SoC04 Hakuna Jambo Baya, Tafuta Jambo Chanya kwenye Hasi

SoC04 Hakuna Jambo Baya, Tafuta Jambo Chanya kwenye Hasi

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Jun 13, 2024
Posts
5
Reaction score
5
Hakuna Jambo Baya, Tafuta Jambo Chanya kwenye Hasi
Katika maisha ya watu hapa duniani kuna nyakati nyingi sana ambazo zinakuja kwenye maisha, nyakati hizi zimegawanyika katika namna kuu tatu, kwanza ni nyakati hasi, pili ni nyakati chanya na tatu ni nyakati ambazo zipo katikati yaani sio chanya wala hasi.

Nyakati chanya ni nyakati ambazo zinaleta furaha, faida au hata mambo mazuri; hizi ni nyakati ambazo zinaleta mabadiliko nyanya kwenye maisha ya mtu, zinamtoa mtu katika hali moja kwenda nyingine. Mfano mtu akipandishwa cheo anakuwa katika furaha kuu na huu ni wakati chanya kwake, mwanafunzi akifaulu mtihani au akipata alama za juu inakuwa ni wakati nyanya kwake.

Nyakati hasi ni zile ambazo zinakuja na maumivu au kumshusha mtu kutoka hali moja kwenda hali ya chini. Hapa ndipo mtu hupatwa na huzuni, mfadhaiko na hatimaye matatizo katika maisha yake. Mfano mtu akipata ajali ambayo itamsababishia kukaa hospitali muda mrefu na kufanya mambo yake kushindwa kwenda inavyotakiwa au hata kuathiri maendeleo yake na familia. Hizi ni nyakati ambazo mwanafunzi anapewa taarifa kwamba ameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu amepata alama za chini, hizi ni nyakati ambazo mama aliyekuwa anajifungua baada ya kulea ujauzito kwa miezi tisa au zaidi ameambiwa kuwa mtoto wako amepoteza maisha ple sana, hizi ni nyakati ambazo mtuhumiwa anasikia sauti ya hakimu kwamba anahukumiwa miaka kadhaa jela kwa kosa fulani.

Nyakati za katikati ni zile ambazo zinakuja bila faida wala hasara katika moja ya nyimbo zake Farid Kubanda maarufu Fid Q amewahi kusema, “Baya lisilokudhuru ni jema lisilo na faida” kwa tafsiri isiyo ya moja kwa moja ni kwamba lipo jambo linakuja kwenye maisha yako linakuwa halina faida wala halina hasara. Mfano kumjua aliyetengeneza pesa hakukufanyi uwe nazo au usiwe nazo.

Mambo yote haya yanatokea kwa sababu maalumu, yaani hakuna namna ambayo mtu atakutana na mambo mazuri tu au chanya tu, la hasha! Bali atakutana na nyakati hasi pamoja na za katikati ila tatizo linakuja namna ya kukabiliana na nyakati hizi. Nyakati hizi zinaweza kumkumba mtu kwenye kazi yake, biashara, elimu, ndoa na kwingine ila namna ya kukabiliana na hizi nyakati ndo inakuwa changamoto.

Kwa mujibu wa nadharia ya “Relativism” ambayo ilibuniwa na Mfizikia Albert Einstein (1905)ni kwamba mambo yote ni ya kweli na mambo yote ni uongo ila tu inategemea na vile unavyolichukulia jambo. Hii ina maana kwamba ili jambo hasi lionekane hasi inategemeana na vile wewe unavyotafsiri, kadhalika kwa jambo chanya. Kwenye nadharia hii nitajikita hasa kuzungumzia nyakati hasi na chanya kwa sababu ndizo ambazo zinaleta matokeo fulani ima hasi au chanya.

Umewahi kujiuliza kwa nini ukitokea msiba kuna wengine wanalia na wengine wanafurahi? Wanaolia ni ndugu, jamaa na marafiki wa karibu lakini wanaofurahi ni wanaouza majeneza, sanda na wanaotoa huduma za mazishi. Ukipata changamoto ya afya ndipo utajua kwa mmiliki wa hospitali ni kicheko na kwako ni huzuni, hii ndio maana halisi ya kupata maana ya kitu kutokana na tafsiri yako mwenyewe. Mfano mwingine ni huu; wakati nikiwa kijijini kipindi hicho hakukuwa na umeme na nyumba zetu nyingi vyoo vilikuwa ni nje ya nyumba hivyo ukibanwa na haja usiku unatoka nje sasa kwa sababu ya hofu unaanza kutengeneza maadui wako wewe mwenyewe kutokana na mizigo au vitu au miti unayoiona kisha unatengeneza suta ya mtu na badae unaanza kumpa mijongeo kwamaba anakufuata lakini kumbe ni picha za hofu kisha baada ya kumaliza haja zako unatoka haraka ukiamini anakufuata kisha unaingia ndani na kubamiza mlango, kumbe ni hofu na namna umetazama vitu.

Matatizo au nyakati hasi tulizonazo ni matokeo ya tafsiri zetu wenyewe hivyo tunaweza kukabiliana nazo hizi nyakati kuanzia kwetu wenyewe (ndani) kuliko kuzipa nafasi ya kutushinda na kisha kutudhoofisha au kutupunguza mwendo, tuna uwezo wa kugeuza matatizo au changamoto kuwa fursa kwa sababu hakuna namna kwamba matatizo au changamoto au shida zitaisha kabisa hapa chini ya jua kwa sababu hizi zipo ili kutengeneza fursa kwa wengine.

Wezi tunawachukia kwa sababu wanatuibia ila wao ni moja ya kinachofanya askari wa jeshi la polisi wawe na kazi ya kufanya na wapate mishahara walishe familia zao. Hatuzipendi kesi lakini ndizo zinafanya mawakili wanaishi na hiyo kada ipo vyuoni na wakufunzi wanafanya kazi ili kujipatia kipato, tunachukia dhambi ila ndizo zinafanya kila uchwao viongozi wa dini wanatoa mahubiri na ndilo jukumu wamepewa na Mwenyezi Mungu.

Ninaamini kwamba ubaya na wema, nyakati hasi na chanya zote ni sawa tu ila inategemeana na namna unavyotafsiri. Mfano kwa mujibu wa mwanafalsafa Plato maadili ni jambo ambalo sio la pamoja au wote maana yake kilicho sawa kwako huenda kikawa sio sawa kwa wengine, hivyo tafsiri ya jambo ndio inaamua hilo jambo kuwa ni baya au zuri.

Hitimisho
Namalizia kwa kusema ukipatwa na changamoto yoyote ili isikuletee shida jitahidi kuifasiri katika namna chanya ili ikupe akili ya kugundua jema kwenye hilo baya. Ukiibiwa simu amini kwamba hiyo simu sio saizi yako hivyo umeibiwa ili ununue kubwa au ya thamani zaidi ya hiyo. Ukiachwa na mpenzi/mke au mume ukilichukulia ni tatizo basi utaumia au hata kufa ila ukiamini kwamba huyu hakuwa mtu sahihi kwenye maisha yako maana yake utajiona ni mtu mwenye faida na utaamini unahitaji kilicho bora zaidi kadhalika na kwa mambo mengine.
 
Upvote 5
Back
Top Bottom