SoC01 Hakuna linalokushinda, ni uamuzi wako tu kufanya au kutokufanya

SoC01 Hakuna linalokushinda, ni uamuzi wako tu kufanya au kutokufanya

Stories of Change - 2021 Competition

iam_jovin_geofrey

New Member
Joined
Jul 16, 2021
Posts
1
Reaction score
0
Na JOVIN Geofrey

Ukimuona, hutaamini! Muonekano wake na anachokifanya vinastaajabisha, kuvutia na vinadhihirisha kuwa hakuna kinachoshindikana ukidhamiria. Ukimuona, utaamini kuwa hakuna mipaka wala aina katika ugunduzi wa fursa. Ni binti mrembo, mwenye tabasamu zuri, macho ya kubembeleza na rangi isiyoumiza macho umtazamapo.

Anavyoandika kwa kasi na ustadi, ukisoma kazi zake hutaamini kama ameandika kwa kutumia ulimi. Hisia za kuwa na nguvu, uwezo, hamasa na kutokata tamaa hunijaa kila nikimkumbuka. Ni mrembo aliyepooza kuanzia mabegani hadi unyayoni, ni shingo na kichwa tu ndio vinavyofanya kazi mwilini wake. Hakika anachokifanya ni mfano bora wa kuigwa.

Kupooza hakukumkatisha tamaa juu ya kipaji chake cha uandishi, kulimpa ubunifu na uchu wa kupambana kutimiza ndoto yake. Alipoona mikono yake haiwezi kuandika, aliamua kutumia ulimi. Nikitafakari ugumu wa kuandika katika simu kwa kutumia ulimi kiukweli sipati picha ni mateso kiasi gani anapitia. Namna shingo, mifupa na macho yanavyochoka na kuumia, ulimi unavyohangaika wakati wa kuandika huku mate yakimjaa mdomoni kila sekunde, hakika anastahili tuzo na mafanikio anayoyapata tena na zaidi.

Amenifunza kukitumia kipaji changu ipasavyo, kuwa na nidhamu, ubunifu na uvumilivu hata katika kipindi kigumu. Amenifunza mengi kuhusu ‘maana ya fursa, maeneo fursa zilipo na namna ya kuzitumia kikazi’, vitu ambavyo ni changamoto kwetu na vinachangia kutukosesha kazi/ajira, japo wengi hatujavishtukia kwani tunaishi kama vile tunafahamu usahihi wa mambo kiutendaji, ilhali hatufahamu.

Maana ya fursa; ni nafasi ya kufanya au kuonyesha kitu anayoigundua au kuipata mtu inayomuwezesha kujifunza, kukua na kupata maendeleo. Nimeandika “anayoigundua au kuipata mtu”, hivyo, ili uwe na fursa, ni lazima uigundue au uipate, kama mrembo hapo juu alivyogundua uandishi kwa kutumia ulimi. Sasa tuachane na kupata, kwani kupata ni matokeo ya nje tusio na uamuzi nayo moja kwa moja, mfano; kuajiriwa ni fursa tusioweza kuamua moja kwa moja kuipata hadi tusubiri uamuzi wa waajiri. Tuangalie hapa katika kugundua ambapo ni matokeo ya ndani na sisi ndio waamuzi wa moja kwa moja.

Ugunduzi hutokana na mtazamo wa mtu, unavyotazama kitu kwa namna yako ndio hukufanya ugundue chochote. Utofauti wa mitazamo yetu ndio hutupelekea kugundua au kutogundua fursa katika tunavyoviona. Mfano; katika kutazama gari nyingi, mmoja kwa mtazamo wake ‘anaweza kuona biashara ya kuosha magari’, mwingine ‘anaweza kuona tu jinsi gari hizo zilivyo nzuri’.

Hivyo ndivo mitazamo yetu hutofautiana na kutofautisha ugunduzi wetu wa fursa. Katika hali hiyo wasioona fursa ndio wale huishia kusema “oi mwanangu, ukiona fursa pande hizo unishtue”, hawajui kuwa hata pale walipo kuna fursa zinazowafaa. Hemu jaribu kujiweka katika nafasi ya huyo mrembo hapo juu, uwe ndio umepooza mwili, je, ungeweza fikiri juu ya fursa unazoweza gundua na kuzifanyia kazi? Wangapi umewaona au kusikia wakikata tamaa angali ni wazima wa afya? Bila shaka umenielewa.

Maeneo fursa zilipo (sehemu za kuzigundua); Hapa ndipo shughuli inapoanzia sasa, wengi hudhani kuna maeneo maalumu ambako fursa hupatikana, hii si sahihi. Fursa ziko kila eneo na katika kila kitu, inategemea tu na mtazamo wako katika unayoyaona na unachoweza kugundua katika hayo. Binafsi nimekuandalia maeneo/vitu kumi ambavyo fursa nyingi hugundulika huko popote utakapokuwa.

