Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,743
- 25,564
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.
NITAKAPOKUFA 1.
Mlango ulisikika ukigongwa kifujo fujo na mzee Kessi ambaye alikuwa ametoka kunywa pombe za kienyeji katika mtaa wa pili kutoka katika mtaa huo aliokuwa akiishi wa Kilingira uliopo Bagamoyo. Sauti yake kali iliyojaa ulevi ilikuwa ikisikika kwa juu sana huku akimtaka mke wake aufungue mlango huo.
Mzee Kessi hakuwa na uwezo wa kusimama wima na kutulia, muda wote alikuwa akiyumbayumba tu kutokana na kunywa kiasi kikubwa cha pombe za kienyeji. Miguuni, mzee Kessi alikuwa na kiatu kimoja tu, chupa moja ya maji ya uhai ambayo ilikuwa na pombe hiyo ya gongo ilikuwa mkononi mwake. Shati lake lilikuwa limeloa jasho, kwa kifupi, hakuonekana kuwa na utanashati wowote ule.
Bi Fatuma alikuwa chumbani kwake, usingizi kwake ukaonekana kuwa mzito kupatikana. Muda wote alikuwa akijigalagaza tu kitandani lakini bado usingizi haukupatikana. Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimfikiria mume wake, mzee Kessi ambaye alikuwa kilabuni akinywa gongo.
Tayari ilikuwa imetimia saa saba usiku lakini bado mzee Kessi hakuwa amerudi nyumbani kitu ambacho kilionekana kumnyima raha Bi Fatuma. Ilipofika saa nane na robo usiku, akasikia mlango ukigongwa kifujo fujo huku sauti ya mumewe ikisikika ikimtaka kuufungua mlango hata kabla hajauvunja.
Huku akionekana kuwa na uchovu mwingi, Bi Fatuma akainuka na kuanza kuelekea ulipokuwa mlango na kisha kuuufungua. Kwanza akakutana na harufu mbaya na kali ya pombe, akaziba pua yake huku mume wake akiingia ndani. Mzee Kessi alikuwa akitembea huku akiyumbayumba kama kawaida yake.
Breki yake ya kwanza ilikuwa katika makochi yaliyokuwa sebuleni hapo, makochi ambayo yalikuwa yamechakaa kupita kawaida. Akajilaza mahali hapo huku pombe yake iliyokuwa katika chupa ya uhai akiwa ameikumbatia kana kwamba hakutaka mtu yeyote aichukue kutoka katika mkono wake.
“Twende ndani ukalale mume wangu” Bi Fatuma alimwambia mume wake, mzee Kessi ambaye hakuonyesha hata dalili kwamba angekwenda kulala chumbani.
“Niache nilale hapa hapa” Mzee Kessi alisema kwa sauti iliyojaa ulevi.
Kila kitu kilikuwa kikionekana kuwa kama zamani. Mzee Kessi alikuwa akilewa kila siku jambo ambalo lilionekana kumkasirisha sana mke wake, Bi Fatuma. Mara kwa mara mzee Kessi alikuwa akirudi nyumbani hapo usiku mkali huku akiwa amelewa kupita kawaida.
Maisha ya ulevi yakaonekana kuwa sehemu ya maisha yake, hakupenda wanawake hata kidogo, starehe yake kubwa wala haikuwa ngono kama walevi wengine, pombe ndio ilionekana kuwa starehe yake kubwa ambayo alikuwa akiipenda kupita kawaida.
Miaka mingi ya nyuma, mzee Kessi hakuwa mlevi kabisa, alikuwa mtu safi, Muislamu ambaye alikuwa akiswali swala tano kila siku. Kila kitu kikaanza kubadilika pale ambapo alipokuja kuchujwa kazini kutokana na kampuni kuwa na wafanyakazi wengi ambao wengine hawakuonekana kuwa na kazi yoyote kazini.
Tukio lile likaonekana kumhuzunisha sana mzee Kessi, kila siku akawa mtu wa mawazo, japokuwa mke wake alikuwa akimfariji sana lakini faraja ile wala haikuonekana kubadilisha kitu chochote kile. Hapo ndipo alipoamua kuanza kunywa pombe kwa kisingizo cha kupunguza mawazo aliyokuwa nayo.
