Fanya hivi ili uweze kukwamuka umasikini

Fanya hivi ili uweze kukwamuka umasikini

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Pengine umekuwa ukiwaza sana nini ufanye ili
uweze kufanikiwa na kuondokana na adha za
umaskini. Yako mambo mengi ya kufanya mimi

nataka kukufungua macho kwa jambo moja tu

tena kwa uchache. Jambo hili anaweza kulifanya
mwenye mtaji mkubwa au mdogo.Viko vitabu
vingi na tena siku hizi zinatolewa DVD za jinsi ya
kufanikiwa katika maisha.

Utashangaa mpaka

unamaliza kusoma au kutazama DVD hizo
hujapata njia ya wazi sana sana utajilaumu tu
kwa kuendelea kupoteza fedha kwa kuchangia
miradi ya wajanja hao. Wengine wanakuambia
"amini tu kuwa wewe ni tajiri na utafanikiwa"
mh!

INAWEZEKANA? Afadhali hao, balaa zaidi ni
wale ambao wanayanadi mafanikikio na utajiri
kwa mizizi, hirizi na hata roho za binadamu
wenzao!

Somo langu ni dogo lakini naamini wapo
watakaopata mafanikio makubwa sana. Sasas
kuwa makini zaidi. Unaweza kuanza kwa mtaji
wa Mil.1 mpaka laki tano au hata chini ya hapo.

Mfano. Unaweza kutumia Tsh 250,000 kununua
kuku 25 kwa bei ya Tsh 10,000 kwa kuku mmoja
(kadirio la juu) Majogoo watakuwa 5 kwa uwiano
wa 1:4 . Hii ina maana kuwa wakishaanza
kutaga utakuwa na vifaranga 20 x 10 = 200

Watunze vizuri. Wale vifaranga tunakadiria kuwa
makoo(majike) watakuwa 150 ambao ndani ya
miezi 3 au zaidi nao wataanza kutaga. Utakuwa
na kuku 200 + 25 =225 ndani ya miezi 6. Miezi 6
inayofuata 225 - (majogoo 55) = 170 Hii ina
maana kuwa 170 x 10= 1,700. Ndugu

mwanajamvi hayo niliyotoa ni makadirio ya chini
sana hivyo mpaka mwisho wa mwaka utakuwa
na kuku zaidi ya 2000. Mwaka utakaofuata
utakuwa na kuku wangapi baada ya kuuza kuku
1,000. Mwaka 2. 750(majike) x 10 = 7500 (uza
wengine) 3000 x 10 = 30,000. Kutegemea na
uwezo wako mpaka mwisho wa mwaka wa pili

utakuwa umefanikiwa sana. Kumbuka huu ni
mwongozo tu, fanya utafiti na ufuatilie zaidi
huku ukiacha kando uzushi wa vitabu vya

wasanii na DVD zao pia. NB. Kumbuka kuku
ninao wazungumzia hapa ni wale wa kawaida sio
wale mataahira (wa kisasa).Fuatilia zaidi kuhusu
matibabu na matunzo mengineyo.

MAELEZO ZAIDI
UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI

Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambaye
ameniwezesha kwa namna moja au nyingine
kutoa mchango wangu kwa mtindo huu. Huu ni

kama mwongozo tu wa nini utakabiliana nacho
au unatakiwa kufanya katika zoezi zima la
ufugaji wa kuku wa kienyeji. Nimeamua kuuleta

kwenu wana JF ili kwa mtu mwenye malengo ya
kufanikiwa kupitia ufugaji wa kuku ajue
mlolongo mzima na changamoto ambazo
atakabiliana nazo.

A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?

1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu
wakikingwa na magonjwa ya kuku kama
mdonde, ndui ya kuku n.k ili kuweza
kuwaendeleza.

2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.

3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na
kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira
magumu kama ukame, baridi n.k

4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko
kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA
KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)

5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama
mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu
muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri,
wakawekwa kwenye mabanda mazuri,
wakapewa maji na chakula cha kutosha.