Eneo/kitu 1 ni Kipaji; huu ni ujuzi asilia wa kufanya kitu ambao Mungu amembariki kila mtu. Hakuna binadamu asiye na kipaji na mtu mmoja anaweza kuwa na vipaji vingi, vipaji pia viko katika aina nyingi. Kipaji ni fursa inayoweza kumpatia mtu kazi/ajira, ila jambo la msingi halipo katika kipaji pekee, lipo katika ugunduzi wa namna ya kukitumia kikazi. Wengi hawajui vipaji walivyonavyo na wanaovijua hawajui namna ya kuvitumia kikazi. Anza leo kupambana kuyafahamu hayo ili vipaji vyako viwe kazi/ajira zako za uhakika.

2 ni Kitu unachokipenda/kinachokuvutia; hiki ni fursa ya kazi/ajira unayoweza kuitumia, kagua vitu unavyovipenda/vinavyokuvutia sana bila kujali ni vitu gani au vikoje. Inawezekana vinapatikana ndani yako, kwa watu wengine au katika mazingira yaliyokuzunguka. Kupitia hivyo unaweza kupata kazi inayokufaa. Naamini kazi kama za u-Dj, udereva na upigaji picha, watu walizigundua katika vitu wanavyovipenda au vinavyowavutia. Usiseme fursa hazipo wakati kuna vingi unavipenda/vinakuvutia, tafuta kimoja/viwili uvifanye kuwa kazi yako.

3 ni Uhitaji uliopo katika jamii; jamii zetu zina mahitaji mengi ya namna tofauti. Kuna mahitaji asilia/lazima, mfano chakula, mavazi, malazi, matibabu na elimu. Kuna mahitaji ya kutengenezwa/yasiyo ya lazima, ‘kutengenezwa’ inamaanisha jamii inakuwa haifahamu uwepo na matumizi ya kitu fulani, lakini mtu/watu wanatengeneza/wanabuni kitu na kukifanya kionekane ni hitaji la muhimu. Mfano; mitandao ya kijamii, vinywaji vitamu, pipi na biskuti. Kwa hivyo, unaweza kutumia uhitaji uliopo katika jamii kugundua fursa za kazi.

4 ni Matatizo yaliyopo katika jamii; imesemwa “mtu anaetatua tatizo ndie anaetajirika”, yaani mafanikio/utajiri umejificha katika matatizo. Wote tunajua mafanikio/utajiri wanaopata watu wanaotatua matatizo ya uongozi, maji, mawasiliano, elimu na magonjwa. Watu kama Mwl. Nyerere, Reginald Mengi, Rebecca Gyumi, Anthony Luvanda na Jovin Geofrey. Umeshangaa kuona jina langu! Hahaa nami nimo, utanielewa nitakapofanikiwa zaidi. Wingi wa matatizo katika jamii zetu ndio wingi wa fursa, hapo ulipo jamii yako ina matatizo mengi, hivyo hakuna ulazima wa kwenda kwingine, anzia hapo kwa kutatua tatizo moja au mawili, nina uhakika yatakupa kazi na baadae mafanikio/utajiri.

5 ni Rasilimali zilizopo; ardhi, maji, mimea, watu, madini, muda na zingine uzijuazo, zote ni fursa. Kupitia hizo watu wamefungua kampuni/biashara za uuzaji mbao, viwanja vya michezo, kumbi za burudani, shule/vyuo, viwanda, nk. Wewe unazitumiaje rasilimali hizi? Au unataka kutuaminisha unakoishi hazipo! Aah sio kweli, acha mambo yako bhana, changamkia fursa hizi, au unadhani huwezi kumiliki kampuni/kiwanda, nk, UNAWEZA, kama fursa za aina hii zinakufaa, gundua moja/mbili ufanye.

6 ni Shughuli za watu; gereji huanzishwa kwa kuwa kuna shughuli za utengenezaji wa vyombo vya moto, kunakuwa na makocha/walimu/washauri kwa kuwa watu hushughulika katika tasnia mbalimbali. Hivi ndivo mambo yalivyo, yani shughuli za watu huwa fursa kwa wengine pia. Hapa mtu hutulia kugundua bidhaa au huduma inayoweza kuhitajika kwa mtu/watu wanaofanya shughuli fulani, hivyo usiwashangae au kuwatamani, jiulize unaweza gundua fursa gani kupitia shughuli zao.

7 ni Vitu wanavyopenda watu; watu tunapenda vitu vingi, mfano muziki, filamu, michezo, kupendeza, kujulikana, kufurahi, kuongea, umbea na vingine vingi kinyama yani. Usiniambie katika vyote hivi hakuna fursa hata moja inayokufaa hapo ulipo. Umeshawaona wanaopaka rangi kucha za wanawake, wanachotumia ni fursa ya kupenda kupendeza kwa wanawake, sasa wewe baki kuwashangaa/kuwadharau wakati wao wanapiga pesa, siku ukikuta wamefungua kampuni usianze kusema “ooh jamaa ana mkono wa biashara au sijui ana nyota”, HAKUNA, watu wanagundua na kutumia fursa vizuri.