Kila alipokuwa akilewa, mawazo yalikuwa yakimtoka kichwani mwake lakini pombe zilipokuwa zikiisha kichwani mwake, mawazo yalikuwa yakirudi kama kawaida. Mzee Kessi hakufikiria kuanzisha biashara yoyote ile japokuwa alikuwa amelipwa kiasi kikubwa cha fedha. Fedha ambazo alikuwa ameliwa akaziingiza kwenye ulevi.
Baada ya mwaka mmoja kupita, hali ya umasikini ambayo ilikuwa ikiwanyemelea ikawaingia. Fedha zikakatika, hapo ndipo akili ya mzee Kessi ilipoanza kukaa sawa. Akaanza kufanya kazi mbalimbali kama ujenzi na kazi nyingine ndogondogo.
Hawakuweza kugharamia gharama za chumba kikubwa ambacho walikuwa wakikaa maeneo ya Block P jambo ambalo likawafanya kuhamia Kisutu tena katika nyumba mbovu isiyokuwa na thamani yoyote ile.
“Mtakaa kwa muda kabla ya nyumba hii kubomolewa. Nimeamua kukusaidi kwa sababu sisi ni marafiki wa kitambo sana” Mzee Shomari alimwambia mzee Kessi.
Hapo ndipo maisha yao yalipoanzia. Maisha ya ndoa hayakuwa ya amani hata mara moja, kila siku mzee Kessi alikuwa akimpiga mke wake hasa katika kipindi ambacho alikuwa akilewa na kurudi nyumbani. Bi Fatuma alionekana kuwa mvumilivu kwa kila kitu, japokuwa alikuwa akipigwa lakini alikuwa akimpenda sana mume wake.
Siku zikaendelea kukatika, maisha ya Kisutu yakaonekana kuwazoea. Mara kwa mara mzee Kessi alikuwa akigombana na majirani zake kwa tabia zake za kurudi usiku na kupiga kelele ovyo. Japokuwa alikuwa akigombana sana na majirani zake lakini kamwe mzee Kessi hakutaka kubadilika, ndio kwanza alikuwa akipiga kelele zaidi na zaidi kila siku.
Katika maisha yao ya miaka ishirini na tano ya ndoa ambayo waliishi pamoja kama mume na mke, wawili hao walifanikiwa kupata mtoto mmoja tu wa kiume aliyeitwa Yusufu. Kipindi cha nyuma Yusufu ndiye ambaye alionekana kuwaunganisha wote wawili na kuwapa amani kubwa katika maisha yao ya ndoa, walimthamini sana Yusufu na kumpa kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji kama mtoto wao, hasa katika kipindi kile ambacho walikuwa na fedha za kutosha.
Kwa sasa Yusufu hakuwa pamoja nao, alikuwa amekwishaanza maisha yake ndani ya jiji la Dar es Salaam huku muda mwingi akiwa anaelekea Bagamoyo kwa ajili ya kuwaona wazazi wake. Hali ambayo walikuwa nayo wazazi wake ikaonekana kumuumiza sana jambo ambalo likamfanya kutafuta sana fedha ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuwatunza wazazi wake ambao walikuwa wakiishi maisha mabovu ambayo hakuyapenda kabisa.
“Nitapata fedha tu na ninyi mtaishi kwenye nyumba nzuri kama ile ya mtaa wa Block P” Yusufu alikuwa akipenda kuwaambia wazazi wake maneno hayo katika kila kipindi alichokuwa akienda kuwasalimia.
*****
Maisha ndani ya jiji la Dar es Salaam hayakuwa rahisi hata mara moja. Kila siku Yusufu alikuwa akifanya kazi mbalimbali lakini wala hazikuweza kubadilisha maisha yake. Kazi zake zilianzia katika kubeba mizigo katika soko la Tandale, huko, maisha yaliendelea kuwa vile vile jambo ambalo likamfanya kuamua kufanya kazi ya ukonda, kwa mbali maisha yake yakaonekana kupata mwanga.
Japokuwa kila siku Yusufu alikuwa na uhakika wa kupata fedha zaidi ya shilingi elfu kumi lakini gharama mbalimbali za maisha ya Dar es Salaam zikamfanya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kila siku ambacho hadi inafika usiku, hakuwa na fedha za kutosha mifukoni mwake.
Maisha yale yalikuwa yakimuumiza sana, hakuyapenda maisha yale ya umasikini ambayo alikuwa akiishi katika kipindi kile, nafsi yake ilikuwa ikitamani kuishi maisha ya kifahari, maisha ya kutanua mitaani na gari, maisha ya kuchukua kila aina ya msichana ambaye alikuwa akimtaka.
Maisha yaliendelea zaidi na zaidi, urafiki wake na Kelvin ukaonekana kuwa mkubwa, wakapanga chumba kimoja na kuishi pamoja. Gharama za kulipia chumba ilikuwa jukumu lao wote. Kila siku asubuhi wote walikuwa wakitoka pamoja na kwenda kutafuta fedha kwa kufanya kazi mbalimbali na usiku kurudi wote.
Maisha hayakuonekana kubadilika, kila walipokuwa wakipata fedha ambazo wala hazikumaliza shida ambazo walikuwa nazo. Fedha ambazo walikuwa wakizipata ziliwatosha katika chakula na kubadilisha mavazi tu.
“Maisha magumu sana” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Yaani ni magumu kiasi ambacho wakati mwingine nafikiri ni bora ningekuwa mwizi tu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hivi hali hii tutakuwa nayo milele au kuna siku itakuja kubadilika?” Kelvin aliuliza.
“Mmmh! Nafikiri itakuwa hivi milele. Kama unaona kuna siku itakuja kubadilika, itabadilika vipi? Tutapata vipi fedha za kufanyia mambo mengine ambayo hatujayafanya?” Yusufu aliuliza.
“Kufanya mambo gani zaidi?”
“Kumiliki magari, kuwa na mademu wakali, fedha za kutosha na kufanya mambo mengine pia” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Yaani bado unafikiria wanawake tu?” Kelvin aliuliza huku akitabasamu.
“Wewe unafikiri nitafikiria nini zaidi? Ili ujione umefanikiwa katika kila kitu basi ni lazima utembee na msichana yeyote unayemtaka kwa kipindi hicho. Hivi unafikiri kama ningekuwa na fedha yule Agness angenikataa?” Yusufu alisema na kuuliza.
“Ndio. Angekukataa” Kelvin alijibu.
“Thubutuuuuu. Niwe nimemfungia breki miguuni mwake na Range, nashusha kioo na kisha kuongea naye, unafikiri angenikataa. Acha masihala Kelvin, fedha ndio kila kitu katika maisha haya” Yusufu alimwambia Kelvin.
Siku hiyo ilikuwa kama siku nyingine tu, muda wote walikuwa wakiongea kuhusu fedha, walikuwa wakihitaji fedha kuliko kitu chochote kile katika maisha yao. Maisha ya kifahari ambayo walikuwa wakiishi watu wengine yalikuwa yakiwatamanisha kupita kawaida.
“Hivi inakuwaje kuhusu kipaji chako cha muziki? Hakitaweza kukutoa kwenye maisha haya kweli?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Mmmh! Nafikiri hakiwezi” Yusufu alijibu.
“Hakuna bwana. Inakupasa kujaribu, huwezi jua, unaweza kuwa kama The King” Kelvin alimwambia Yusufu huku akimtaja msanii wa muziki ambaye alikuwa juu sana katika kipindi hicho nchini Tanzania.
“Kitu cha kwanza ni lazima tukumbuke kwamba kurekodi muziki si chini ya shilingi laki tano. Unaweza ukagharamia muziki kwa kiasi hicho halafu mwisho wa siku Madj wa vituo mbalimbali wakaanza kukubania tena” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Ila ngoja tujaribu” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Poa. Ila fedha tutazipata wapi? Kutunga nyimbo si jambo gumu kwangu, tatizo upatikanaji wa fedha za kurekodia tu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hakuna jinsi Yusufu. Kila kitu kinaonekana kuwa kigumu kwetu. Nitafanya kitu kimoja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba unapata fedha za kurekodia” Kelvin alimwambia Yususfu.
“Kitu gani?”
“Kuiba”
“Acha masihala Kelvin”
“Hakuna jinsi Yusufu. Acha nijaribu kwa ajili yako ila nakuomba nawe fanya kitu kimoja tu” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Kitu gani?”
“Tunga wimbo mkali, wimbo ambao kila atakayeusikia ataupenda na kuanza kukuita sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutumbuiza kwenye matamasha mbalimbali” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Hilo si tatizo. Ila na wewe itakubidi kuwa makini kwenye kufanya huo wizi wako. Si unajua sitaki kukupoteza” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Najua. Usijali, kila kitu kitakuwa sawa” Kelvin alimwambia Yusufu na kisha kulala huku kila mtu kichwa chake kikifikiria fedha tu.
