Fursa za Uwekezaji nchini Tanzania kwa wajasiriamali

Fursa za Uwekezaji nchini Tanzania kwa wajasiriamali

figganigga

JF-Expert Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
25,724
Reaction score
55,906
Zifuatazo ni baadhi ya fursa zilizopo Tanzania ambazo wajasiliamali wanaweza kuzitumia kupanua biashara zao.

Uzalishaji miwa
Kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa kipato miongoni mwa watanzania, ukuaji wa soko la sukari Tanzania unakadiriwa kufikia asilimia 6% kwa mwaka. Upungufu wa usambazaji wa sukari kwa sasa unakadiriwa kufika tani 300,000.

Takwimu hizi zinategemewa kupanda kwa kasi kwa sababu wazalishaji wa sukari waliopo hawajaongeza uwezo wao wa kuzalisha kulingana na ukuaji wa mahitaji. Mbali na upungufu huo ndani ya Tanzania, upungufu wa sukari kwa soko la Afrika Mashariki unakadiriwa kufikia tani 400,000 kwa mwaka. Kwa kuzingatia hayo uzalishaji wa sukari ni fursa ambayo wajasiriamali kwa ujumla wanatakiwa kuitumia ili kujiongezea kipato. Mikoa kama Kagera na Morogoro ndio mikoa ambayo kilimo cha miwa kinashamiri vizuri.

Ukulima wa mpunga
Kwa kuzingatia ukuaji wa pato la taifa ni fursa nyingine ya uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania. Wajasiriamali wanashauriwa kutumia pengo lililopo la usambazaji wa mchele ili kuhudumia mahitaji ya soko linalokua kwa kasi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kutokana ukuaji wa ongezeko la watu maeneo ya mjini nchini Tanzania unaokadiriwa kufikia asilimia 4.7%, inasadikiwa kuwa watu wengi wa daraja la kati kimaisha nchini Tanzania wanapendelea mchele kama chakula kikuu kulinganisha na vyakula vingine, kwa hiyo hali hii inaongeza tija kwa wajasiriamali watakaojishughulisha na ukulima wa mpunga kuwa na uhakika wa soko linalokua kila mwaka.

Vile vile wajasiriamali wa Tanzania wanayo fursa nyingine ya soko la Afrika Mashariki, Soko la muungano wa nchi za kusini mwa Afrika (SADC), na COMESA, ambako mahitaji ya mchele yanaongezeka kila baada ya muda. Mikoa ambayo kilimo cha mchele kinakubali nchini Tanzania ni kama Morogoro na Mbeya.

Ufugaji
Fursa nyingine kwa wajasiriamali wa Tanzania ni katika sekta ya ufugaji. Katika sekta hii kumekuwepo na uongezekaji wa mahitaji ya bidhaa za ufugaji, hususani nyama. Hii inatokana na ongezeko la watu, ukuaji wa miji pamoja na ukuaji wa vipato baina ya watanzania inaongeza mahitaji ya nyama. Kwa makadirio ya matumizi ya nyama kwa kilogramu 12 kwa mwaka kwa mtu mmoja, soko lanyama kwa Tanzania linakadiriwa kufikia mara tatu ya sasa hivi ifikapo mwaka 20130. Mbali ya soko la ndani la nyama, Tanzania pia inasafirisha nyama kwenda nchi jirani na nchi za Mashariki ya Kati.

Kilimo cha Bustani
Hii ni fursa nyingine kwa wajasiriamali nchini kupitia kilimo cha mboga mboga, matunda, maua, viungo na mbegu kwa ajili ya kuuza nchini, katika ukanda wa Africa Mashariki na kimataifa. Kuna upatikanaji usio wa uhakika wa mazao yanayokidhi ubora na viwango kiasi cha kuifanya nchi iagize matunda, mboga mboga na viungo mbali mbali kama vile nyanya, vitunguu, vitunguu swaumu, matufaha, zabibu, mapeasi na matunda madogo aina ya strawberry.
Kwa bidhaa za matunda zinazokidhi viwango, mahitaji ni makubwa sana kwa soko la ndani na hata kwa ajili ya kusafirisha, na hata kiasi cha matunda kianchosafirishwa kutoka Tanzania kimeongezeka maradufu.