B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.

Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza
zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni
ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata
maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza
kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba
mbadala)

- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika
kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama
mapambo.

Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:

Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu
na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza

Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji
unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili
ya uendelezaji wa kuku

C:MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini
hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi.
MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri
ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia
kuchanja kuku kwa wakati.

D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu
makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna
ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila

hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi
kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo
kuku hawa wana tofauti za kimaumbile

zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo
wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia
zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku
wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji
wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao

Mfano:

a. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni

b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale
wenye manyoya yaliyosimama.

c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi
kichwani.

d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha
kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko.
Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na
alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au
Kibutu.

Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza
kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa
kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo
wanakotoka.

(i) KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama
mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache
mwilinini na hasa kifuani, vilemba vyao ni
vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa

Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana
uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa
hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza,
Shinyanga, Tabora na Zanzibar.

(ii) CHING'WEKWE
Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa
mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa
zifuatazo.

Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea
wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku
hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi

maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia
sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai
mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa
kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa
sana kwa biashara ya mayai.

(iii)UMBO LA KATI

Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9,
Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa
wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti.
Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua
upesi na hupata kinga upesi baada ya

kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo
(Castle desease)

Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka
kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo
mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika
anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito
wa kutosha pia kutaga mayai mengi na
makubwa.

(iv) SINGAMAGAZI

Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji
wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana
utambulisho maalum kutokana na rangi zao.
Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea
huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito
wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2
mayai gramu 56.

(iiv) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya.
Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani
ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana
damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop".
Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49

(iiiv)PEMBA
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea
Kg 1 mayai wastani gm 42

(xi) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6,mitetea kg 1.2 mayai gm 42.
Kuku hawa wa Unguja na Pemba
wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa
ni wadogo.

SEHEMU YA PILI
1. MIFUMO YA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI.
A. MFUMO HURIA

Katika mfumo huu kuku huachiwa wakitembea
toka asubuhi wakijitafutia chakula na maji na
kufungiwa kwenye vibanda visivyo rasmi wakati
wa usiku. Huu ni mfumo rahisi lakini si nzuri
kwa mfugaji wa kuku wengi kwani atahitaji eneo
kubwa la ardhi.

FAIDA.
Mfumo huu una faida za gharama ndogo za
uendeshaji kiujumla.

HASARA
Uwezekano mkubwa wa kuku kuliwa na
vicheche, kuibiwa mitaani n.k
Kuku huweza kutaga popote na kusababisha
upotevu mkubwa wa mayai.

Ni rahisi kuku kuambukizwa magonjwa
Utagaji unakuwa si nzuri kulingana na
mabadiliko ya hali ya hewa.

Uwekaji kumbukumbu si nzuri.
Ni vigumu kugundua kuku wagonjwa hivyo
kusababisha ugumu katika utoaji wa tiba.

UTUMIAJI NZURI WA MFUMO HUU

Kuku wajengewe banda kwa ajili ya kulala
nyakati za usiku na liwasaidie wakati mwingine
wowote hali ya hewa inapokuwa si nzuri.

Kuku wapatiwe chakula cha ziada na maji.
Kuku waandaliwe kwa viota vya kutagia.
Kuku 100 ni vizuri wakitumia eneo la ardhi la
ekari 1.

B.MFUMO NUSU HURIA
Huu ni mfumo ambao kuku hujengewa banda
rasmi na banda hilo huzungushiwa uzio/ wigo.
Mfumo huu ni ghari kiasi ukilinganisha na
mfumo huria lakini huweza kumpatia mfugaji
faida haraka sana.

FAIDA
Sehemu ndogo ya kufugia hutumika kuliko
ufugaji huria, utunzaji wa kuku ni rahisi
ukilinganisha na mfumo huria, Ni rahisi kutibu

magonjwa ya mlipuka kama mdondo (Newcastle
desease), Upotevu wa kuku na mayai ni mdogo
sana ukilinganisha na mfumo huria.