*****
Muda ulikuwa ni saa 2.14 asubuhi, Kelvin alikuwa akilandalanda katika barabara za Posta Mpya huku macho yake yakiangalia katika kila gari ambalo lilikuwa limepakiwa. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kufanya wizi wa kitu chochote kile ambacho atakiuza na mwisho wa siku kupata fedha ambazo zitamfanya Yusufu kuingia studio na kurekodi muziki.
Idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakitembea huku na kule ilimfanya kuhofia sana kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya. Mara nyingi alikuwa akiyaona magari ambayo ndani kulikuwa na laptop pamoja na simu za gharama kubwa lakini kukishusha kioo kwa kutumia waya mgumu aliokuwa nao lilikuwa jambo gumu kufanyika.
Alipoona kwamba kila kitu kimeshindikana, hapo ndipo akaamua kwenda katika ghorofa la Macafee lililokuwa Posta mtaa wa Samora View na kisha kupanda kule ambako magari yalikuwa yakiegeshwa. Kelvin akaanza kutembea huku na kule huku akiyaangalia magari yale ambayo yalikuwa yamepakiwa.
Tayari hali ikaonekana kuwa rahisi kwake, kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu ikaonekana kuwa kama nafasi kubwa kwake ya kuanza kufanya kile ambacho alikuwa amepanga kukifanya. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kulifuata gari moja la kifahari, Range ambalo lilikuwa limepakiwa pembezoni kabisa mwa sehemu ile ya kuegesha magari.
Alipolifikia, akaanza kuangalia huku na kule kuona kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akimwangalia, alipoona kwamba kila kitu kipo salama, akaanza kuchungulia ndani ya gari lile huku akiuandaa waya wake.
Macho yake yakatua kwenye laptop moja aina ya Apple pamoja na simu mbili za aina ya iPhone 5. Kelvin hakutaka kuchelewa, kwa hali jinsi ilivyoonekana, ilionyesha kwamba mwenye gari angerudi muda wowote ule kutokana na vitu vyake vyote kuwa ndani ya gari.
Akauchukua waya wake na kisha kuupitisha kwenye uwazi wa kioo ambao ulikuwa umeachwa kwa ajili ya hewa na kisha kuangaika kuitoa loki kwa kutumia waya ule. Kazi haikuwa ndogo hata kidogo, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka huku akihakikisha kwamba haligusi gari hilo hata kidogo kwa kuona kwamba lingepiga kelele ya kumshtua mmiliki wa gari lile.
Alijitahidi sana huku kijasho kikiendelea kumtoka, kila alipokuwa akiikamata loki ya mlango wa gari ile na kujaribu kuivuta kwa kutumia waya ule, loki ilionekana kuwa ngumu kuvutika. Kelvin hakutaka kukata tamaa, kila alipokuwa akiziangalia mali zilizokuwa ndani ya gari lile aliendelea kuvuta zaidi na zaidi.
Huku akiwa anaendelea na kazi yake, mara sauti za watu zikaanza kusikika kutoka katika upande mwingine jambo lililomfanya kuinama na kuanza kusikilizia kwa makini kama watu wale walikuwa wakija upande aliokuwepo. Akasikia mlango wa gari moja ukifunguliwa, watu wale kuingia na kisha gari kuwashwa na kuondoka mahali hapo.
Kelvin akaendelea kufanya kazi yake kama kawaida. Hakujua alijisahau vipi mpaka kuligusa gari lile, ghafla likaanza kupiga kelele. Kadri sekunde zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo kelele zile zilivyozidi kuwa za juu zaidi na zaidi jambo ambalo liliwashtua walinzi ambao walikuwa wamewekwa kuhakikisha ulinzi wa magari yale yaliyokuwa yamepakiwa kwenye ghorofa ile kwa juu.
Vishindo vya watu vilikuwa vikisikika vikija kule ambako alipokuwepo, sehemu ambayo gari ile ilikuwa ikiendelea kupiga kelele. Kelvin alikuwa akiendelea zaidi na zaidi kuhakikisha kwamba mlango unafunguka na kisha kuchukua mali zile ambazo zilikuwa kwa juu kabisa.
