kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,677
Mpambanaji wa mgombea binafsi Christopher Mtikila
Wapenda demokrasia hawataweza kumsahau Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Christopher Mtikila katika harakati zake za kuona demokrasia inafikia kileleni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Moja ya haki aliyopigania Mtikila ni mgombea binafsi katika uchaguzi. Katiba ya sasa inazuia haki hiyo.
Mwaka 1993 Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma akiiomba mahakama iruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi kwa msingi wahoja kwamba ni haki za kiraia za kuchagua na kuchaguliwa bila kushurutishwa kupitia mlango wa vyama vya siasa.
Katika hukumu ya Mahakama Kuuya Oktoba 24 mwaka 1994, Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, Jaji Kahwa Rugakingira ambaye sasa ni marehemu alisema ni haki kuwapo kwa mgombea binafsi.
Serikali haikupendezwa na uamuzi wa mahakama na ikaamua kupinga kwa kukata rufaa Mahakama ya rufaa.
Kwa mshangao wa wengi Serikalihiyo hiyo ikaamua kutumia njia ya mkato pale Bunge lilipotunga sheria ya kulazimisha raia wa Tanzani anayetaka kugombea katika uchaguzi wa dola lazima awe mwanachama wa chama cha siasa!
Hatimaye Bunge likafanya marekebisho. Ibara ya 34 ya mwaka 1994 ya mabadiliko ya 11 ya Katiba yakazuia mgombea binafsi kugombea nafasi za Urais,Ubunge na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Haikuwa dawa wala haikuwa sababu ya kumkatisha tamaa Mtikila kwani Februari 17, 2005 alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho Katiba ya mwaka 1994.
Katika kesi hiyo alikuwa akiiombaMahakama hiyo pamoja na mambo mengine, iamuru kuwapo kwa mgombe binafsi.
Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo katika hukumu yao ya Mei 5 mwaka 2006 walikubaliana na hoja za Mtikila ya kuwa ni haki ya raia kuchagua na kuchaguliwa siyo lazima kupitia Chama cha siasa.
Baada ya uamuzi huo, Serikali mbio Mahakamani, ikaenda kukataa rufaa katika Mahakama ya rufaa ya Tanzania kupinga hukumu ya Mahakama Kuu. Aprili8 mwaka 2010 Jopo la Majaji sabawa Mahakama ya rufaa wakasikiliza shauri hilo.
Jaji Mkuu wa Tanzania kwa wakati huo, Augustino Ramadhan aliongoza Jopo la Majaji hao ambao ni Nathalia Kimaro, Benard Luanda, Eusebio Munuo, Sauda Mjasiri, Januari Msofe na Mbarouk Mbarouk.
Mahakama ya rufaa katika hukumu yake hiyo ya Juni 16 ikatoa hukumu kwamba haina mamlaka ya kutengua ibara ya katiba!
Baada ya historia hiyo fupi sasa tuendelee na niliyokusudia leo kwa muktadha huo huo wa katiba mpya na haki ya mgombeabinafsi katika nafasi za uongozi wa dola.
Kwa wapenda haki na demokrasia hawatasita kuungana nami katika kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Warioba kupendekeza kuwapo kwa mgombea binafsi katika rasimu ya katiba mpya.
Nimesoma maoni mengi kuhusu kuandikwa kwa katiba mpya kupitia vyombo vya habari, suala moja ambalo linaonekana kutopewa uzito kwa waliotoa maoni kuhusu mgombea binafsi.
Ingawa wapo walioeleza, lakini hoja yenyewe inaonekana kupita kama upepo.
Tuunge mkono suala zima la mgombea binafsi litatufanya kutimiza matakwa halisi ya demokrasia iliyowazi kama wenzetu wanavyofanya katika mataifa yaliyoendelea na yenye misingi imara ya utawala bora.
Wapenda demokrasia na haki bado watakumbuka kuwa hata Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni miongoni mwa watu waliokuwa wakiunga mkono hoja ya kuwapo mgombea binafsi.
Mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi.
Hili jambo limekosewa ni la msingi.
Ndiyo maana napenda kulisema ni la msingi, linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura na kupigiwa kura. Hii ni haki ya uraia Alisema Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake mwaka 1995.
Hatujachelewa, tunaweza kupazasauti kuhusu mgombea binafsi na bila shaka kwa kuwa katiba tuitakayo ni katiba ya wananchi siyo watawala shime kila mmoja wetu aunge mkono kwa nguvu ya hoja mapendekezo ya Jaji Warioba katika eneo la mgombeabinafsi.
Kuwapo kwa mgombea binafsi itakuwa si jambo jipya ni sawa navyama vingi vya siasa, vilifutwa baada ya uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964,vikaja kurejeshwa tena mwaka 1992.
Na hili nalo litakuwa linarejeshwatena katika mfumo wa siasa za Tanzania. Itakumbukwa kuwa kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mgombea binafsi hakuwa amekatazwa kwa mujibu wa sheria na katiba.
Katiba ya Kwanza ya Tanganyika Constitution Order in Council 1961 haikuwa inakataza mgombea binafsi. Tanganyika ilipokuwa Jamhuri mwaka 1962 katiba yake haikukataza mgombea binafsi.
Mambo yalianza kubadilika baadaya Muungano wa Dola mbili huru,Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika zilipoamua kuungana na kuunda Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili mwaka 1964 ndiyo mambo yakaanza kuwa tafauti.
Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 ndiyo iliyofuta mfumo wa vyama vingi vya siasa na kutamka wazi kuwa mambo yote ya siasa katika Tanzania yatasimamiwa naTanganyika African Union(TANU) kwa upande wa Tanganyika na Afro Shiraz Party(ASP )kwa upande wa Zanzibar.
