Hainan Airlines sasa kutua moja kwa moja Tanzania kutokea China

Kakke

JF-Expert Member
Joined
Dec 4, 2010
Posts
1,883
Reaction score
1,482

KAMPUNI ya Ndege ya Hainan ya China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.

Ahadi hiyo imetolewa leo mchana (Alhamisi, Oktoba 24, 2013) na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la Hainan (Hainan Airlines), Bw. Chen Feng baada ya kuombwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika mazungumzo yao alimwomba akubali

Ndege za shirika lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na Angola kupitia anga la Tanzania.



Picha ya kwanza: Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akizungumza na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la China la Hainan Airlines ,BW. Chen Feng. (na picha ya pili) Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akipokea mfano wa ndege kutoka kwa Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la China la Hainan Airlines ,BW. Chen Feng baada ya mazungumzo yao kwenye Hoteli ya Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu ambaye yuko ziara ya kikazi nchini hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za China ni kufikiria kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara pamoja na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli za kitalii. Pia alisema kuna Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua bidhaa hapa China lakini wanalazimika kuunganisha safari mara tatu hadi nne kabla hawajafika China jambo ambalo alisema linawaongezea gharama mno.

Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu, Bw. Chen alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi yake watayafanyia kazi na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja za ndege kutoka China kwenda Tanzania.

Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo iendelezwe ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana Tanzania kiwe kitovu cha usafiri wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda na kutoka China.

Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha usafiri wa China, ni lazima abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi zao.

Alisema dawa pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo litashirikiana na Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa kuwafikisha abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.

Pia alisema ili Dar es Salaam iwe kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa (international standards). Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini kushiriki katika kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe wa kisasa.

“Tuna wataaalam waliobobea katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya ndege vipatavyo 16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege inaweza kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.

Bw. Chen pia alisema suala la utalii ni la muhimu zaidi kwani anatambua kuwa Tanzania kuna vivutio vingi kama fukwe za bahari, mbuga za wanyama na vingine vingi na akaongeza kuwa shirika lake lina uzoefu wa biashara ya utalii kwani lina kampuni zinazofanya kazi ndani ya China na Hong Kong. “Tunaweza kusaidia kuwaleta Wachina waje kutalii Tanzania,” alisema Bw. Chen na kusisitiza kuwa wataangalia katika kuwekeza kwenye hoteli karibu na hifadhi za taifa.

Hainan ni moja ya mashirika makubwa ya ndege duniani. Ina ndege 470 na imeajiri wafanyakazi wapatao 1,000. Shirika hilo pia lina hoteli 500 za kitalii duniani na lina viwanja vya ndege vipatavyo 16 vikiwemo vitatu vya kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi za kujikomboa kiuchumi; lakini bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala ya usafiri wa anga ili iweze kupiga hatua kutoka hapo ilipo.

Alisema Tanzania kuna shirika la ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia muda huo kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua ATC ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan.

“Ndio maana tunawakaribisha nyinyi Hainan ni shirika kubwa ambalo naamini linaweza kuisaidia Tanzania katika eneo hilo la usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya safari za moja kwa moja hadi Tanzania; lakini pia na kuangalia namna ya kulifufua shirika la ndege la Tanzania (ATC),” alisema Waziri Mkuu.

Alimwomba Bw. Chen aangalie uwezekano kuja kujenga hoteli za kitalii karibu na viwanja vya ndege. “Iweje hoteli za utalii katika nchi yetu zijengwe na wafanyabiashara wa nchi za magharibi tu wakati na nyinyi mna uwezo wa kufanya vizuri zaidi hata kuliko wao?" Alihoji.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU
 
Hili sio jambo baya lakini tukubali kuwa na Taratibu na sharia za kuingiza vitu vya china ,maana kuna mambo 2 lazima viongozi wa nchi wangalie:

1.) Nikuingiziwa takataka za ki-china zisizo na kiwango yani mali Fake
2.) Nikutawaliwa biashara zote sasa na wachina huku Watanzania wakiwa hawana tena biashara.

Kwa hiyo nilazima tushemshe bongo kuhusu wachina wakivamia nchi, nchi nyingi wananchi wana kosa agira wakiingia wachina, kwa hio na sisi tuwe na sharia zetu na taratibu zetu, tukiteleza kidogo tu basi wachina watatuumbua, biashara zote watazitawala wao na kutaingizwa fake mpaka tujute.
 
