SURA YA 6
Robisnon Kruso alitazama huku na huku akafikiri labda adui aweza kumrukia, lakini hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa yule kasuku wake, ambaye alilia, “Robin, Robin!” Alipokuwa akilia kasuku huyo alisugua mdomo wake penye shavu la Robinson.
Katika siku na majuma yaliyofuata, Robinson wakati wote alikuwa na wasiwasi katika kisiwa chake. Kwa hiyo ilimbidi ajilinde asishambuliwe na adui ghafla.
Siku moja alikuwa kilimani karibu na nyumbani kwake. Alipoangalia pwani aliona mitumbwi ikija kuelekea ufukoni. Alijificha mwituni karibu na ufuko. Mara mitumbwi ikafika ufukoni na wakashuka washenzi wakali sana, nao walikuwa na wafungwa ambao walikuwa wakiwatendea ukatili sana.
Robinson aliwaangalia wakati walipokoka moto mkubwa tayari kwa kula karamu yao na kucheza. Akafikiri, “Sijui alikuwa mmoja wa wale walioacha alama ya unyayo mchangani.”
Kisha alimuona mfungwa mmoja akijitahidi kujifungua kamba alizofungwa. Mtu yule aliruka ghafula akawakimbia washenzi wale wakali kama alivyoweza. Alipokuwa akikimbia hivyo wale washenzi walimtupia mikuki lakini hakusimama na wala haikumpata.
Robinson akawaza, “Sina budi kumsaidia mtu yule.” Basi alitoka mle mwituni, aliinua bunduki yake akawapiga wale washenzi ambao walikuwa wakimfukuza yule mfungwa. Watu wale walishikwa na hofu sana kwa bunduki ile, wakamwacha yule mfungwa aende zake. Wao wenyewe wakaingia ndani ya mitumbwi yao hali wakitambaa na kukimbia upesi.
Yule mtu mweusi aliyekuwa mfungwa wao, alipiga magoti mchangani. Kisha akaibusu miguu ya Robinson kuonyesha kwamba amekubali kuwa mtumwa wake.
Robisnon alichekelea akasema, “Njoo simama!” Yule mtu alielewa maana ya maneno ya Robinson ingawa hakufahamu maneno yenyewe. Alisimama akangoja.
Robinson akasema tena. “Njoo.” Naye akaanza kwenda upande ule wa kwenye kibanda, alimpungia mkono na yule mtu akaanza akumfuata.
Robinson alikwenda na furaha kwa kumuokoa mtu huyu. Walipokuwa wanakwenda aliwaza, “Atakaa nami na nitamfundisha kusema kiingereza.”
Yule mtu mweusi alikuwa na njaa sana. Tena alikuwa amechoka sana baada ya msukosuko alioupata. Basi Robinson alimpa chakula akamuonyesha mahali pa kulala. Alipoamka Robinson akakata shauri kwamba ni wakati wa kupeana majina.
Akasema . “Mimi Robinson,” huku akijionyeshea kidole, “Robinson.”
Yule mtu mweusi akainamisha kichwa chake . Alijibu polepole, “Robinson, Robinson.”
Kisha yule mtu akajinyoshea kidole kifuani pake akasema maneno fulani ambayo Robinson hakuweza kuyafahamu maana hakujua lugha yenyewe.
Alicheka akasema, “Sitaweza kabisa kusema hivyo. Hebu kwanza – nitakuita kwa jina la siku niliyokupata…Ijumaa.”
Basi jina la mtu yule likawa Ijumaa. Akawa mtumishi na rafiki muaminifu wa Robinson. Kila siku alijifunza maneno machache ya kiingereza mpaka akaweza kuongea na Robinson. Jambo hilo lilimfurahisha sana Robinson, maana alikuwa amekaa kwa muda mrefu bila ya kuwa na mtu wa kuzumngumza naye.
Alimuonyesha Ijumaa jinsi ya kutumia vyombo, na jinsi ya kutunza shamba na wale wanyama.
Siku moja Ijumaa alimwita Robinson , Je, huyu ndege wa ajabu anayezungumza naye nimpe chakula?”
Robinson akajibu, “Ndiyo waweza kumpa huyu kasuku mbegu. Huyu ni mpole. Hatakuuma.”
Alipoona kuwa Ijumaa aweza kuaminika kuchukua bunduki, alimfundisha jinsi ya kuitumia ili waweze kwenda kuwinda pamoja.
Kulikuwa na mambo mengine ambayo Ijumaa alimfundisha Robinson. Alimfundisha kutengeneza mtumbwi na mikuki ya kuvulia samaki, na jinsi ya kupanda minazi na kuangua nazi pevu.
Wakati walipokwenda kuwinda, Robinson alivaa mavazi yake ya ngozi za mbuzi, lakini maskini Ijumaa hakuwa na chochote cha kuvaa. Mvua iliponyesha, maji yalimwingia katika nywele zake na kutiririka katika ngozi yake. Yeye mwenyewe Ijumaa hakujali. Lakini siku moja Robinson alisema, “Lazima nawe uwe na mavazi kama yangu ya kukuhifadhi na jua na mvua.” Basi wote wawili wakaanza kumtengenezea Ijumaa mavazi ya ngozi ya mbuzi. Yalipokamilika na alipoyavaa, Ijumaa alirukaruka na kucheza kwa furaha.
Akasema kwa kiingereza kibovu, “Mimi kama wewe, bwana.”
Ijumaa alitaka kujua habari zote za nchi ya wazungu, na Robinson alimsimulia habari za miji na za merikebu zilizoweza kuvuka bahari kuu. Ijumaa alimwambia habari za watu wa kwao wanaoishi katika kisiwa kingine.
Robinson akastaajabu , akasema kwa nguvu, “Watu weupe! Labda hao ni mabaharia waliovunjikiwa na merikebu. Nitakwenda kuwatazama.