Futari nyumbani kwa marehemu Hamza Aziz siku aliyowaeleza wageni wake kisa chake akiwa Inspector Geneal Of Police ( IGP) alipokataa kutii amri kutoka

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
FUTARI NYUMBANI KWA MAREHEMU HAMZA AZIZ SIKU ALIYOWAELEZA WAGENI WAKE KISA CHAKE AKIWA INSPECTOR GENEAL OF POLICE ( IGP) ALIPOKATAA KUTII AMRI KUTOKA JUU



Kuna rafiki zangu watu maarufu katika duru za Kiislam waliniomba niwapeleke kwa Hamza Aziz na ilikuwa katikati ya miaka ya 2000.

Nilimpigia simu na akatukaribisha nyumbani kwake nyumba ambayo kwangu mimi sikuwa mgeni.

Siku hii kwa kuwa nilikuwa nimekwenda na wageni Hamza Aziz hakutukaribisha kwenye kibanda chake cha makuti cha kupunga upepo, kibanda kinachoangalia Bahari ya Hindi.

Hiki kibanda kilikuwa Majlis yetu sisi wawili.

Siku hiyo tulikuwa katika ukumbi wake ndani ya nyumba yake nzuri ya gorofa moja Msasani unaelekea Kawe.

Ulikuwa Mfungo wa Ramadhani.

Baada ya wale rafiki zangu kumaliza kile kilichowaleta tukawa tunafanya mazungumzo ya hili na lile.

Ghafla Hamza Aziz akaniuliza, ‘’Mohamed nimekualikeni futari?’’

Mimi nikamjibu kuwa hakutualika futari miadi ilikuwa ni mimi kuwaleta kwake wale rafiki zangu kwa lile walilotaka kuzungumzanae.

Pale pale Hamza Aziz akasema, ‘’Basi nakualikeni futari leo msiondoke.’’

Kadri tulivyojaribu kumkatalia hakukubali akasema mshafika nyumbani kwangu leo tufuturu pamoja.

Basi ikawa sasa ule wasiwasi wa kuondoka kwenda majumbani kwetu kuwahi kufuturu umeondoka tukawa sasa tumekaa tumetulia tukifaidi upepo mwanana wa Bahari ya Hindi uliokuwa ukiingia kupitia madirisha yale makubwa na huku tukiiangalia bahari yenyewe iliyokuwa na rangi ya bluu ya kupendeza.



Sasa mimi nakijua kisa cha Hamza Aziz ambacho alinihadithia mwenyewe alivyokataa kutii amri kutoka juu ya kumkamata Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Ameir akituhumiwa kuwa alikuwa katika mipango ya kupindua serikali ya Tanzania.

Hamza Aziz alimkatalia Waziri wa Mambo ya Ndani Said Ali Maswanya aliyemfikishia amri ile kuwa hawezi kamwe kumkamata Sheikh Hassan bin Ameir kwa sababu za uongo.

Basi nikamchokoza Hamza Aziz nkamwambia, ‘’Baba hebu tueleze kile kisa cha Sheikh Hassan bin Ameir.’’

Mimi nilifanya hivyo kwa kutaka na wale ndugu zangu wasikie kisa kile kutoka kwenye mdomo wa farasi mwenyewe.

Waingereza wanasema, ‘’From the horse’s mouth.’’

Nilitaka na wao wawe shahidi wa historia ile muhimu sana katika historia ya Tanganyika baada ya uhuru wake mwaka wa 1961.

Hamza Aziz aliwageukia wageni wake akasema huku akicheka, ‘’Huyu Mohamed ni mchokozi sana.’’

Hamza Aziz alianza kueleza kisa kile akianza na mgogoro uliokuwapo wakati ule wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) serikali ikitaka ivunjwe ili ipatikane nafasi ya kuuunda BAKWATA.

Ukumbi ghafla ulikuwa kimya na sauti iliyokuwa ikisikika ilikuwa ya Hamza Aziz akieleza mkasa ule na upepo uliokuwa ukivuma na kutikisa matawi ya miti iliyokuwa nje jirani na nyumba yake.

Hamza Aziz alimaliza kwa kusema maneno haya: ‘’Siku zote namshukuru Allah kwa kuniongoza kufanya uamuzi ule kwani laiti mimi ningelitoa amri ya polisi kumkamata Sheikh Hassan bin Ameir leo ningeliwatazamaje Waislam?’’

Maghrib iliingia tukapiga adhana, tukafungua kwa tende na vinono vilivyokuwapo tukaswali ukumbini kwake, tukafuturu pamoja kisha tukaagana.

Picha hapo juu Hamza Aziz akiwa askari kijana na picha nyingine ni Sheikh Hassan bin Ameir na viongozi wakuu wa serikali ya Tanzania..
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…