Uvuvi
Tanzania ni nchi ya kumi kwenye shughuli za mazao ya uvuvi. Fursa kubwa zinazopatikana katika sekta ya uvuvi nchini Tanzania zipo katika maeneo kama: uvuvi, usindikaji wa samaki, uongezaji wa thamani ya samaki na bidhaa nyingine za samaki; ujenzi wa boti, ujenzi wa bandari za uvuvi, ujenzi wa bandari kavu, utalii unaohusisha utunzanji wa mazingira, utengenezaji wa vifaa vya uvuvi. Eneo jingine muhimu la uwekezaji kwa wajasiriamali kwenye upande wa uvuvi ni ufugaji wa samaki aina ya kamba, ufugaji wa samaki kaa, ufugaji utamaduni lulu, ufugaji wa finfish, ukulima wa mwani, na uzalishaji wa chakula cha samaki.

Misitu
Serikali inafanya juhudi kubwa katika kukuza sekta binafsi na ushiriki wa jamii katika uendeshaji wa mashamba ya serikali. Serikali ianajaribu kuzishawishi kampuni na watu mmoja mmoja kuwekeza katika ukulima wa miti ya magogo, kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi. Uanzishwaji wa viwanda unahitajika ili kutumia vizuri mazao ya misitu kuzalisha mbao, aina mbalimbali za mbao, samani na nguzo.

Ufugaji Nyuki
Fursa zipo kwa ajili ya viwanda na usambazaji wa vifaa vya kutumika katika ufugaji nyuki, kwa mfano, mizinga ya nyuki, vifaa vya kinga, na vifaa vya kurina asali. Upande mwingine kwa uwekezaji katika ufugaji nyuki ni kutengeneza viwanda vya mishumaa, rangi za kung’arishia viatu, rangi kung’arishia mbao, vilainishi na bidhaa za famasia. Pia viwanda vya vifungashio vya asali na viwanda vinginevyo vinavyotumia asali kutengenzea pombe, mvinyo, na waokaji vyakula pia wanaweza kutumia fursa hii.

Utalii
Zaidi ya asilimia 44 ya ardhi ya Tanzania ina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori na hifadhi za taifa. Kuna hifadhi za taifa 16, maeneo 29 yaliyotengwa kwa wanyamapori, maeneo 40 chini ya udhibiti wa uhifadhi na hifadhi ya maeneo katika mwambao wa bahari. Uwekezaji katika utalii waweza kuwa katika njia ya malazi (mahoteli, kambi za kitalii), huduma za utalii na ufanyaji shughuli zinazoendana na utalii na uwakala katika utalii.

Uzalishaji
Sekta ya uzalishaji iko katika hatua changa ikiwa na maeneo machache yanayotumika ambapo kwa kiasi kikubwa inatawaliwa na mazao ya kilimo yanayosafirishwa yakiwa hayajachakatwa. Fursa zilizopo katika sekta hii ni kupitia uzalishaji kwa ajili ya watumiaji wa kawaida bidhaa kama vyakula, vinywaji, nguo, tumbaku, mbao, mazao ya mbao, mazao ya mipira, chuma, na bidhaa za chuma.

Kusindika Matunda/Mboga
Tanzania ina utajiri mkubwa wa aina nyingi za matunda na mbogamboga. Ni chini ya asilimia 10 tu ya matunda na mboga zote zinazozalishwa zinasindikwa. Maeneo yenye ardhi inayokubali kilimo cha matunda ni mikoa kama ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza na Kagera.

Nguo na mavazi
Kuna fursa za kuanzisha viwanda vya nguo jumuishi pamoja na viwanda vya kusindika na kuchakata pamba. Fursa hii nchini Tanzania ipo kulingana na ukweli kwamba kuna uzalishaji mkubwa wa pamba unaopelekea zao hili kukosa soko muda mwingine. Hii ikitiliwa maanani na wajasiriamali aidha mmoja au vikundi inaweza kuleta tija katika kukuza uchumi wa wajasiriamali.

Ngozi
Sekta ya ngozi inatoa fursa kubwa ya kuwekeza katika uzalishaji. Tanzania huzalisha takribani vipande milioni 2.6 vya ngozi ghafi kwa mwaka, wakati ambapo inayochakatwa nchini ni asilimia 10 na sehemu kubwa inasafirishwa nje ya nchi kama mali ghafi. Fursa katika eneo hili zipo ili kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa katika sekta ya ngozi na mazao yake kama viatu, mikoba, mikanda, na bidhaa nyingine za ngozi.

Chanzo: FURSA ZA UWEKEZAJI | MSMEs Information Portal
 
Labda hizo shughuli zifanywe kama machinga mkuu
 
ulivyozitaja mkuu utafikri ni vyepesi kweri kuvitumia... but ?.
 
Back
Top Bottom