Haki na wajibu kwa wafanyakazi wa kazi za ndani

Haki na wajibu kwa wafanyakazi wa kazi za ndani

Mr George Francis

JF-Expert Member
Joined
Jun 27, 2022
Posts
234
Reaction score
376
HAKI NA WAJIBU KWA WAFANYAKAZI WA KAZI ZA NDANI.
[Updated Thread, 2024]

[Prepared and posted on Facebook by Mr George Francis In 2021 & Posted On JamiiForums in 2022, now it's reposted here in 2024.]

KAZI ZA NDANDANI ni kazi zinazofanywa ndani au nje ya nyumba. Mfano: usafi wa nyumba, kufua, kupika, kulea watoto, kutunza mifugo nk.

Mfanyakazi wa kazi za ndani ni mtu yeyote anayefanya kazi za ndani, ndani ya uhusiano wa kazi.

Mfanyakazi wa kazi za ndani anazo haki za msingi na wajibu sawa na wafanyakazi wengine katika kazi nyingine.

Kumekuwa na wimbi kubwa la uvunjifu wa haki dhidi ya wafanyakazi wa kazi za ndani. Lakini pia nao wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao katika mambo mbalimbali.

Uvunjifu wa haki na wajibu unatokana zaidi na mwajiri au mwajiriwa kutokujua haki na wajibu wake pamoja na mipaka ya kazi husika kisheria.

Wafanyakazi wa kazi za ndani sawa na wafanya kazi wengine, wanalindwa na Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Kutokana na umuhimu wa kulinda haki na wajibu wa wafanyakazi wa kazi za ndani mwaka 2011 ulianzishwa mkataba maalumu wa kimataifa ambao Tanzania bado haijauidhinisha.

Mkataba huo unajulikana kama "DOMESTIC WORKERS CONVENTION, 2011 (No. 189).

Lakini ili wafanyakazi wa kazi za ndani waweze kulindwa na mkataba huu basi hatuna budi kuuidhinisha bungeni ili utumike mojakwamoja katika kulinda haki na wajibu wa wafanyakazi wa kazi za ndani.

Tunaliomba bunge letu na Serikali kwa ujumla iweze kuungalia kwa kina mkataba huu na kwa masrahi ya wafanyakazi wa kazi za ndani na kwa kuzingatia masrahi mapana ya nchi yetu mkataba huu uweze kuidhinishwa.

Pia tunaweza kwenda mbali zaidi katika kutunga sheria ya ndani itakayosimamia haki na wajibu wa wafanyakazi wa kazi za ndani.

Hii itasaidia sana kupunguza vitendo vya ukatili au uhalifu dhidi ya wafanyakazi wa kazi za ndani au dhidi ya watoto na watu wengine mahala pa kazi.

Wafanyakazi wa kazi za ndani wapo katika makundi makuu mawili.

1. Wafanyakazi wanaoishi na mwjiri wao majumbani.

2. Wafanyakazi wanaoishi nje ya nyumba wanayofanyia kazi. Yaani anaishi sehemu nyingine ila anakuja kufanya kazi na kuondoka.

Mfanyakazi wa kazi za ndani anaweza kuwa wa kike au wa kiume, inategemea na uhitaji wa mwajiri.

Hao wote wanatakiwa kulindwa kisheria kwa kuzingatia haki na wajibu wao katika kazi husika.

Kwanza kabisa Katiba ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, inaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kufanya kazi na kila mtu ana haki ya kupata malipo stahiki kuligana na kazi yake. Kama ilivyoandikwa katika ibara ya 22 na 23 ya Katiba.

Kwa mujibu wa Katiba yetu kila mtu ana haki ya kufanya kazi yoyote kama amekidhi vigezo vya kufanya kazi husika ikiwemo hizo kazi za ndani.

Sheria ya Kazi na Uhusiano Kazini imeweka kiwango sahihi cha umri wa mtu kuajiriwa kufanya kazi.

Umri sahihi wa mtu kufanya kazi ikiwemo kazi za ndani ni miaka 18 na kuendelea.

Lakini mtoto chini ya miaka 18 kushuka chini hadi miaka 14 anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi. Kazi ambazo hazitaathiri afya ya mtoto, masomo na ustawi wake kwa ujumla.

