Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Filamu zilizozuiwa kuonyeshwa hadharani na kwenye vyombo vya usafiri ni Filamu ya Mtoto wa Mama, Inye, inye Plus, Inye Ndembendembe na Inye Gwedegwede.
Sababu kubwa ya Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza kuzuia filamu hizo ni pamoja na filamu hizo kutokuwa na maudhui na maadili ya Kitanzania, ambapo zinaonyesha vitendo vya Ushoga sambamba na kudhalilisha wanawake hasa wanene kwa kugeuza miondoko yao ambayo inaamsha hisia za kingono.
Tunaipongeza Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza kwa kuzuia filamu hizo kuonyeshwa, ingawa hatujalidhishwa na utaratibu wanaotumia wa kuruhusu filamu zisizo na maadili ya kitanzania kurekodiwa na kuonyeshwa huku pia wakichelewa kukagua filamu nyingi zinazotengenezwa nchini kwa sababu zimeishasambaa kila kona ya nchini na watu wanazo majumbani kwao.
Tunasema hivyo kwa sababu watunzi na watengenezaji wa filamu hawatakiwi kutengeneza filamu bila kuwa na kibali cha Waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu filamu na michezo ya kuigiza na hawatakiwi kuonyesha filamu yoyote bila kukaguliwa na Bodi na kupewa daraja.
Tunapenda kuishauri Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza kuwa makini na kuendesha zoezi hilo la ukaguzi kila mwezi ili kuhakikisha filamu zilizo sokoni zinastahili kuangaliwa na watanzania na kuondoa sokoni filamu ambazo hazistahili.
Tunaamini zipo filamu nyingi ambazo zinatengenezwa bila kibali cha Waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu filamu na michezo ya kuigiza kwa sababu jinsi zilivyo wazazi hawawezi kukaa na watoto wao na kutazama filamu hizo pamoja.
Tunaishauri Bodi ya Filamu kutengeneza utaratibu wa kukutana na watunzi na watengenezaji wa filamu ili kupeana miongozo muhimu itakayohakikisha tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza inakua na kuzingatia maadili ya kitanzania.
Ni wazi Bodi ya Filamu wakikutana na watunzi na watengenezaji wa filamu watafundishana kuhusu maadili ya Mtanzania kwa sababu inavyoonekana asilimia kubwa ya watunzi na watengenezaji wa filamu hawajui maadili ya kitanzania na kama wanajua basi wanafanya makusudi kupotosha maadili ya kitanzania, ipo haja ya kufahamu maadili ya kitanzania yapo vipi.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi