UNCLE THREE
Member
- Jul 20, 2021
- 25
- 88
FAIDA ZA KUWA WAZALENDO
UTANGULIZI
Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini na kujitoa kwa ajili ya nchi yake na kuweka maslahi ya nchi mbele na ya kwake binafsi nyuma. Na mara nyingi mzalengo huwa mzawa na mwenye kuipenda nchi yake na huweza kujitoa mhanga hata wakati mwingine huweza kufa kwa ajili ya nchi yake. Uzalendo unabeba dhana nyingi sana ikianzia asili, utamaduni, lugha, siasa na historia ambapo dhana zote hizo hufungamana kwenye dhana kuu ya utaifa. Mfano wa wazalendo wa kihistoria wa nchi yetu ni Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaweza kuwa mfano mzuri wa Mtanzani mzalendo na Edward Moringe Sokoine pia anawekwa kwenye orodha ya watanzania wazalendo ambao kwa kweli waliipigania hii nchi na watu wake na rasilimali zake hata na kupoteza maisha yake.
Ili mtu aweze kuitwa mzalendo wa kweli ni lazima awe na sifa kama vile;-Kuzaliwa nchini na angalau mzazi mmoja au wote wawili wawe ni wazawa, Ni lazima awe mwaminifu wa kulipa kodi, kutoibia nchi kwa njia yeyote, Kutokuwa mharibifu au mvujaji wa mali na rasilimali za nchi, Kuwapenda watu wote, hata viongozi wanaoijenga nchi bila kujali uchama, udini, ukabila wala rangi yake, Kuwapiga vita na kuwapinga kwa nguvu zote raia wote wanaobomoa na kuharibu nchi hata kama ni wa chama chake, dini yake, kabila lake, rangi yake au ndugu na jamaa zake, Kusaidiana na viongozi wake kuijenga nchi bila kujali uchama, udini, ukabila wala rangi yake na Kuweka juhudi kubwa katika kuisema na kuitangaza nchi yake vizuri ndani na nje ya mipaka yake.
FAIDA ZA RAIA KUWA NA UZALENDO
UONGOZI BORA
Kama raia wote wa nchi yetu wakiwa na uzalendo na nchi yetu ni hakika kwamba tutapata viongozi bora ambao watasimika uongozi bora unaofuata misingi ya uongozi bora na kuondokana na vitu vinavyotia doa uongozi kama vile rushwa, ufisadi, ubaguzi, upendeleo na siasa za uongo. Mfano Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amekuwa mfano bora wa kiongozi bora aliyesimama imara kutetea maslahi ya nchi yake na kuweka nyuma maslahi yake binafsi.
KUKUA KWA UCHUMI
Uzalendo na kupanda kwa uchumi ni vitu ambavyo vinategemea kwa kiasi fulani kwa maana kama raia wa nchi husika wakiwa wazalendo basi watakuwa waaminifu katika kuchangia kupanda kwa pato la taifa kutokana na utaoaji kwa kodi kwa uaminifu masipo uhujumu na ukwepaji kodi. Lakini pia wananchi wakiwa wazalendo watapenda vitu vyao na kupeleka kukua kwa viwanda vya ndani kwa uwepo wa soko la uhakika. Kwa nchi zilizoendelea kiuchumi kama vile Marekeni na uingereza wafanyabiashara wa nchi hizo wanakuwa waaminifu katika ulipaji kodi, mapato hukusanywa kwa uaminifu na wanakuwa wanathamini na kupenda bidhaa zao jambo ambalo linapelekea kukua kwa uchumi siku hadi siku.
MATUMIZI MAZURI YA RASILIMALI NA MIUNDOMBINU
Nchi ya Tanzania imejaliwa Rasilimali nyingi kama vile misitu, mbuga za wanyama, madini, vyanzo vikubwa vya maji na ardhi yenye rutuba. Lakini pia kuna miundombinu mizuri na endelevu kama vile bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Treni ya umeme, madaraja makubwa, bandari na miradi mingeneyo mingi. Miradi hii yote pamoja na rasilimali hizi haviwezi kudumu na kuwa na faida kwa vizazi vijavyo endapo raia wa Tanzania hawatakuwa na uzalendo wa kuvitumia vitu hivyo kiuendelevu kwa manufaa ya sasa na siku zijazo. Kwa mfano vitendo vya ujangiri wa wanyama pori, uvamizi wa misitu, uharibifu wa miundombinu kama vile vyanzo vya maji sio tabia ya raia mzalendo.
KUTOKOMEZA UBAGUZI WA KIKABILA NA KIDINI
Uzalendo ni chachu ya kutokomeza matabaka na tofauti zinazoletwa na dini na ukabila na Vyama vya siasa. Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema kuwa katika Karne ya 21 nchi ndogo za dunia ya tatu kama Tanzania tunapaswa kujiepusha na ubaguzi wa kidini, kikabila na kikanda ili tuweze kuendelea kuitunza amani iliyosimikwa na viongozi waasisi ta Taifa letu. Mfano Mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 yalipelekewa na suala la ukabila ambapo takribani watu 800,000-1,000,000 ambao ni 20% ya raia wa Nchi ya Rwanda walikufa. Hivyo suala la ukabila na udini ni masuala ambayo kama wazalendo tunapaswa kujiepusha nayo kwa maana sisi site tu Watanzana wazungumzaji wa Lugha moja, na dini zote Waisamu na wakristo tu watoto wa taifa moja na Mungu wetu ni mmoja.
AMANI, UMOJA NA UPENDO
Tanzania imekuwa nchi ya kuigwa kwa kuwa kisiwa cha amani tangu ilipokuwa nchi huru. Hii ni kutokana na kuwepo kwa viongozi na raia wazalendo wanaweka maslahi yao kando na kuweka mbele maslahi ya taifa letu. Na hata katika Wimbo wa taifa letu una maneno yanayoasa raia kuwa na hekima, umoja pia na amani. Hivyo uzalendo ukiwepo nchi itaendelea kuwa na amani kama ilivyo kwa nchi yetu tangu ilipopata Uhuru. Kwa mfano nchi kama Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 kulitokea machafuko na uvunjifu wa amani, umoja na upendo kwa sababu ya raia kutokuwa na ukomavu katika suala la uzalendo na kufarakanishwa na ukabila na uchama.
HITIMSHO
Malmaka za Elimu, Taasisi ya Elimu, watunga sheria na wadau wa elimu wanatakiwa kuangalia jinsi ya kufanya ili mbali na uzalendo kufundishwa kama kipande kidogo cha mada ndani ya somo la uraia (civics) lakini pia kunahitajika mkazo katika ufundishaji wa mada ya uzalendo kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu ili kupata zao la raia wema wanaoipenda nchi yao na kudumisha amani toka kizazi hadi kizazi.
Upvote
21