Melubo Letema
JF-Expert Member
- Apr 1, 2020
- 416
- 414
KATIKA kuadhimisha Siku ya Afrika 'Africa Day', Tanzania itaadhimisha kwa tukio hilo kwa mbio zitakazokwenda kwa jina la 'Africa Day Marathon' zitakazopambwa na wanariadha nyota wa zamani na wa sasa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wakili Jackson Ndaweka, aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kuamua kuuchagua mchezo wa Riadha katika maadhimisho hayo.
Alisema mbio hizo za Km. 15 na Km. 5 Fun Run, zitapambwa na nguli wa Radha Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na Kanali mstaafu Juma Ikangaa.
Mbio hizo zitarindima Mei 18 zikianzia eneo la Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ikiwa ni siku saba kabla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 61 tangu kuanzishwa Umoja wa Afrika, Mei 25, 1963 wakati huo ukijulikana kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika.
Mbali na nguli hao, pia watakuwepo wanariadha watakaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki Paris 2024, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu.
Ndaweka, alitoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na nje, kujitokeza kwa wingi kujisajili, kuungana na nguli na nyota hao kushiriki maadhimisho hayo huku wakijenga afya zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Ali Bujiku, alisema lengo la mbio hizo ni kusherehekea mafanikio ya miaka 61 ya nchi za Afrika.
Balozi Bujiku, alisema mbio hizo pia zitashirikisha viongozi na mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini.
Mbio hizo zimeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Balozi za nchi za Kiafrika nchini na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Washiriki katika mbio hizo watajipatia medali, fulana na kibegi, huku pia kukiwa na zawadi ya fedha taslimu kwa washindi wa kwanza hadi 10 kwenye Km. 15.