8 ni Ujuzi/Utaalamu na uzoefu ulionao katika kitu fulani; kuna watu ni wataalamu/wajuzi/wazoefu lakini hawana hata habari kama ujuzi, utaalamu au uzoefu huo unaweza kuwa kazi/ajira. Unakuta mtu ni mjuzi wa kusuluhisha migogoro, kila mgogoro ukitokea mtaa mzima wanamtafuta yeye asuluhishe, lakini kazubaa bila kazi utafikiri hakuna anachoweza kufanya duniani hapa. Jichunguze vizuri katika eneo hili, usije kufa maskini angali una ujuzi/utaalamu au uzoefu.

9 ni Ujuzi/utaalamu wa watu wengine; tunaishi katika mchanganyiko na mgawanyo wa sifa ndani yetu. Kuna wasioweza unachofanya na usioweza wanachofanya, kila mmoja anaweza kutumia ujuzi/utaalamu wa wengine kama fursa kwake. Ukiona watu wataalamu katika ususi, fungua saluni waajiri, ukikutana na wajuzi wa kuimba, fungua studio warekodi nyimbo kwako, hata ukiona wataalamu wa kupiga mbonji a.k.a kulala, fungua kituo cha kulala kama kile cha Nyerere Square Dodoma pale. Mwisho wa siku hakikisha hupitwi na fursa zinazotokana na ujuzi/utaalamu wa watu kama hili eneo linakufaa.

10 ni Mapungufu/Maboresho ya bidhaa/huduma za watu; bila shaka wanaochapisha/kuchora tisheti, wanaopaka/kubadili rangi za nyumba/gari/viatu, wanaoshona/kubadili vitambaa kuwa nguo na wanaohariri makala/vitabu na kazi za sauti/video na wengine sampuli hii, waligeuza mapungufu au maboresho ya bidhaa/huduma za watu kuwa fursa kwao. Wewe unayatumia vipi mapungufu au maboresho unayoona yanaweza kufanyika katika bidhaa/huduma za watu!? Kama panakufaa hapa, patumie.

Jinsi ya kuzitumia fursa kikazi au kibiashara; umeelewa maana na maeneo fursa zilipo, hivyo punguza kupigia watu simu kuulizia fursa huko waliko, hapo ulipo fursa zipo pia. Sasa, changamoto ipo katika namna ya kuzitumia fursa na uwezo wa kuzitumia. Binafsi nitatilia mkazo vitu 3, japo wengi husema tatizo kubwa lipo katika kimojawapo ambacho ni mtaji, cha ajabu wengi wao hata wakipata mitaji wanayoililia huwa wanashindwa katika kazi/biashara wanazoanzisha.

1 ni Kutafuta Ujuzi/Maarifa; Jifunze zaidi kuhusu fursa uliyoigundua, unaweza kuanza kujifunza biashara, uchumi, mahusiano ya kikazi, stadi za maisha na usimamizi wa pesa. Kujifunza kupo kwa aina nyingi, unaweza kujifunza kupitia kusoma vitabu/makala, kusikiliza/kuangalia video za mafunzo pamoja na kushirikiana na watu waliofanikiwa katika maeneo hayo.

2 ni Kutafuta Mtaji; sasa katika mitaji hapa ndio huwa tunalia sana, huchelewi kusikia “mi mwanangu kila kitu nimeweka sawa, nasikilizia mtaji tu, nikiupata mambo yataenda freshi”. Kuna namna nyingi za kupata mitaji; kujiwekea akiba, kuomba misaada kwa watu wa karibu (wengi huomba hela za mambo mengine tu ila za mitaji hawaombi), kwa kukopa (kwa watu binafsi au taasisi za fedha) na kupitia ubia na wengine (business partnerships).

3 ni Kuyafanyia Kazi; yafanyie kazi, usipofanya hakuna kitakachobadilika maishani mwako. Usijali kuhusu kuanzia chini/kufeli, ili ufanikiwe utapitia huko, hivyo usiogope, anzia ulipo na kwa hicho ulichonacho. Hapa ndio huhusisha sana ufanyaji wa maamuzi sahihi, nidhamu, kuvumilia changamoto, kuongeza juhudi, kutumia mbinu mpya au ubunifu na mengine sampuli hiyo. Kumbuka hakuna linalokushinda, ni uamuzi wako tu kufanya au kutokufanya. Nakutakia ugunduzi na utumiaji mzuri wa FURSA na MUNGU akubariki.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom