SoC03 Filamu za Kitanzania zitumike kurithisha utamaduni na historia

SoC03 Filamu za Kitanzania zitumike kurithisha utamaduni na historia

Stories of Change - 2023 Competition

Damaso

JF-Expert Member
Joined
Jul 18, 2018
Posts
3,978
Reaction score
6,739
Habari jukwaa,

Dunia ina mabara saba ambayo yameruhusu watu kuweka maskani yao, hapo tunamzungumzia bara la Asia, Afrika, Ulaya, Australia, Amerika ya kusini, Amerika ya Kaskazini pamoja na Antarctica. Ukienda Asia utakutana na taifa kama India ambalo kwa mujibu wa mtandao wa indiantribalheritage.com wanadai kuwa India ina makabila takribani 705, tukija nyumbani Afrika hapa utakutana na makabila takribani 3000 na lugha zaidi ya 2000, ikiwemo lugha tamu sana ya Hausa, Igbo, Sukuma, Oromo, Amhara, Fulani, Akan, Somali, Yoruba na kadhalika, hizi ni lugha ambazo zinazungumzwa na watu zaidi ya bilioni 1.3.

IMG_1268.jpg


Kwa hapa Tanzania wasukuma ndo wanaongoza kwa kuchukua 13% ya idadi yote ya watu.
IMG_1270.jpg



Upande wa Marekani au Amerika ya Kaskazini wao wana lugha takribani 430 za asili ambazo zinazungumzwa na makabila ya wahindi wekundu zaidi ya 574.

IMG_1271.jpg


Unaweza kujiuliza kwanini nimeanza na hizi takwimu, ndio Nitakupa sababu;

Ukienda Marekani na kuuliza majina kama, Tatanka Iyotanke na Tasunke Witko kutoka kabila la Lakota basi utapewa hadithi na visa vingi vya kishujaa kuhusu hawa mashujaa, vivyo hivyo mashujaa wa makabila ya wahindi wekundu wamepewa heshima kubwa ya kuenziwa katika picha mjongeo na filamu bila kusahau tamthilia.

IMG_1272.jpg


Mfano filamu za Captured Hearts ya mwaka 1997, Gunsmoke; The Last Apache ya mwaka 1990, pamoja na tamthilia ya Yellow Stone iliyoanza kuoneshwa mwaka 2018 mpaka sasa. Kwa hakika utaona namna ya kipekee sana filamu inavyotumika kuwaenzi na kuonesha ushujaa wa mashujaa ambao walipambania jamii na makabila yao.

Swali la msingi ambalo najiuliza ni kuhusu tasnia yetu ya filamu inatumia historia zetu na masimulizi ya zamani kuwaenzi mashujaa mbalimbali? Afrika tuna mashujaa wengi sio hata wawili au kumi wapo wengi sana, kuanzia Sunni Ali Ber, Askia Mashuhuri, Shaka Zulu, Mtemi Bugando, Idris Alooma, Behanzin Bowelle, Mfalme Menelik wa Pili, Mansa Musa, Mtemi Makongoro, Samory Toure na kadhalika. Je tumeruhusu filamu ifasiri maandishi na masimulizi na kuyaweka kuwa filamu kwa ajili ya kizazi kinachokuja?

Ulaya wao wapo mubashara kila siku kutangaza miji na utamaduni wao, tazama filamu kama Call me by your name, To catch a thief, Porco Rosso pamoja na Sleep Furiously, utaona namna ya ajabu na jinsi walivyotangaza utamaduni wao kwa dunia.

Namkumbuka sana muongozaji Musa Banzi, muongozaji ambaye alitupatia utamu wa filamu kama vile, Tabana, Odama, Nsyuka sehemu ya kwanza na pili, pamoja na fungu la kukosa.

Ukitazama filamu ya Odama alituonesha asili ya mtanzania kwa upana sana kuanzia mavazi, matumizi ya majina ya asilia, Mfalme Garagarauka Adumba, Mtabiri Tambitambi, Msisi wa Msisiri, Kantala na kadhalika, Hapo ndipo tulikuwa na chetu sasa kama Waafrika na Watanzania.

Mpaka leo tumeshindwa kutengeneza filamu kuhusu maisha ya dokoa, chifu mangugo wa msovero kweli tumekosa filamu kuhusu maisha ya Mtemi Mirambo, Tumekosa filamu za kuelezea ushujaa wa Kinjekitile Ng’wale na vita ya Maji Maji, tumeshindwa kabsa kutengeneza filamu kuhusu Tipu Tipu au hatuna muda wa kuumiza vichwa vyetu kuwafundisha watoto wetu na kikazi kijacho kuhusu historia ya kweli kuhusu mwafrika na mtanzania.
IMG_1276.jpg


Leo ni rahisi sana kwa mtoto wa kitanzania kufahamu maisha ya familia ya Kardashians wanafahamu wanakula nini, pamoja na majina ya wanafamilia wote. Ni rahisi kwa mtoto wa kisukuma kujua kuimba vizuri sana wimbo kutoka Pingfong wa Baby Shark ila sio kuimba nyimbo za asili za kabila la kisukuma. Afrika kusini wametuacha mbali sana kwani wao wameshatengeneza filamu na tamthilia kuhusu maisha ya Shujaa Shaka Zulu.


