Taratibu za Upigaji Kura
Wajibu wa Vyama vya Siasa katika kupanga Vituo vya Kupigia Kura na Uteuzi wa Wasimamizi wa Vituo
- Kupanga Vituo
Msimamizi wa Uchaguzi atavipatia Vyama vya Siasa orodha ya vituo anavyotarajia kuvitumia kwa ajili ya upigaji kura. Vyama vya Siasa vina haki ya kutoa maoni kuhusu mahali vilipo vituo hivyo.
- Uteuzi wa Wasimamizi wa Vituo
Msimamizi wa Uchaguzi atatangaza kwenye ubao wa matangazo mahali pa wazi nje ya ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi orodha ya majina ya watu anaotarajia kuwateua kama Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura. Vyama vya Siasa vina haki ya kuota pingamizi kama wanazo dhidi ya jina lolote lililomo katika orodha hiyo kaika siku nne toka Msimamizi wa Uchaguzi alipotangaza orodha hiyo.
Msimamizi wa Uchaguzi atakuwa na uamuzi wa mwisho katika kuteua Wasimamizi wa vituo.
Haki ya kuteua Mawakala
Kila Chama cha Siasa, baada ya kushauriana na Wagombea, kina haki ya kuteua Wakala mmoja kwa kila kutuo cha kupigia kura. Ni vema Mawakala wapangwe vituo vya upigaji kura ndani ya kata wanakoishi ili waweze kuangalia vizuri maslahi ya wagombea. Majina ya Mawakala, anuani zao na vituo walivyopangiwa yawasilishwe kwa Msimamizi wa Uchaguzi siku saba kabla ya siku ya kupiga kura.
Vyama au Wagombea kushuhudia ugawaji wa vifaa
- Vifaa vinavyotumika siku ya kupiga kura vitakabidhiwa kwa Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura mbele ya Mgombea au Wawakilishi wao.
- Chama kitapatiwa orodha kamili ya vifaa muhimu vitakavyotolewa kwa kila kituo vikiwemo, namba za masanduku ya kura, idadi ya namba za karatasi za kura.
Mafunzo kwa Mawakala
Vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi vitawajibika kutoa mafunzo kwa Mawakala kwa gharama zao.
Wajibu wa Mawakala
Mawakala wa Upigaji kura wana wajibu ufuatao:-
- Kuhakikisha kwamba anayepiga kura ndiye aliyejiandikisha
- Kushirikiana na Msimamizi wa kituo cha kupigia kura katika kuhakikisha kwamba upigaji kura unafanywa kwa kuzingatia sheria
- Kulinda maslahi ya mgombea anayemwakilisha kituoni.
Hata hivyo kutokuwepo kwa wakala wa upigaji au kuhesabu kura kituoni hakutazuia wala kubatilisha shughuli yoyote itakaoendeshwa kwa mujibu wa Sheria.
Mawakala waliojiandikisha kupiga kura, ambao watapangwa katika vituo ambavyo hawakujiandikisha kupiga kura, wanaweza kumjulisha Msimamizi wa Uchaguzi mapema kabla ya siku ya uchaguzi ili awapatie shahada za utumishi.
Mawakala wanawajibika kujaza fomu zote ambazo zimewekwa kisheria ili kuonyesha kuridhika au kutoridhika na mwenendo wa uchaguzi. Fomu hizo ni namba 14 na 16.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mawakala wa upigaji au kuhesabu kura watakaosimamia vituo vya mwisho ambako misafara ya kukusanya masanduku na vifaa vingine itaanzia, ndio pia watakaosindikiza na watakaoshuhudia makabidhiano ya vifaa hivyo kwenye kituo cha kujumlisha kura.
Kiapo cha Kutunza Siri
Kwa mujibu wa kifungu cha 93(1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 1/85 na kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Madiwani namba 4/79 Mawakala wa upigaji kura wanatakiwa kula kiapo cha kutunza siri mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi. Kila Chama au Mgombea ahakikishe kuwa Mawakala wake wanakula kiapo kabla ya siku ya uchaguzi.
Mawakala wanaruhusiwa kuwepo katika vituo vya kupiga kura walivyopangiwa tangu mwanzo wa hatua za upigaji kura hadi matokeo ya uchaguzi katika kituo hicho yatakapotangazwa ili waweze kutekeleza majukumu yaliyotajwa. Hata hivyo, kisheria shughuli za upigaji kura zitaendelea hata kama Mawakala hawatakuwepo. Mawakala hao watagharamiwa na vyama vyao.
Wanaoruhusiwa kuwepo katika kituo cha kupigia kura
- Msimamizi wa Kituo
- Msimamizi Msaidizi wa Kituo
- Wakala
- Mpiga kura
- Mtu anayemsaidia mpiga kura asiyeweza kupiga kura mwenyewe kwa sababu ya ulemavu au asiyejua kusoma
- Mtazamaji wa Uchaguzi aliyeidhinishwa na Tume, kwa maandishi
- Mjumbe wa Tume
- Mkurugenzi wa Uchaguzi
- Afisa wa Tume
- Msimamizi wa Uchaguzi na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi
- Askari wa Polisi au Mlinzi wa Kituo
Kabla ya upigaji kura kuanza Mawakala au Wagombea waliopo watalazimika kujaza Fomu namba 14 kuonyesha kuridhika au kutokuridhika na maandalizi ya kituo cha upigaji kura.
Baada ya upigaji kura kukamilika Mawakala au Wagombea watajaza tena fomu namba 14 kuonyesha kuridhika au kutokuridhika kwao na mwenendo wa upigaji kura.
Shahada ya Utumishi / Maalumu
Watendaji na Mawakala ambao kutokana na majukumu yao katika uchaguzi hawataweza kupiga kura katika vituo walivyopangiwa watapatiwa Shahada za Utumishi ili waweze kupiga kura katika vituo watakapofanyia kazi. Endapo mtendaji au Wakala anayehusika atapangiwa kufanya kazi kwenye kata nyinigne ambako hakujiandikisha hatapiga kura ya Diwani. Vilevile atakayepangiwa nje ya jimbo alipojiandikisha hatapiga kura ya Mbunge wala Diwani bali atapiga kura ya Rais tu.
Wagombea watapatiwa Shahada Maalumu ambazo zitawawezesha kupiga kura katika kituo chochote katika Kata kwa Mgombea Udiwani au Jimbo kwa Mgombea Ubunge. Endapo Mgombea Ubunge atahitaji kupiga kura katika kata ambako hakujiandikisha hatapiga kura ya Diwani.
Mambo yasiyoruhusiwa kufanyika siku ya kupiga kura
- Hairuhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote
- Kuvaa sare au alama za chama, kubeba au kubandika matangazo na kuimba nyimbo za vyama