C. MFUMO WA NDANI
Kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa
wakiwa ndani. Mfumo huu kuku huwekwa

kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa
kwa matandiko ya makapi ya mpunga, takataka
za mbao(randa), maganda ya karanga au majani
makavu yaliyokatwa katwa.

FAIDA
Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia,
uangalizi mzuri na rahisi wa kuku, Joto litokanalo
na matandiko lina uwezo wa kuua vimelea vya
maradhi, kuku wanakingwa na hali ya hewa
mbaya na maadui wengine.

HASARA
Uwezekano wa kuku kudonoana ni mkubw na
pia Gharama za ujenzi wa mabanda

UTUMIAJI MZURI WA MFUMO HUU.

1. Matandiko yageuzwe kila siku

2. Kila mara matandiko yawe makavu kwa kuwa
na madirisha yanayopitisha hewa ya kutosha,
ambayo yatatoa unyevunyevu hewa chafu
ikiwemo ammonia.

4. Mita mraba moja hutosha kuku 5 hadi 8.
UTATUZI WA KUKABILIANA NA VIKWAZO KATIKA
UFUGAJI.

Mambo ya kuzingatia:
Mabanda bora - Fuatilia kwa wataalamu wa
mifugo walio karibu nawe.

Sifa za banda bora (Waone wataalam wa
mifugo)
Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi
Kuwa makini na aina ya mitetea na majogoo
unatakiwa kuchagua ili kuwa na kizazi bora.

UTAGAJI WA MAYAI

Kwa kawaida kuku huanza kutetea(Kutoa mlio
wa ishara ya kutaga) anapofikisha miezi sita hadi
minane. Hivyo ni vyema viota viandaliwe
mapema wakiwa na umri wa miezi mitano. Kuku

anapoanza kutaga akifikisha mayai matatu
mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi
hayo matatu kila siku linapotagwa na kuliweka

alama ya tarehe au namba kwa kutumia penseli
ili kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la
kufikisha mayai 15 mpaka 20. Mayai

yanayoondolewa yawekwe kwenye chombo
kikavu kinachopitisha hewa ni vizuri pia kuweka
mchanga ndani ya chombo hicho.
Hakikisha ya fuatayo.
Sehemu iliyochongoka iwe chini na pana iwe
juu.

Hifadhi sehemu yenye hewa ya kutosha na
isiyohifadhi joto
Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki
mbili toka siku ya kuanza kutagwa.

UATAMIAJI WA MAYAI NA UANGUAJI WA
VIFARANGA

Uatamiaji na uanguaji wa kubuni - Mfumo huu
hutumia mashine za kutotoleshea vifaranga

(Incubators) hutumika kuangua mayai mengi kati
ya 50 hadi 500 kwa wakati mmoja Mashine
zinazotumika kutotoleshea vifaranga wa kisasa
zinaweza kutumika pia kutotoleshea wa kienyeji.
Uatamiaji na uanguaji wa asili

KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.

Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri
kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa
yaweze kuuzwa au kutumiwa nyumbani kwa
chakula. Mayai ya kuatamia yawe na sifa
zifuatazo

Yasiwe na uchafu yawe masafi
Yasiwe na nyufa
Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na
ukubwa wa wastani kulingana na umbile la
kuku.

Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha
kali sana.
Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili
toka yalipotagwa

Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye
joto.

KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA

Pamoja na matayarisho hayo zingatia
kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni vizuri
yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia

ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya
kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana
chawa, utitiri n.k. Kuwepo kwa wadudu hao

huwafanya kuku wakose raha na kutotulia
kwenye viota vyao. Hali hii husababisha
kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-

Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia
kuatamia
Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako
ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka kuwa na harufu
kwani kuku anaweza kuyasusa.

Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku
anayetaka kuatamia wakati wa usiku. Pia
ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia
mayai yake siku 21.

PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI MENGI
KWA NJIA ZA ASILI

Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati
mmoja ni vema ukawafanya wakaatamia na
kutotoa pamoja.

Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya
kuatamia ukianzia na yai la mwisho kutaga.

Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja
ili waanze kuatamia kwa pamoja na kupata

vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza
anapoanza kuatamia. Mwekee mayai viza au ya

kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai
yanapoanguliwa hivyo ukimuwekea mayai yasiyo
na mbegu atakaa hapo muda mrefu hadi
vifaranga watoke.

UTEKELEZAJI WAKE
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba
au tarehe kulinganisha na siku anayotaga

Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee
mayai viza au ya kisasa huku ukiendelea kuweka
alama mayai yanayotagwa kila siku.

Mara kuku anapoanza kuatamia muongezee
mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10

Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi
utakapoweza kupata idadi itakayoweza
kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.

Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa
kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea mayai
ya ukweli wakati wa usiku.

MUHIMU
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio
wazi na wala yasipate harufu za mafuta ya taa,
manukato n.k.

JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA
MBEGU NA YALE YASUYO NA MBEGU.

Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na
mbegu na yale yasiyo na mbegu siku ya saba
baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai
kwa kutumia box lililotengenezwa maalum

pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya
chumba chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji
ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa chakula
cha familia au kuyauza.

TAMBUA VYAKULA NA UZALISHAJI WA KUKU -
Sitalielezea hili naomba ufuatilie mwenyewe.

JIFUNZE MBINU ZA KUZALISHA KUKU WENGI
KWA MUDA MFUPI

Zoezi hili linawezekana iwapo uleaji wa vifaranga
kwa njia ya kubuni utatumika. Kuku mmoja
anaweza kutotoa zaidi ya mara saba kwa
mwaka.
Taz.

Hesabu ya uzalishaji wa kuku wengi kwa mwaka
kwa kutumia mtetea mmoja tu.
Mpaka mwisho wa mwaka unaweza kuwa na

idadi ya vifaranga 252 kwa kadirio la vifaranga 8
kila mzao. Hivyo kama una kuku 10
wanaotunzwa vizuri utakuwa umezalisha jumla
ya vifaranga 2520.

Fuatilia kwa wataalamu wa mifugo ili
ufundishwe zaidi kuhusu mbinu hiyo ya
kuzalisha kuku wengi.

ULEAJI WA VIFARANGA
NJIA YA KUBUNI
NJIA YA ASILI

Njia zote mbili zinafahamika kama huzifahamu
tafadhali fuatilia kwa mtaalamu aliye karibu
nawe.

MAGONJWA NA WADUDU WANAOSHAMBULIA
KUKU WA KIENYEJI NA JINSI YA KUKINGA.
A. MAGONJWA.

Ugonjwa hatari - Mdondo/ Kideri (Newcastle
desease) Hapo nyuma dawa ya kukinga ugonjwa

huu ilikuwepo lakini ilikuwa inahitaji kuhifadhiwa
kwenye hali ya ubaridi (Friji) Hali hiyo
ilisababisha iwe ngumu kutumika vijijini kwa

dawa hiyo. Hivi sasa kumepatikana chanjoa
ambayo inastahimili joto ambayo inaweza
kutumika hata vijijini.

Pamoja na mdondo yapo pia magonjwa
yanayoshambulia kuku hapa nchini
Ndui ya kuku(Fowl pox)

Mafua ya kuku(Infectious coryza)
Homa ya matumbo (Cocciodiosis)
Minyoo na wadudu kama viroboto, chawa, utitiri
na kupe wa kuku.

