja mwengine na mwengine hadi itafika wakati papa hao wanakuwa wengi kuliko idadi ya samaki na wanashtukizia kuwa wanatafunana wenyewe kwa wenyewe hadi damu kumwagika na kufanya rangi ya ile bahari kuwa nyekundu, na ndio maana ikaitwa red ocean strategy.

Huo ndio mfano wa wafanyabiashara wengi.

Utakuta mtu anaanzisha duka lake. Mambo yake yanaenda vizuri na anaanza kupata wateja.

Mtu mwengine anaona ile biashara na kusema “Kumbe biashara ile inalipa! Wacha na mimi nianzishe duka langu.”,

Anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na yule aliyefungua duka la mwanzo. Baada ya muda, mwengine nae anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na wale wawili.

Inafika wakati mlolongo wa watu wanafungua biashara kama ile na wanaingia katika ushindani hadi wanafikia 20, 30 hali ya kuwa idadi ya wateja bado ni ileile.

Inafika wakati wanajikuta wapo katika ushindani na biashara zote zinakuwa zinaumia.

Lakini Blue Ocean Strategy inakufanya wewe kujichomoa katika eneo lile la bahari na kuenda katika eneo jengine ambalo halina mapapa na kuwavuta samaki kuja kwako.

Na kwa vile lile eneo ni lako na ushaweka bendera yako hata papa mwengine akija hawezi kushindana na wewe kwa sababu eneo lile unalifahamu vizuri na samaki wale wamevutiwa na wewe kuliko mapapa wengine.

Vipi unaanzisha Blue Ocean Strategy?

Kwanza unatakiwa kufahamu kuwa kuna aina mbili za wajasiriamali au wafanyabiashara ambao ni
  1. Generalist na
  2. Specialist
Generalist ni mfanyabiashara anayewalenga wateja wote na Specialist ni mfanyabiashara anayelenga kundi fulani tu la watu na anafanya hivyo kwa sababu anajuwa kuwa hakuna mtu mwengine kama yeye anayeweza kutatua matatizo ya kikundi hilo kama yeye.

Ingawa watu wengi wanaona ni bora kuwa generalist kwa sababu soko lake ni kubwa, kitu wasichokifahamu kuwa kuwa generalist haitaji taaluma kubwa na soko lenye taalum ndogo linakuwa na ushindani mkubwa kuliko soko lenye taaluma ndogo.

Lakini ukiwa specialist unakuwa na uwezo wa kuwanasa watu wengi kwa sababu wewe unaonekana kuwa ni mtaalamu mbele ya macho ya soko lako na watu wanakufata wewe na wapo tayari kukulipa pesa zaidi kuliko yule mtu ambaye anaonekana anafanya kila kitu (generalist).

Na mfano mzuri ni kama madaktari.

Daktari ambaye anatibu wagonjwa wote ni generalist (MD) na daktari ambaye ni specialist anaona wagonjwa wachache lakini analipwa pesa nyingi na super specialist analipwa pesa nyingi zaidi kuliko wote.

Na kama wewe unataka kuua soko lako basi huna budi kuwa specialist au hata super specialist.

Mfano mimi (Dr Said) nilivyoanza biashara yangu niliingia katika soko la web design ambalo lilikuwa na ushindani mkubwa.

Nilianza kuwatengenezea tovuti wafanyabiashara, lakini nikaona nikijiweka kama Web Designer watu watanifananisha na Web Designer wengine na kunihoji kuhusu bei zangu kuwa juu kulinganisha na web designers wengine.

Hivyo sikujiweka kama Web Designer, na hata nilipokuwa nawapigia simu nilikuwa nikiwaambia

“Hello! Kwa jina naitwa Dr. Said Said, ninawasaidia wafanyabiashara kama wewe kutumia tovuti kunasa wateja kwenye mtandao. Na sasa hivi natoa consultation ya bure ya saa 1. Je ungependa kupata consultation ya bure kujifunza namna unavyoweza kutumia tovuti yako kunasa wateja?”

Wengi walikuwa wanajibu kuwa wangependa kupata consultation hiyo.

Na mimi nikienda kule nawaonyesha njia wanazoweza kutumia kupata wateja kwenye biashara zao kupitia website (tovuti) na sio jinsi wanavyoweza kumiliki website yenye kupendeza.

Najua wateja wangu hawajali sana kuhusu kumiliki website nzuri kama wanavyojali kupata wateja kupitia website zao.

Kujiweka kwangu kama Specialist (Online Marketer) kumenisaidia sana kupata projects nyingi zenye thamani (Blue Ocean Strategy) badala ya kujitangaza kama web Designer ambayo ni Red Ocean fani yenye ushindani mkubwa.

Mbinu hiyo na wewe unaweza kuitumia katika biashara yoyote ile.

Tuchukulie mfano wa biashara ya tour:

Muda si mrefu nimetoka kupigiwa simu na mmiliki wa kampuni ya tour na anataka ushauri vipi aitumie website yake kupata wateja.

Kitu cha mwanzo nilichomwambia ni kujiposition vizuri kwenye soko kama specialist badala ya generalist, ushauri huohuo ambao niliokupa wewe nilimpa yeye.

Badala ya kusema sisi ni tour company ambao tunapokea wageni kutoka nje sema sisi tunaspecialise kuwasaidia kundi fulani la watu kupata jambo fulani.

Kwa mfano nina rafiki yangu ambaye yeye amejikita kwenye motorbike safari.

Anasema “Sisi tunashughulika na Adventure safari za Motorbike tu! Kama wewe hujui kuendesha pikipiki hapa sio kwako”.

Kwa haraka haraka unaweza kuona kuwa atapata wateja wachache lakini kwa vile hana ushindani, wateja anaowapata wanamtosha sana na anatengeneza pesa nzuri sana na anaweza kuweka chaji ambayo washindani wake hawawezi kuweka kwa sababu washindani wake hawafanyi motorbike safari.

Swali unalotakiwa kujiuliza nia nijiweke vipi kwenye soko kama mtaalam wa kitu fulani ili niwavute watu waje kwangu?

Siku zote angalia wateja wako wana matatizo gani na kitu gani maalumu utafanya.

Usijaribu kufanya mambo mengi . Chagua kitu kimoja tu cha kufanya.

Muhimu hilo tatizo liwepo katika soko na watu wachache waweze kutatua hilo tatizo. Kama wewe ni miongoni mwa hao wachache ambao wanaweza kutatua tatizo hilo basi nakuhakikishia utapata wateja wengi na utakuwa huna ushindani katika biashara yako.

Ifanyie kazi na unijulishe umefaidika vipi na mbinu hiyo.

Ni mimi mwenye kujali mafanikio yako,

Dr. Said Said
Mkurugenzi wa Online Profits

[Makala hii imechapwa na Abdallah Hemedi - Content Manager | Online Profits] .
 
Elimu nzuri sana,specialization ya biashara ni kitu kizuri sana na kuna faida kubwa, shida inakuja wengi wetu hatujui nini soko lina taka ndio maana tunapenda kutumia mfumo wa red ocean.............unaangalia wanacho uza wenzio,ukiona wanauza na wewe una uza hicho hicho.......
 
Biashara za Tanzania ni zaidi ya uijuavyo npo mkoa flani kanda ya ziwa kikazi nilichoona wanaofanya biashara ni wazawa na wenyeji tu nikawauliza wageni wng mbona nyie amchangamkii fursa wakaniambia wengi wao washafungua biashara ila zikafa ili wateja waje kununua kwako inabidii uwe kabila lao au uwe umeoa au kuolewa na mtu wa kabila lao.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…