Ni habari nzuri na ya kupongezwa kuwepo usafiri wa moja kwa moja kati ya nchi yetu na Uchina! Nakumbuka kama sikosei walitaka kuwekaza ktk ATC na kujenga Terminal mpya pale JKNIA wakati wa awamu ya kwanza ya Kikwete,wakakimbizwa na warasimu Serikalini!
 
Naunga mkono swala hili kweli tunahitaji ndege za moja kwa moja kwenda kwenye mataifa mengi si kwa Uarabuni peke yake. Challenge kubwa ni hiyo waliosema kuwa na shirika la ndege la Taifa (Tanzania) lenye nguvu. Hapo ndo ndoto. Air Tanzania imeshakufa wataifufuaje?
 
Well said mkuu, tatizo ni kwamba wanao ingia na kutoka wizarani ni Mawaziri tu lakini warasimu bado wapo pale pale na jeuri zao mpaka siku ya kustaafu, hao ndio janga la Taifa letu - bila ya ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais kusimamia suala hili hakuna kitakacho fanyika, Wachina watapigwa danadana mpaka warudi makwao au watakwenda kuwekeza Kenya na Uganda actually Wakenya wanatupiku sana katika kuchangamkia wawekezaji wa Kichina sisi tanabaki kwenye ngojera za kuhofia kuibiwa sijui bidhaa feki as if Wachina ndio wanawalazimisha wafanya biashara wetu kuingiza bidhaa zenye kiwango cha chini nchini - wakulahumiwa pale ni wafanya biashara Watanzania sio Wachina. Kiwanja cha ndege cha Julius kinaonekana kuchukua eneo kubwa sana baada ya kuhamisha wakazi, sasa eneo liko wazi tu! Kwa nini Serikali aitafuti wawekezaji wenye uwezo wakatujengea a very modern termials zaidi ya moja naona terminals nne zingekidhi demand, Hainan Airways inatakiwa iwe na ndege za aina mbili za kwa ajili ya usafiri kuja Tanzania - moja kwa ajili ya cargo tu na nyingine ya abiria; vile vile eneo lingine la kiwanja wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania wajenga four/five star Hotels, viwanda vya electronics i.e simu za viganjani, computers, vifaa vya mawasiliano nk.
 
Hiyo ndege itafanya safari si zaidi ya miezi sita ,usifikiri ni rahisi kuileta ndege direct kutoka china ,Watz ikiwa wataweza kuijaza ndege hiyo kwenda na kurudi basi poa ila kama dege hilo la watu miatatu mtaenda 20 na kurudi kuminatano ,itaonekana ni hasara na safari hizo kufungwa au kutafutwa link ingine, ila kitu kimoja nchi za jirani wakipata habari wataweza kusaidia kudumisha safari.

AIRTANZANIA (Twiga) zipo wapi ? Mmeua na kufungua zenu binafsi fanyeni muwe mnazipeleka huko tuone ?
 
Tembo wetu na pembe zitakua zinapanda ndege kirahisi sasa mamaa....!!
 
that's very fine waingie ubia kwanza ktk kuimarisha atc then waendelee na mpango wa pili,nb;-ni vema serikali ikatekeleza haraka mda wa kufikiri mno kama kikongwe hauna maana "after talks that follow is imediate action"
 
Punda wa sembe wajiandae kwenda kunyongwa kiulaini huko china!
 
Mbona unga utavunwa sana mwaka huu na wabongo ndiyo wataongoza kunyongwa huko China.
 
Punda wa sembe wajiandae kwenda kunyongwa kiulaini huko china!

Mzee pinda angewaombea msamaha waTZ 150 huko magerezani China kabla hajaruhusu wengine waende kunyongwa maana ukiweka safari ya moja kwa moja Mapunda wanaona simple maana umewarahisishia safari
 
Ni jambo zuri ngoja tuangalie upande wa nauli zao zitakuwa kiasi gani. Kwa sasa watanzania wengi kwenda China tunapanda Fuso( Ethiopian) dola 1300.
 
Baada ya ile mikataba 17 kusainiwa mwezi kati; juzi tena tumesaini mingine 7. Sasa na ndege ya moja kwa moja hadi uchina imeshatua - naona sasa ndoa yetu na wachina imekamilika - ila hatujui nani mke /mme.
 
Hiyo ni noma, moja kwa moja... Tanzania patajaa mateja sana...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…