De Opera
JF-Expert Member
- May 23, 2013
- 780
- 1,664
Habari ya muda huu Wapwa?
Natumaini mnaendelea vizuri kabisa, ila kwa wale ambao hamko vizuri kwa namna yoyote Mungu awaongoze mvuke katika hilo.
Wapwa, leo nagusia kuhusu uchangamfu katika biashara, mahusiano au sehemu zingine.
Kabla sijaendelea nikuulize, hivi ulishawahi kukaa, kuhudumiwa, au kuongea na mtu ambaye si mchangamfu?. Huwa unajisikiaje?
Jibu nadhani ni 'Ndio' na kiukweli inaboa.
Uchangamfu ni hali ambayo watu wengi tunapenda kuoneshewa yaani kuchangamkiwa.
Unaweza ukaenda dukani kununua kitu ila yule muuzaji alivo kaa kaa ukaahirisha ukaenda duka lingine kwa sababu amekaa kama ana makasiriko, amezubaa, kama kanuna hivi.
Au muda mwingine unaweza ukapita dukani ukajikuta umehemea pasipo matarajio kwa sababu muuzaji kakuchangamkia, kakushawishi hadi ukaamua kuanika pochi yako nje.
Hata kwa watoto pia. Mtoto mchangamfu huwa anapendwa na watu wengi, kila mtu atahitaji aishi naye, atembee naye.
Siku zote watu wachangamfu ndio huangukiwa na fursa mara nyingi. Michongo na madili kwao huwa kama gulio.
Unaweza kuwa na mtu (mpenzi/mke/mme/ n.k) umepanga kumfanyia 'surprise', unakutana naye kanuna, mzito kama kompyuta ya DDR1 250Mb. Au unampigia simu au ujumbe mfupi anakupa shortcuts, unashindwa hata hiyo surprise uisapraizi vipi, matokeo yake inabaki kwenye pocket.
Kuna watu automatically wao huwa wako hivyo, yaani dakika 5 tabasamu, zilizobaki zote hagusiki, sura ameikunja kama shati ambalo toka linunuliwe halijaonja joto la pasi.
Tutalalamika kuwa watu wengine wanabahati, kumbe sisi ndio wachawi wa hizo bahati.
Mapokezi ya mtu yanaweza kukuvunja moyo au kukupa nia.
Uchangamfu ni kama connector au kiroho tunasema 'Imani au Nia'. Ili Mungu aweze kujibu ombi lako lazima imani yako iwe thabiti.
Hivi ulishawachunguza watoto?
Watoto huwa wanaangalia mtu alivyowachangamkia, ndio nao huchangamkia.
Lakini mtoto akiona unamakasiriko, hutabasamu, umenuna, kamwe huwezi kuwaona karibu yako. Watakuona kama adui, ndio maana haipaswi kuonesha makasiriko mbele ya watoto.
Kwa hiyo, uchangamfu ni kitu muhimu sana katika maisha tunayoishi. Tusikae kulaumu biashara haiendi, ni vile uso wako unavyoonekana kwa wateja.
Tusikae kulaumu hatupati wenza, ni vile tunavowapokea, wanakata tamaa na kwenda zao.
Naufunga ukurasa wangu siku ya leo. Ahsanteni kwa kuwa nami.
Kwenye mitandao ya kijamii nifuate as De Opera au @deoperacc, siku njema wapwa.