Hakuna mtu anayeruhusiwa kumwajiri mtoto chini ya miaka 14. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 5(1)&(2) wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini.

Swali la kujiuliza
Je, ni wangapi tunawaajiri watoto chini ya umri wa miaka 14 kufanya kazi za ndani?

Tatizo linaanzia hapo. Watu wengi wamekuwa wakiwaajiri watoto wadogo tena hata wenye umri wa miaka saba kama wafanyakazi wa kazi za ndani.

Wengi huogopa kuwaajiri watu wenye umri kuanzia miaka 18 au 14 kama inavyoruhusiwa kwa kazi nyepesi wakihofia pengine watajihusisha kimapenzi na wake zao au waume zao au watahitaji malipo makubwa na mambo mengine kadha wa kadha ambayo yanaonekana kuwa kero kwa waajiri wengi lakini ukweli ni kwamba ni uvunjifu wa sheria kumwajiri mtoto ambaye hajafikisha umri sahihi wa kuajiriwa unaoruhusiwa kisheria.

Kumwajiri mtoto chini ya umri unaoruhusiwa ni kosa kwani kunamnyima mtoto haki zake za msingi ikiwemo kukosa nafasi ya kupata elimu, ukuaji na ustawi wa mtoto.

Swali lingine
Je, ni wangapi mnawapa mkataba wa kazi hao wafanyakazi wa kazi za ndani?

Mfanyakazi wa kazi za ndani anahitaji kupewa mkataba wa kazi unaobainisha makubaliano na masharti ya kazi mazuri na yenye kueleweka kulingana na sheria, miongozo, kanuni na taratibu za nchi.
Kifungu cha 13 na 14 cha Sheria ya Ajira na Uhusino Kazini kinaweka hayo bayana takwa la kisheria la kuwepo kwa mkataba wa kazi kati ya mwajiri na mwajiriwa.

Mkataba wa kazi unatakiwa uoneshe
1. Jina la mwajiri na la mwajiriwa

2. Mahali pa kazi.

3. Aina ya kazi atakazotakiwa kufanywa.

4. Kiwango cha mshahara.

5. Masharti ya kuvunja mkataba kama mwajiri akitaka kumwachisha kazi mfanyakazi wake au kama mwajiriwa akitaka kuacha kazi.

Ni lazima pawepo na muda maalumu wa kutoa taarifa juu ya kuacha au kuachishwa kazi kazi ilivyo katika kazi nyingine kwa kuzingatia Sheria zetu za kazi.

Lakini wengi hawafanyi hivyo, utakuta mfanyakazi wa kazi za ndani anatoroka bila taarifa au mwajiri anamfukuza ghafra mfanyakazi wa ndani. Hiyo hairuhusiwi kisheria.

6. Mkataba pia uoneshe masaa ya kazi. Masaa ya kazi yasizidi masaa 12 kwa siku. Kifungu cha 19 cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini.

Mwajiri anatakiwa atambue kwamba kwa mfanyakazi wa ndani mwenye chini ya umri wa miaka 18 haruhusiwi kufanya kazi za usiku. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 20(2)(c) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini.

Wafanyakazi wa kazi za ndani hawatakiwi kutengwa wala kunyanyaswa kwa namna yoyote. Wanatakiwa kufanya kazi katika mazingira mazuri na waishi katika mazingira mazuri.

Pamoja na haki hizo lakini mfanyakazi wa ndani anatakiwa kuzingatia wajibu wake wa kazi ikiwemo na kufanya yafuatayo.
1. Kuipenda, kuiheshimu, kuijali na kuithamini kazi yake.

2.Kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa weredi mkubwa.

3.Kutunza siri za mwajiri wake.

4.Kumuheshimu mwajiri wake na familia kwa ujumla.

Kazi za ndani zinatamburika kisheria na wafanyakazi wa kazi za ndani wanalindwa kwa mujibu wa sheria za nchi na zile za kimataifa.

Muhimu sana kwa wafanyakazi wa kazi za ndani pamoja na waajiri wao kutambua na kuheshimu haki na wajibu wa kila mmoja kwa mujibu wa Sheria pamoja na kuzingatia utu na tamaduni zetu.

Ahsante kwa kuwa nami katika mada hii. MUNGU akubariki sana.

It's Me Mr George Francis
Email: mr.georgefrancis21@gmail.com
 
Back
Top Bottom