2008: Mwaka uliotesa vigogo
Mwandishi Wetu Disemba 31, 2008
MWAKA 2008, utakumbukwa kuwa wa kuporomoka kisiasa kwa baadhi ya vigogo, baadhi wakijikuta katika kuta za magereza na wengine wakihofia kupita mitaani kwa uwazi, kwamba wanaweza kuzomewa.
Ni mwaka wa kihistoria kwa Rais Jakaya Kikwete. Mawaziri wanne, akiwamo Waziri Mkuu, walijikuta wakibisha hodi Ikulu kuwasilisha barua za kuomba kujiuzulu tena kwa shinikizo ambalo msingi wake ni kashfa.
Rais alipokea barua ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, akapokea barua ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge.
Mwanzo (Januari) na mwisho (Desemba) wa mwaka 2008 unafanana. Ni mwaka ulioanza kwa hofu miongoni mwa vigogo na hivyo ndivyo unavyokwisha.
Mwanzoni mwa mwaka 2008, msingi wa hofu kwa baadhi ya vigogo ulikuwa kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Lakini wakati mwaka 2008 ukianza kwa hofu ya Richmond, pia unakwisha kwa hofu ambayo msingi wake ni wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na matumizi mabaya ya ofisi.
Vigogo walionusurika kuburuzwa mahakamani hadi sasa wanarejea kumbukumbu zao na kujiridhisha kama waliwahi kutumia vibaya madaraka waliyopewa kitaifa.
Na bila shaka, wengine walioko kwenye orodha ya kushitakiwa wanashukuru kwa kupumua kidogo japo mwaka uishe kwanza.
Mwaka 2008 ulianza wakati baadhi ya vigogo wakiwa katika hofu wasijue hatima yao hasa wakati kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ilipokuwa mikononi mwa uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge, iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe.
Miongoni mwa viongozi watakaoukumbuka mwanzo wa mwaka 2008 ni pamoja na Lowassa, Karamagi na Dk. Msabaha. Februari mwaka 2008, itakumbukwa sana na viongozi hawa. Huo ndio mwezi ambao Richmond iliwaporomosha kutoka katika matawi ya juu ya kisiasa nchini.
Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa Novemba 13, mwaka 2007, na kupewa siku 30 kukamilisha kazi yake, ikiwa na hadidu za rejea sita iliwaporomosha kisiasa viongozi hao.
Hadidu hizo za rejea za kamati hiyo ni pamoja na: kubainisha Richmond Development Company LLC ni kina nani, na ni kampuni ya shughuli zipi na hivyo kupima uwezo wake kupatiwa zabuni ya kuleta nchini na kujenga mtambo wa umeme wa gesi wa megawati 100.
Pili, kutathmini mchakato mzima wa jinsi zabuni waliyoshinda Richmond ilivyoshughulikiwa kuanzia kamati ya zabuni hadi mwisho ili kujiridhisha kuwa sheria, taratibu, miiko na maadili ya zabuni yanayotawala zabuni za aina hiyo vilifuatwa au la.
Tatu, kutathmini mkataba baina ya Richmond Development Company LLC na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa masharti ya mkataba huo ukizingatia gharama na masharti mengine kwa kulinganisha na masharti yaliyomo katika mikataba ya aina hiyo iliyoafikiwa na TANESCO au Serikali.
Nne, kubainisha huduma na misaada mbalimbali waliyopewa Richmond kama vile kufunguliwa Letter of Credit na kupima uhalali wake.
Hadidu ya tano ya rejea kwa kamati hiyo ilikuwa kuziangalia na kuzitolea maoni taarifa za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) na taarifa zozote nyingine zilizoangalia utaratibu wa zabuni ya Richmond.
Hadidu ya mwisho ya rejea kwa kamati hiyo ilikuwa kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na mchakato mzima wa Richmond ili kutoa mapendekezo ya kuboresha taratibu za zabuni kwa siku zijazo, kwa maslahi ya Taifa.
Hatimaye, ripoti ilisomwa na matokeo yake ni kujiuzulu kwa mawaziri hao. Hata hivyo, ripoti hii ilivuta hisia za wengi wakati inasomwa bungeni hasa pale mwenyekiti wake, Dk. Mwakyembe alipoamua kutaja mambo waliyodokezwa na waliowahoji nje ya kiapo.
Hayo ni mambo waliyodokezwa kwa siri na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Msabaha na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi Fulgence Kazaura. Kamati hiyo Teule iliwahoji mashahidi 75 na kuuliza maswali 2,717 na kupitia nyaraka na kumbukumbu 104.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, Msabaha aliwauma sikio (nje ya kiapo) akisema; Katika suala hilo atakuwa kondoo wa kafara tu au, kwa maneno yake mwenyewe, Bangusilo kwa lugha ya Kizaramo.
Mbali na Dk. Msabaha pia, Balozi Kazaura aliwauma sikio akina Mwakyembe akawadokeza; Richmond ilikuwa mradi wa bwana mkubwa na mshiriki wake mkubwa kibiashara
Lakini mbali na kashfa ya Richmond kuwaporomosha Lowassa, Karamagi na Msabaha pia iliacha gizani hatima ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na baadhi ya viongozi katika Wizara ya Nishati na Madini.
