Geuza Kibao: Tumia sababu zako za kutokuwekeza kupata msukumo wa kuwekeza zaidi

Geuza Kibao: Tumia sababu zako za kutokuwekeza kupata msukumo wa kuwekeza zaidi

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Uwekezaji ndiyo nyenzo kuu ya mtu kujenga utajiri na uhuru wa kifedha. Ni nyenzo ambayo iko wazi kwa watu wote kuweza kutumia bila ya kuwepo kwa ubaguzi wowote. Wenye kipato kikubwa wanaweza kutumia njia hii, kadhalika wenye kipato kidogo.

Licha ya umuhimu huo mkubwa wa uwekezaji kwenye kujenga utajiri na uhuru wa kifedha, bado watu wengi wamekuwa hawafanyi uwekezaji. Wapo ambao hawawekezi kabisa na wapo ambao wanawekeza ila siyo kwa msimamo.

Wote ambao hawawekezi wanakosa fursa nzuri ya kutumia fedha zao kuzalisha fedha zaidi kitu kinachowakwamisha kujenga utajiri na uhuru wa kifedha.

Kwa kuwa hakuna binadamu anayefanya kitu bila kuwa na sababu, hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wasiowekeza. Huwa wanakuwa na sababu ambazo ni sahihi kabisa kwao, japo kiuhalisia zinaweza zisiwe sahihi.

Kubishana na watu kwamba sababu zao siyo sahihi haijawahi kuleta muafaka mzuri. Na hata mtu kubishana na yeye mwenyewe kwamba sababu zake siyo sahihi haimsaidii.

WhatsApp-Image-2024-08-26-at-18.39.59_ae7ad26f-723x1024.jpg

Njia pekee ambayo mtu anaweza kutumia sababu zake kwa manufaa ni kuzikubali sababu hizo, kisha kuzitumia kama sababu ya kufanya.

Yaani mtu anakuwa na sababu zinazomzuia kufanya kitu, anazikubali sababu hizo, halafu anazitumia kama msukumo wa kufanya kitu hicho.

Ili kufanya uwekezaji kwa msimamo bila kuacha, mtu unapaswa kujua sababu zinazokuzuia kufanya hivyo, kisha kuzitumia kama msukumo wa wewe kuwekeza.

Karibu ujifunze jinsi ya kufanya hilo kwenye somo hili.

SABABU ZINAZOWAZUIA WENGI KUWEKEZA NA JINSI YA KUZITUMIA KUWEKEZA ZAIDI

Kama tulivyoona hapo juu, kama huwekezi kabisa au kama huwekezi kwa msimamo, kuna sababu zinakuzuia. Hapa tunakwenda kuziangalia sababu hizo na jinsi ya kuzitumia kama msukumo wa kuwekeza zaidi.

1. NIMECHELEWA KUANZA KUWEKEZA

Wengi huona wamechelewa kuanza kuwekeza na hivyo kukata tamaa juu ya uwekezaji.

Hatua; Unapojiona umechelewa, jiambie hutaendelea kusubiri tena, badala yake utawekeza kwa ukubwa ili kufidia muda uliochelewa. Kila mara jikumbushe uko nyuma ya muda ili uwekeze zaidi.

2. KIPATO HAKITOSHELEZI KUWEKEZA

Hii ndiyo sababu ya wengi, kwamba kipato walichonacho ni kidogo na hivyo hawawezi kutoa fungu la kuwekeza.

Hatua; Pale kipato chako kinapokuwa hakitoshelezi ndiyo unalazimika kufanya uwekezaji ili utengeneze fursa za kujiongezea kipato. Kila unapoona kipato chako ni kidogo, jiambie napaswa kuwekeza zaidi ili nitoke kwenye hali hii.

3. FAIDA NI NDOGO KWENYE UWEKEZAJI

Faida ya uwekezaji huwa ni ndogo kuliko mtu akizalisha fedha hiyo moja kwa moja. Lakini mtu anapowekeza hasumbuki kwa kitu chochote kile, anapokea faida tu. Na kwa muda mrefu, faida hiyo inajikusanya na kuwa kubwa.

Hatua; Unapoona faida ni ndogo, pata msukumo wa kuwekeza kwa muda mrefu zaidi bila kutoa ili faida ijizalishe na kujikusanya kuwa kubwa zaidi.

4. MUDA BADO WA KUANZA UWEKEZAJI

Kwa ambao wana umri mdogo huwa wanaona bado wana muda mrefu hivyo hawana haja ya kuwekeza mapema.

Hatua; Unapojiambia bado una muda, hiyo ndiyo sababu ya kuwekeza sasa kwa sababu kwa uwekezaji mdogo kabisa utaweza kuzalisha thamani kubwa kwa muda mrefu.

5. SIHITAJI KUFANYA UWEKEZAJI

Kwa watu ambao wana kipato kikubwa cha moja kwa moja, iwe ni kutoka kwenye ajira au biashara, huwa wanabweteka na kuona hawahitaji kuwekeza. Huona kipato hicho watakuwa nacho milele.

