Anyways huwa nawaza sana kumbe .. maisha ni nini..
"Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya" - Mhubiri 12:13-14
Maisha ni kama Mfalme mmoja ambaye aliamua kuwapa watu watu sehemu ya milki yao ili wawe na mamlaka kiasi fulani ya kujiamulia. Baada ya kuwapa mamlaka hayo akawa anawatembelea kila mara ili kufurahia kwa pamoja maana aliwapenda sana. Yule Mfalme alikuwa na moja ya watumwa wake ambaye alimchukia sana. Akijua hana cha kumfanya kwa sababu ya mamlaka yake, akanuia kuwaharibu watu wa milki yake ambao Mfalme aliwapenda na kuwajali sana.
Siku moja, mtumwa mwovu alimtembelea mke wa gavana wa lile jimbo liliopewa mamlaka lijiendeshe chini ya milki ya Mfalme. Akamshawishi kwa habari ya kumwasi Mfalme ili wao wawe wafalme. "Kuwa gavana haitoshi, kama unaweza kuwa mfalme". Kuna shida gani ukitangaza uhuru wako? Mke wa gavana aliyachukua yale maneno akamshawishi gavana kuwa watakuwa huru zaidi wakiwa nje ya Ufalme na kuwa ufalme huru. Gavana alikubaliana na mkewe wakatangaza mapinduzi na kujitangaza wafalme. Wakaungana na mtumishi mwovu kuupinga Ufalme. Pamoja na kuwapenda sana watu wa jimbo lile, kwa sababu ya uadilifu wake Mfalme akatangaza siku ya kwenda kulikomboa jimbo na adhabu ya kifo kwa waasi wote.
Mfalme akatangaza sheria mpya kuwa kwa muda aliompangia kila raia wa jimbo lile, atapaswa kurudishwa katika makao makuu ya Ufalme apate kuhukumiwa kulingana na matendo ya uasi wake. Gereza likaandaliwa lenye kila aina ya mateso, kwa ajili ya mtumishi mwovu na watu wa jimbo lile. Ikawa kila siku watu zaidi ya mia moja wa jimbo lile waliitwa kurudi kwa Mfalme, na kuhukumia kifo katika gereza lile. Walitamani sana na walijaribu sana wasiitike. Walitengeneza kila aina ya dawa, kuziba masikio yao wasisikie sauti ya Mfalme, maana akikuita hakuna namna utaacha kuitika. Lakini haya hayakufua dafu, watu walimiminika kila siku na walihukumiwa kila siku.
Mfalme alikuwa ametoa amri. Ya kuwa yeyote ambaye ataamua kuweka silaha chini, kuukana uasi wa jimbo lile na kupokea msamaha huo, ujapofika muda wake wa kuitwa, hataadhibiwa. Mfalme alikwishalipa adhabu kwa wote walio tayari kuweka chini silaha na kuukana uasi wao. Wengi wa watu wa jimbo hili walijisikia fahari kwamba wako huru. Hawakutaka kabisa kuingiliwa katika uasi wao. Walimchukia Mfalme na wengine waliamua mioyoni mwao kuwa hayupo. Wengine walimtukana na wengine waliendelea katika uais wao bila kelele.
Watu walioamua kupokea msamaha wa Mfalme walionekana vichaa, wasio na akili na wasaliti. Walichukiwa na baadhi ya maeneo ya jimbo lile waliuawa. Kuna wananchi wengine waliwaona ni wasaliti na wakapigwa marufuku kuishi au hata kuonekana maeneo yale. Wengine hawakujali, ilimradi wao wanaendelea katika uasi wao. Lakini kila siku mamia waliitwa na mamia walihukumiwa.
Siku hata siku, nyakati za Mfalme kurudi jimbo lile kulikomboa ulikaribia. Mtumishi mwovu alijua hilo naye akachochea uasi uwe mbaya siku hata siku. Hata hivyo wengi walikubali kuweka silaha chini na kuupokea msamaha. Wengi zaidi na zaidi waliukataa, wakaudhihaki na kutema mate.......
Summary ya maisha ni nini, ni hii hapo. Mwenye kusoma na afahamu
Mamndenyi