DALILI ZA KUKU MGONJWA.
Huzubaa
Hali chakula/maji vizuri
Hujitenga na wenzake
Hujikunyata au kuinama
Hutetemeka
Hutembea kwa shida
Utagaji wa mayai hupungua au hukoma kabisa

MAGONJWA YA KUKU HUSABABISHWA NA NINI?
Yako mambo mengi yanayosababisha lakini
matunzo hafifu pia huchangia.

ATHARI ZA MAGONJWA.
Hili liko wazi
Maelezo haya ya magonjwa ni mengi hivyo tuwe
wafuatiliaji kwa wataalam.
MATIBABU

KIDERI - Sifahamu tiba ya kitaalam ya ugonjwa
huu kama kuna ambaye anafahamu tunaomba
atufahamishe lakini ziko dawa za asili na za
kitaalam ambazo zinafaa zaidi kwa chanjo.

Ugonjwa huu unaweza kuukinga kwa kuwapa
kuku chanjo ya Mdondo. Pia usichanganye kuku
wako na kuku ambao huna taarifa zao za
chanjo.

KUMBUKA
Mdondo au kideri ni ugonjwa tishio ambao
huweza kuua kuku wote
Mdondo ukitokea vifo huwa vingi pia kuku

hupumua kwa taabu, hupooza na wengine
huzunguka na huzungusha vichwa.
Mdondo unaweza kuzuilika kwa chanjo kila
baada ya miezi 3

NDUI YA KUKU
HOMA YA MATUMBO (Fowly typhoid)
MAFUA YA KUKU(Infectious coryzya)
KUHARISHA DAMU(Coccidiosis)

Minyoo na wadudu wanaoshambulia kuku kama
viroboto n.k
Kwa magonjwa na wadudu tuliowataja hapo juu
please wasiliana na mtaalamu wa mifugo aliye
karibu nawe Kwani siwezi kueleza kila kitu hapa
wataalamu tunao naamini watatusaidia.

TIBA ZA ASILI
Kuna madawa ya asili ambayo hutokana na
mimea ambayo hukinga kuku.

BAADHI YA MIMEA INAYOTIBU NA KUKINGA
MARADHI YA KUKU.

MWAROBAINI - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na
vidonda
ALOEVERA - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na
vidonda,ngozi na Cholera. Tutaelekezana zaidi
namna ya kuandaa dawa hii.

Hapa nataka niorodheshe baadhi ya madawa ya
asili ambayo yanasaidia kutibu na kukinga kuku.
Mwarobaini, Aloevera, Mtakalang'onyo

(Euphorbia),Mbarika, mlonge, Ndulele/
dungurusi/tura/ndura, Majani ya mpapai,
Mwembe, Minyaa na Pilipili kichaa.

NAWASHUKURU PIA NAOMBA MWENYE
MCHANGO ZAIDI AENDELEE KUONGEZEA TUSIWE
WACHOYO WA MAARIFA KIDOGO GAWANA NA
MWENZIO
 
Tumekupata vilivyo MZIZIMKAVU, ahsante kwa somo tamu na lilotukuka.
Unaweza pia pitia thread ya ndugu KUBOTA yenye heading "ZIJUE MBINU ZANGU: UFUGAJI KUKU WA KIENYEJI " kuna mambo mengi sana yamezungumzwa hapo na ushahd tosha wa wadau juu ya ufugaji wa kuku wa kienyeji pamoja na dawa zote za asili na za kisasa za kutibu magonjwa ya kuku.
 
chakula gani nikiwapa watakua na afya nzuri na pia kuongeza utagaji wao wa mayai?
 
ahsante sana Mkuu, somo zuri sana utajiri ni kwa kila mtu, kinachoturudisha nyuma ni mipango na vipaumbele
 
ushauri mzuri sna huu,isipokuw sasa watz tulivyo na wivu,wakiona una mafanikio ya kufuga kuku,utashangaa mwngne anaanzisha mradi wa kufuga vicheche wanaokula kuku!!
Yaani nimecheka hadi nimetokwa na uchozi
solar_system_menu.jpg
 
Back
Top Bottom