Hatua; Pale unapoona huhitaji kuwekeza kwa sababu una kipato kikubwa, jikumbushe ambao walikuwa na kipato kama hicho na baadaye wakakikosa kitu kilichowashusha chini. Wewe wekeza kwa ukubwa kipindi una kipato kikubwa ili hata kikiondoka unufaike na uwekezaji uliofanya.

SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.

6. SIJUI NIWEKEZE WAPI

Elimu ya uwekezaji haijatolewa vya kutosha na wale wanaotuzunguka hawana uelewa kuhusu uwekezaji. Hivyo wengi wanajikuta wakiwa hawajui wapi wawekeze na hivyo kutokuwekeza kabisa.

Hatua; Unapoona hujui wapi pa kuwekeza, tumia hiyo kama sababu ya kujifunza na kufanya uwekezaji. Anza kwa kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja ya uwekezaji ambayo haitaki uwe na ujuzi mkubwa sana.

7. SINA MUDA WA KUFUATILIA UWEKEZAJI

Watu wametingwa na kazi au biashara zao kiasi kwamba hawana muda kabisa kwa ajili ya mambo mengine. Hilo linawafanya wakose nafasi ya kufanya na kufuatilia uwekezaji.

Hatua; Unapokwama kuwekeza kwa sababu ya kukosa muda, tumia hiyo kama sababu ya kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kwa sababu haikutaki ufuatilie chochote. Unaweza kuwekeza ukiwa popote na ndani ya muda mfupi sana.

8. NITAKUFA NA KUACHA UWEKEZAJI

Faida kubwa ya uwekezaji huwa inaonekana muda mrefu ujao, miaka 10, 20, 30 na kuendelea. Wengi wakipiga hesabu zao wanajiona wakiwa wamekufa kwenye umri huo na kuona wakiwekeza wataacha uwekezaji huo.

Hatua; Unapokwama kuwekeza kwa sababu ya kuona utakufa, tumia huo kama msukumo wa kuwekeza. Jiambie ni heri ufe ukiwa na uwekezaji, kuliko uishi miaka mingi ukiwa huna uwekezaji. Kwa zama hizi, watu wengi wanaishi maisha marefu, hivyo wekeza, utaishi kuliko unavyotarajia.

9. UWEKEZAJI NI HATARI

Kila aina ya uwekezaji huwa ina hatari zake. Hakuna uwekezaji wowote ambao una usalama na uhakika wa asilimia 100. Kuna watu kwa kufikiria hizo hatari hukwama kuwekeza.

Hatua; Unapozuia na hatari kuwekeza, tumia hiyo kama kichocheo kwa sababu kila kitu kwenye maisha kina hatari. Na pia chagua uwekezaji ambao una hatari kidogo.

10. NAAMINI ZAIDI KWENYE ARDHI NA MALI

Watu ambao wanaamini kwenye uwekezaji wa vitu vinavyoonekana, huwa ni wagumu sana kuwashawishi kuwekeza kwenye masoko ya mitaji.

Hatua; Kama unakwama kuwekeza kwenye masoko ya mitaji kwa sababu unawekeza zaidi kwenye mali, jikumbushe pale utakapohitaji ukwasi kwa haraka uwekezaji wa mali unakuwa kikwazo. Fanya sehemu ya uwekezaji wako kuwa masoko ya mitaji ili upate ukwasi kwa urahisi.

Hatupaswi kukubali sababu yoyote ile kutuzuia kufanya uwekezaji kwenye maisha yetu. Kwani hizo hizo sababu za kutokuwekeza, ndiyo sababu za kuwekeza. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uwekeze kwa msimamo bila kuacha.

Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2024 ambapo utakwenda kujifunza na kuweka mpango huu kwa vitendo kisha kusimamiwa kwenye kuutekeleza kwa msimamo bila kuacha. Tuma sasa ujumbe wenye maneno SEMINA 2024 kwenda namba 0752 977 175 upate nafasi ya kushiriki semina.

Kitabu kipya cha USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI kina nguzo saba muhimu kwa kila mtu kujijengea ili kuwa imara kifedha. Hiki ni kitabu muhimu kwa kila aliye makini na fedha zake kukisoma. Wasiliana sasa na namba 0752 977 175 kupata nakala yako ya kitabu.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.


View: https://youtu.be/YEzvU8yqY6s

MJADALA WA SOMO

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Ni sababu zipi kuu zilikuwa zinakuzuia kuwekeza?

2. Unazitumiaje sababu hizo sasa kama msukumo wa kuwekeza zaidi?

3. Pale unapopata vishawishi vya ndani au nje kutokufanya uwekezaji kama ulivyopanga, huwa unavivukaje?

4. Pale unapopata vishawishi vya ndani au nje kutoa uwekezaji tofauti na ulivyopanga, huwa unavivukaje?

5. Mtu akikuambia wewe ni mjinga kwa kuwekeza sehemu ambazo zina faida ndogo na hatari ya kupoteza, utamjibuje?

6. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Back
Top Bottom