Kila alipokuwa akijitahidi kutoa loki ile, loki ilionekana kuwa ngumu kufunguka jambo ambalo lilionekana kumtia wasiwasi zaidi. Kuondoka mahali hapo hakutaka kabisa, hakutaka kuondoka na kuziacha mali zile ambazo kwa haraka haraka zilikuwa na thamani isiyopungua milioni sita.
“Funguka. Loki funguka” Kelvin alisema huku akiendelea kufungua loki ile kwa kutumia waya mgumu huku walinzi wale wakizidi kusogea kule kulipokuwa na gari lile ambalo lilikuwa likizidi kupiga kelele.
*****
Walinzi ambao walikuwa na bunduki walikuwa wakizidi kusogea kule ambako kulikuwa na gari lile lililokuwa likipiga kelele, tayari walikwishajua kwamba kuna mtu ambaye alikuwa ameligusa gari lile na hivyo kuanza kupiga kelele. Tayari wasiwasi kwamba mtu aliyeligusa gari lile alikuwa mwizi ukaanza kuwaingia akilini.
Wakaziandaa silaha zao tayari kwa ajili ya kumfyatulia risasi mtu huyo ambaye alikuwa ameligusa gari lile kwa lengo la kuliiba au kuiba kitu chochote kile ambacho kilikuwa ndani ya gari lile. Wakaongeza kasi zao zaidi na zaidi mpaka kulifikia gari hilo ambali lilikuwa likiendelea kupiga kelele kama kawaida.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akionekana mahali hapo, milango yote ilikuwa imefungwa kama kawaida japokuwa gari lile lilikuwa likiendelea kupiga kelele. Walichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kuangalia huku na kule kuona kama wangeweza kumuona mtu yeyote ambaye alikuwa ameligusa gari lile lakini hawakumuona mtu yeyote.
“Mbona patupu?” Mlinzi mmoja alimuuliza mwenzake.
“Inawezekana kuna ndege aliingia na kuligusa” Mlinzi mwingine alimwambia mwenzake.
“Labda inaweza kuwa hivyo”
Mara mmiliki wagari lile ambaye alikuwa mwanamke wa makamo akatokea mahali hapo huku akiwa na ufunguo wa gari lake na kisha kuanza kuwaangalia walinzi wale ambao walikuwa wamesimama pembeni ya gari lake.
“Kuna nini? Alamu imenishtua kwamba kuna kitu kimetokea garini mwangu?” Mwanamke yule aliuliza.
“Hata sisi tulisikia alamu na ndio maana tukafika haraka sana ila hatukuona mtu. Inawezekana kuna ndege alikuja na kutua kwenye gari lako” Mlinzi mmoja alimwambia mwanamke yule.
Alichokifanya mwanamke yule ni kuufuata mlango wa gari lake na kisha kuufungua. Macho yake hayakuamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali pale, laptop yake pamoja na simu zake mbili hazikuwa zikionekana. Hapo hapo akawageukia walinzi huku macho yake yakionekana kubadilika.
“Nani kachukua simu zangu na laptop yangu?” Mwanamke yule aliuliza swali ambalo liliwafanya walinzi wote kushangaa.
“Unasemaje?” Mlinzi mmoja aliuliza.
“Nani ameniibia simu zangu na laptop yangu?” Mwanamke yule aliuliza kwa sauti ya juu.
Walinzi wote wakapigwa na mshangao, maneno aliyoongea mwanamke yule yakaonekana kuwashangaza kupita kawaida. Hawakujua kwamba kuna vitu vilikuwa vimeibiwa ndani ya lile gari, wakausogelea mlango ule na kuchungulia ndani.
“Nimeibiwa” Mwanamke yule alisema huku akionekana kukasirika.
“Mbona tulipokuja hapa hatukuona mtu yeyote?”
“Ila nimeibiwa. Nimeibiwa kila kitu nilichokiacha ndani ya gari langu. Hadi pochi yangu imeibwa ambayo ilikuwa na fedha nyingi pamoja na kadi yangu ya ATM” Mwanamke yule alisema maneno yaliyowafanya walinzi wale kuondoka mahali hapo na kuanza kuzunguka huku na kule kwa lengo la kumtafuta mtu aliyeiba simu, laptop na pochi ya yule mwanamke.
Je nini kitaendelea?
Je Kelvin atakamatwa?
Je Yusufu ataweza kutoka kimaisha na Kelvin?
Huu ni mwanzo tu, kuna mengi yanakuja na mengi mtajifunza.