JamiiForums
JF Official Account
- Nov 9, 2006
- 6,229
- 5,285
TAARIFA KWA UMMA
Taarifa inatolewa kwa umma kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Kinondoni Kanda ya Dar es salaam kilikaa kikao chake tarehe 1 Disemba 2009 na kuazimia masuala mawili kama sehemu ya kuadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania: Mosi, Kutoa Tuzo ya Vijana ya Freeman Mbowe kuhusu Uhuru wa Kweli (Freeman Mbowe Real Freedom Youth Award 2009). Pili; kuitisha Kongamano la Vijana kuadhimisha siku ya Uhuru lenye mada/ujumbe: "Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.
Tuzo hiyo itatolewa kwa vijana watakaoandika hotuba ya kurasa kati ya mbili na kumi kuhusu mada/ujumbe "Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli" yenye mawazo ya vijana kuhusu hali ya Taifa miaka 48 baada ya uhuru na kupendekeza mwelekeo mbadala. Wanaoweza kushiriki katika shindano hilo ni vijana wa kitanzania wa kike na wa kiume wenye umri kati ya miaka 12 na 35 wanaoishi katika Halmashauri ya Kinondoni Mkoani Dar es salaam.
Washindi katika shindano hilo watapa fursa ya kualikwa kutoa hotuba zao kwenye Kongamano hilo la maadhimisho ya siku ya uhuru mbele ya viongozi, wanachama na wananchi kwa ujumla. Washindi katika shindano hilo atazawadiwa vyeti vilivyosainiwa na BAVICHA pamoja na John Mnyika; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda ya Dar es salaam. Pamoja na zawadi hizo; mshindi wa kwanza atapatiwa kifuta jasho cha shilingi laki moja wakati mshindi wa pili atapata shilingi elfu hamsini na washindi watakuwa katika uwiano wa kijinsia. Washiriki kumi bora wa shindano hilo watapatiwa Tshirt maalum za Vijana. Aidha uongozi wa vijana unaomba wapenda demokrasia na maendeleo ndani na nje ya Tanzania kuchangia tuzo hii.
Vijana wameanza kutangaziwa shindano hilo toka tarehe 1 Disemba 2009 na mwisho wa kutuma hotuba kwa wanaohitaji kushiriki ni tarehe 8 Disemba 2009 saa 6 mchana. Washiriki wanaweza kutuma hotuba zao kwa barua pepe kwenda kinondoni@chadema.or.tz ama chademakinondoni@gmail.com ama kuandika kwa mkono na kupeleka katika ofisi za CHADEMA mkoa zilizopo Kinondoni Kata ya Hananasifu Mtaa wa Kisutu. BAVICHA kinondoni inahimiza vijana wote wazalendo bila kujali itikadi kuandika mawazo yao ili kufikisha ujumbe kwa watanzania wote kuhusu mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.
Uamuzi wa kuchagua kuiita Tuzo jina la Freeman Mbowe umetokana na mchango wake katika harakati za mabadiliko ya kweli uhuru wa kweli. Freeman Mbowe alizaliwa miezi michache kabla ya Tanganyika kupata uhuru lakini wazazi wake hawakumbatiza mpaka tarehe 9 Disemba 1961 siku ya uhuru ndipo alipobatizwa na kupewa jina la Freeman; maana yake "Mtu Huru". Aidha amekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Vijana wa CHADEMA katikati ya kundi la vijana wa zamani (Wazee) walioamini katika nafasi ya vijana katika kuleta mabadiliko ndio maana chama kiliposajiliwa mwaka 1992 kilianza na kauli mbiu ya: Vijana; Taifa la Leo. Kwa sasa BAVICHA imeongezea kauli mbiu ya: Vijana; Nguvu ya Mabadiliko. Freeman Mbowe ni mmoja wa wafanyabiashara waliofanya vizuri kuanzia katika ujana wake na kuwa mfano katika harakati za kuleta uhuru wa kweli wa kiuchumi. Freeman Mbowe alipata kuwa mbunge wa Hai na mafanikio yake katika jimbo lake katika sekta ya afya, elimu nk yalikuwa ya mfano wa kuigwa. Pamoja na mambo mengine aligawa kompyuta mashuleni na kuanzisha mafunzo ya aina hiyo mpaka vijijini ili kutoa uhuru kwa vijana kuweza kuendana na karne ya sayansi ya Teknolojia. Pia alianzisha programu ya chakula na maziwa mashuleni ili kuwafanya wasome na kuwa mfano katika harakati za kuleta uhuru wa kweli wa kijamii. Freeman Mbowe amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa mwaka 2004; na katika kipindi chake cha uongozi amekuwa mstari wa mbele kuwapa kipaumbele vijana wasomi na hata vijana kwa kuwapa fursa za kuongoza nafasi za juu katika chama.
Zitto Kabwe, Halima Mdee, John Mnyika na wengineo na kuwa mfano katika harakati za kuleta uhuru wa kweli wa kisiasa. Freeman Mbowe ameendelea kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA akiongoza kipindi chake cha pili na cha mwisho kinachomalizika mwaka 2014. Freeman Mbowe amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha mabadiliko ya kweli kwa ajili ya kuleta uhuru wa kweli akiamini kwamba uhuru wa bendera pekee hautoshi kama taifa litaongozwa kwa ukoloni mamboleo unaopora rasilimali na kwamba uhuru wa kweli ni ule unaowezesha wananchi kuwa huru kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aidha BAVICHA Kinondoni inatambua na kupongeza kufanyika kwa Kongamano la Kumbukumbu ya Miaka 10 ya Kifo cha Nyerere lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere(MNF). Hivyo, pamoja na hotuba zitakazotolewa na washindi kuhusu mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli; Kongamano la Vijana Mkoa wa Kinondoni Kanda ya Dar es salaam katika kuadhimisha miaka 48 ya uhuru litatafakari namna ya kuhamasisha utekelezaji maazimio ya Kongamano la Kumbukumbu ya Nyerere lililomalizika hususani yale yanayolenga kulinusuru Taifa.
Maazimio hayo saba ni pamoja na: Mosi; Kufanyika maamuzi magumu na hatua za kijasiri kwa lengo la kurejesha maadili aliyoacha Nyerere. Maadili hayo ni pamoja na kuheshimu na kuzingatia katiba, utawala wa sheria kwa mujibu wa katiba, na viapo vya uongozi/utumishi. Pili; kutambua kwamba cheo ni dhamana na kamwe kisitumike kwa faida binafsi. Tatu; Viongozi kusimamia matumizi bora ya rasilimali za Taifa. Nne; Wananchi kutambua kwamba wanajukumu la kwanza kuhakikisha wanapata viongozi wazuri. Tano; Viongozi nao kutambua na kuheshimu maamuzi ya wananchi waliowapa madaraka. Sita; viongozi wakishirikiana na wananchi wachukie rushwa na ufisadi na wapinge kwa kwa kauli na vitendo. Saba; Viongozi wajenge utamaduni wa kuwajibika pale wananchi wanapowahusisha na kashfa na makosa ya kimaadili ya uongozi.
Imetolewa na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Kinondoni Kanda ya Dar es Salaam, Hemed Msabaha; kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia 0712222214 au 0653329668
Disemba 5, 2009