Shukrani nyingi ziende kwa mpambanaji, Seko Shamte ambaye ni muongozaji mwenye kipaji kikubwa sana cha fikra na kipawa fahamivu, ni Seko ndiye aliyetupatia Tanzania zawadi ya filamu ya Mkwawa.


Munyigumba Mwamuyinga shujaa ambaye amelala pale Mlambalasi Iringa, je waongozaji wengine hamuoni kama huu ni ukumbusho wa kuamka kutoka usingizi, na kuanza kuruhusu historia ienziwe kizazi mpaka kizazi.


Nina imani kuwa kwa kiwango cha utandawazi na teknolojia, filamu inaweza kutoka leo na kuendelea kuishi mpaka miaka 100, Nitakupa mfano, wengi tunafurahi na kucheka sana tukitazama filamu za Chaplin kama vile Making a Living, Mabel's Strange Predicament pamoja na Caught in the Rain lakini kaa ukifahamu kuwa filamu hizi zilitoka mwaka 1914 yaani mpaka sasa zina miaka zaidi ya mia moja.


Kwa lugha nyepesi zina miaka 109 toka zimetolewa, filamu ya City Lights ambayo inatuburudisha kila uchao ilitoka mwaka 1928. Tunakumbuka ile filamu ya papa mla watu ya Jaws je unafahamu kuwa ilitoka mwaka 1975 na mpaka sasa ina miaka 48 na bado ina ubora ule ule.

Kuna kipindi soko la filamu la Tanzania lilitoa filamu mbili ambazo bora sana, filamu za White Maasai ya mwaka 2005 pamoja na White Shadow ya mwaka 2013, na kwa mujibu mtandao wa IMDB wao wanaonesha kuwa hizi ni moja ya filamu bora sana za kitanzania kuonesha uhalisia wa jamii.


Mpaka sasa suala la mazingira bado ni changamoto kwa Tanzania, kwanini tusitumie filamu na tamthilia kuiwajibisha serikali na mamlaka husika kuhusu kusimamia mazingira, tokea tumepata uhuru mpaka leo umasikini bado umetamalaki kwa fujo kama simba mwenye njaa, na filamu haina mchango wowote, basi atokee muongozaji mmoja aende kufanya makala kuhusu hilo na kuonesha tatizo hilo kwa ukaribu.

Sidhani kama ni sahihi kwa kile ambacho kinaendelea kwenye tasnia ya filamu Tanzania, maisha ya mwanadamu ya kila siku sio kuhusu mahaba na usaliti, kuna vitu vingi ambavyo vinahitaji kuoneshwa ili watu wapate kuwajibika na kuvifanyia kazi. Tasnia ya filamu hubeba dhamira nyingi sana za sanaa, na kama moja ya utanzu mpana sana katika sanaa ni ajabu kukutana na filamu zenye ujumbe ule ule, tunaacha kuonesha uhalisia tunakazana kuonesha nadharia tu. Filamu ni darasa kubwa sana kwa jamii, inaweza kutumika kuelimisha au kupotosha, kufariji au kuumiza pia kupongeza au kukebehi.



Naiomba serikali kupitia wizara husika pamoja na wadau kwa kushirikiana na viongozi wa BASATA na wasanii kukaa chini na kutafakari kwa kina, wakusanye maoni waone ni dhamira zipi zinapaswa kuoneshwa kwa Watanzania.
Nakupenda sana Tanzania mpenzi wangu.
 

Attachments

  • IMG_1269.jpg
    IMG_1269.jpg
    25.7 KB · Views: 6
  • IMG_1277.jpg
    IMG_1277.jpg
    66.8 KB · Views: 4
  • IMG_1278.jpg
    IMG_1278.jpg
    31.4 KB · Views: 4
  • IMG_1279.jpg
    IMG_1279.jpg
    16.8 KB · Views: 4
  • IMG_1280.jpg
    IMG_1280.jpg
    33.9 KB · Views: 4
  • IMG_1281.jpg
    IMG_1281.jpg
    63.4 KB · Views: 4
  • IMG_1282.jpg
    IMG_1282.jpg
    38.7 KB · Views: 5
Upvote 0
Back
Top Bottom