Dk. Hosea hatima yake ilibaki gizani baada ya TAKUKURU anayoiongoza kuwahi kuchunguza mchakato wa zabuni kwa Richmond na kubaini kuwa hapakuwa na kasoro katika mchakato huo.
Lakini saratani ya kashfa ya Richmond haikuishia hapo, ilisababishwa kuvunjwa kwa Serikali. Baraza jipya la mawaziri likatangazwa, baadhi ya mawaziri wakongwe na wenye majina mazito wakaporomoka.
Yote haya yalitokea Februari 2008, na kuporomoka kwa mawaziri hao wakongwe kukapichikwa msamiati wameomba kungatuka.
Watu wakajiuliza, vipi watu wanangatuka katika nafasi za uteuzi? Kwani walikuwa na uhakika gani kuwa watateuliwa. Je, ni Rais ndiye aliyewashinikiza kungatuka?
Hao ni pamoja na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Harith Bakari Mwapachu, Joseph Mungai na Basil Mramba. Mawaziri wengine waliokuwa wakingara waliporomoka, hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji. Meghji pengine angeweza kubaki katika baraza jipya la mawaziri lililotangazwa Februari, lakini nyota yake ilififia zaidi pale alipoyumba katika maelezo yake kuhusu sakata la wizi wa fedha BoT.
Katika moja ya kauli zake kuhusu wizi wa mabilioni BoT, Meghji alidai aliyekuwa Gavana wa Benki hiyo, Dk. Daudi Ballali (sasa marehemu), alimdanganya katika barua.
Hata hivyo, kashfa hii ya Richmond ilifanikisha kumuibua Mizengo Peter Kayanza Pinda, kutoka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hadi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaweza kusema ya kuwa huu ulikuwa ni mwaka wa mafanikio kikazi kwa Mizengo Pinda.
Mbali na kashfa hiyo iliyowaporomosha wanasiasa, kashfa ya EPA katika BoT iliporomosha viongozi wengine watendaji, akiwamo aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk. Ballali.
Kama ilivyo kwa Richmond, EPA nayo iliwaweka roho juu wahusika ambao baadhi tayari wameanza kufikishwa mahakamani.
Wafanyabiashara wakubwa kama Jeetu Patel anayetajwa kuwa na uhusiano wa karibu na vigogo waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hawatausahau mwaka huu wa maporomoko. Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kigoma, Rajabu Maranda, naye amelala gerezani kwa kashfa hii ya EPA.
Aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, naye mwaka 2008 anaweza kuutambua kama mwaka wa maporomoko.
Chenge aliporomoka kisiasa hasa baada ya kubainika kuwa anamiliki akaunti nono ya Sh zaidi ya bilioni moja katika akaunti ya benki moja katika kisiwa Jersey.
Kashfa ya Chenge kuchunguzwa na Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) na kubainika kumiliki akaunti hiyo nono, iliibuka wakati akiwa ziarani na Rais Jakaya Kikwete nchini China, Aprili, 2008.
Ni kashfa iliyoibuliwa kwa mara ya kwanza na gazeti la The Guardian la Uingereza. Ilikuwa Aprili 16, Chenge alirejea nchini akitokea China na akapokewa na waandishi wa habari, katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Aliulizwa kuhusu kashfa hiyo. Akajibu; "Unapotuhumiwa, uchunguzi unafanyika, kwa kanuni na taratibu za uchunguzi, siruhusiwi kuzungumza. Kwa sasa ni mapema mno, tuvipe nafasi vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake,"
"Hoja ya msingi hapa ni kwamba, nimelipwa fedha na Kampuni ya BAE System (ya Uingereza) katika ununuzi wa rada. Tuhuma hiyo ni nzito kweli kweli na si ya kuropoka,"
Wakimaliza uchunguzi wao then wakiuliza Bw. Chenge hivi vijisenti ulivipateje ndipo nitaeleza.
Vijisenti ni kauli ambayo inatajwa kumgharimu mno Chenge ambaye baada ya mjadala kuhusu kauli yake hiyo kupamba moto alijitosa na kuomba msamaha Watanzania akisema yeye ni Msukuma Kiswahili chake si kizuri.
Hata hivyo, siku aliporejea nchini kutoka nchini China Chenge aliwaambia waandishi wa habari kuwa katu hatajiuzulu. Lakini siku kadhaa baadaye alimwandikia barua Rais Kikwete akiomba kujiuzulu.
Wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wakaamini kuwa uamuzi huo wa Chenge umetokana na shinikizo kutoka ngazi za juu, na bila shaka kutoka kwa Rais.
Kashfa ya Chenge kwa kiasi kikubwa iliamsha hisia za wanasiasa na hasa wa kambi ya Upinzani na baadhi ya wanaharakati nchini. Baadhi ya wanasiasa wakawasili ofisi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Wakataka waonyeshwe fomu zinazotumiwa na viongozi kujaza orodha ya mali zao.
Wanasiasa hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema na Erasto Tumbo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Walitaka kuonyeshwa fomu za mali za viongozi waliwaohi kutajwa katika orodha ya watuhumiwa wa ufisadi, iliyopachikwa jina la List of Shame.
Viongozi wengine walioporomoka kwa kishindo mwaka 2008 ni Waziri katika Serikali mbalimbali, ikiwamo ya Awamu ya Kwanza, Basil Mramba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Awamu ya Tatu, Daniel Yona.
Hawa wameburuzwa mahakamani, wamesafiri kwa mabasi ya mahabusu na wakalala rumande. Maisha hayo ya gerezani ya akina Mramba na Yona ndiyo yamemkuta aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.
Mivutano baina ya vigogo
Lakini mbali na vigogo kuporomoka, mwaka 2008 umeshuhudia malumbano na mivutano baina yao.
Kati ya mambo yaliyoibua mvutano na hasa kati ya viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni suala la Zanzibar ni nchi au la.
Baadhi ya viongozi walianza kuonyesha dalili za wazi za kuchoshwa na Muungano wa sasa wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Miongoni mwa vigogo waliocharukia suala hilo ni Naibu Waziri Kiongozi wa SMZ, Juma Ali Shamhuna. Kwa nyakati tofauti, Shamhuna alionekana kutaka kushambulia kauli za Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Pinda aliwahi kuulizwa bungeni katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, kwamba Zanzibar ni nchi au la. Akajibu kwa kurejea matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, akasema si nchi.
Mvutano mwingine wa hatari uliojitokeza nchini ni kuhusu suala la Tanzania kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu Tanzania (OIC). Haukuwa mjadala mpya mbele ya Watanzania, uliwahi kuibuka na kusinzia.
Lakini mwaka 2008, aliyechokoza alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Kwa maoni yake, Membe haoni tatizo kwa Tanzania kujiunga na OIC.
Malumbano mengine yaliyoshuhudiwa mwaka 2008 ni kati ya mfanyabiashara anayemiliki baadhi ya vyombo vya habari nchini, Reginald Mengi, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha.
Mengi alizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kudai kuwa katika kikao fulani cha viongozi kilichofanyika Dar es Salaam, Waziri mmoja kijana na msomi alipendekeza kuwa yeye (Mengi) abambikiziwe kiasi kikubwa cha kodi ili ashindwe kulipa na hatimaye afilisiwe.
Kwa mujibu wa Mengi, msingi wa mapendekezo ya waziri huyo unatokana na kile kinachodaiwa vyombo vya habari vya Mengi kushabikia vita dhidi ya ufisadi.
Lakini siku kadhaa baada ya Mengi kutoa kauli hiyo, Waziri Masha ambaye hakuwapo nchini katika siku ambayo Mengi alitoa kauli hiyo akapanda munkari.
Akampa siku saba Mengi kuwasilisha ushahidi wake huo na waandishi wa habari wakamuuliza Mengi kuhusu maoni yake naye akasema siku saba ni nyingi mno.
Hata hivyo, hadi mwaka unakwisha hatima ya suala hilo haijulikani na zaidi ya mwezi sasa umepita.
Taasisi zilizovuta hisia za Watanzania
Kati ya taasisi zilizotia fora kwa kuvuta hisia za Watanzania wengi ni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Taasisi ya Kuzuiya na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Taasisi hizi zilivuta hisia za Watanzania wengi baada ya vigogo wa wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wengine kuanza kufikishwa mahakamani.
TAKUKURU, IGP kwa niaba ya Jeshi la Polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo waliokuwa wakichunguza mafaili ya wezi wa fedha za EPA. Wakakabidhi ripoti ya uchunguzi wao kwa Rais Kikwete ambaye aliagiza mafaili hayo yafikishwe kwa DPP kwa hatua zaidi.
Mashirika, taasisi zilizovutana na Serikali
Kati ya taasisi zilizojikuta katika mvutano na Serikali ni pamoja na Benki ya NMB na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), huku Kampuni ya Reli Tanzania ikijikuta katika ukata hadi kushindwa kulipa mishahara wafanyakazi wake.
Fedha ndiyo msingi wa taasisi hizi kujikuta katika mvutano na Serikali. Walimu kupitia CWT walikuja juu wakitaka kulipwa malimbikizo yao ya posho, nyongeza ya mishahara na fedha za matibabu na usafiri.
Lakini wakati walimu wakidai hayo, Serikali ilipaza sauti ikitaka ufanyike uhakiki kwa sababu haikuwa na imani na kiasi kilichotajwa na walimu kilipwe.
Taasisi nyingine iliyotumbukia katika mvutano na Serikali ni Vyuo Vikuu na hasa serikali za wanafunzi vyuoni. Mvutano uliobuka ni wanafunzi kutaka wote wapewe mkopo wa elimu kwa asilimia 100 tofauti na ilivyo sasa.
Serikali iliwajibu wanafunzi hao kuwa haina uwezo huo. Na wanafunzi wakatangaza mgomo, na matokeo yake ni vyuo vya umma kufungwa.