Nikiwarudisha nyuma kidogo mtaona kwamba Uchaguzi wa Agosti 8 mwaka 1960 huko Tanganyika kulikuwa na mgombea binafsi. Jumla ya wagombea 25 walijitokeza kuwania nafasi za uongozi, kati ya hao 11 walisimamishwa na TANU na walishinda.
Katika Jimbo la Mbulu, TANU mgombea wake Chifu Amri Dodo aliangukia pua baada ya kushindwa, aliyeshinda alikuwa ni mwanachama mwenzake wa TANU Herman Elias Sarwatt ambaye alikuwa mgombea binafsi.
Sarwatt alikuwa ni mwanachamawa TANU hivyo ushindi wake ulikinufaisha Chama hicho ijapokuwa alikatwa wakati wa mchakato wa kupitisha majina akidaiwa kutokuwa na mvuto kwa wapigakura, lakini matokeo yake yeye ndiye aliyeshinda na siyo mgombea aliyesimamishwa na Chama chake cha TANU.
Hapa kuna funzo kubwa linapatikana katika vyama vya siasa kupitia TANU. Hoja iliyotumiwa na TANU kumuenguaSarwatt ilikuwa dhaifu kwani mwisho wa siku ilidhihirika kuwamwanachama huyo anauzika katika soko la wapigakura kuliko aliyetakiwa na viongozi wa Chama(TANU).
Je, kama siyo haki ya mgombea binafsi, mwanasiasa huyu ambaye kwa sasa ni marehemu sihaki yake ingepotea? Bila shaka tunahitaji kulizingatia hilo tukielekea kwenye mabaraza ya katiba hapo baadaye.
Tujenge hoja ya ulazima wa kuwana mgombea binafsi katika uchaguzi kama ambavyo wananchi walivyojenga hoja ya kutaka mabadiliko katika muundo wa Muungano wakiamini kuwa mfumo utakaopatikana unaweza kuwa bora zaidi katika mazingira ya leo.
Ingawa hatuwezi kuepuka ukwelikwamba mfumo uliopo umetutumikia kwa miaka 49, lakini lazima pia tukubali ukweli wa mabadiliko ya dunia, mabadiliko ya Zanzibar na watu wake, mabadiliko ya Tanganyika na watu wake.
Mgombea binafsi anaweza pia kumaliza mivutano ya kisiasa au wananchi wasiopenda kujiunga na vyama vya siasa kuwa huru kusimamia nadharia zao na inawezekena ikapunguza lile jotola kushupaliana ndani ya vyama.
Hali ya sasa inayoendelea Zanzibar na Tanganyika inanikumbusha nyakati zile za mchakato wa wanamageuzi kutaka mfumo wa vyama vingi, walipingwa, wakaitwa kila aina ya majina, kisa kwanini wanatakamabadiliko ya mfumo wa siasa wa nchi yetu.
Katika maoni ya wananchi, asilimia 80 walisema tubaki na mfumo wa Chama kimoja, lakini ukiyachambua kwa kina utabaini kuwa walichokisema ni kile kile walichokuwa wanakitaka cha vyama vingi.
Nami nategemea kwamba hata hao Wahafidhina wa kale ambao wanasema Hapana mabadiliko baadhi ya wachambuzi wanasema ukiyapima katika mizania utaweza kubaini kuwa mawazo yao yamesheheni salamu za nyakati; kwamba wakati ni ukuta.
Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema "Inawezekana tatizo la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa kengele shingoni: Taabu ni kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo.
Na panya watakuwa wajinga sana wakidhani kuwa paka watajifunga au watafungana kengele shingoni!" Tusisubiri kuambiwa na watawala sisi wananchi wenyewe ndiyo wenye haki ya kuamua mfumo wa sheria ya nchi yetu uweje na katiba tunaitaka iwe katika sura gani, hivyo si kituko wala uasi ikiwa tutabariki mgombea binafsi, tuacheni unafiki katika siasa.
Tuache hulka za popo, tusimame katika ukweli katika mambo muhimu maana katika jamii, baadhi ya watu wanakuwa kama popo, ndumilakuwili kama ilivyosimuliwa katika kisa kimoja katika Ikulu ya Mfalme Louis XIV wa Ufaransa ya kale.
Siku moja Mfalme aliamua kwenda katika chumba cha ibadaakiwa na wasaidizi wake, alikutana na muhubiri Francois Fenelon peke yake. Mfalme Louis akauliza, Hii ina maana gani?
Fenelon akajibu, Mimi nilitangaza kwamba hutakuja kanisani leo, ili kwamba wewe Mheshimiwa uweze kujionea mwenyewe wale wanaomtumikia Mungu kihalali na wale wanao mhadaa mfalme.
Mchakato wa kupata katiba mpyaulipoanza na hata hivi sasa unatusaidia kuwabaini wale wanaoitumikia Zanzibar na Tanganyika kwa dhati ya uzalendo wao kwa sababu ya hisia za utambulisho wa nchi na wale wanaomuhadaa mfalme mbele ya macho yake kwa kubembeleza vyeo.
Vimbwanga vyao havikuishia kwenye utoaji maoni hata kwenye mabaraza ya katiba, lakini pia viliendelea hata nje ya uwanja, wakasema mengi na matokeo yake kweli ikadhihirika.
Hii ndiyo misingi ya uhuru na demokrasia ambayo inakataza wananchi kunyimwa haki ya kutofautiana kimawazo.
Misingi hiyo pia inataka mamlakazote katika nchi kutambuwa na kudumisha demokrasia, uhuru nahaki za wananchi.
Aidha, matamko ya haki za binadamu zinasisitiza hakuna kikundi chochote cha wananchi kilichosusiwa uongozi wa nchi, ndiyo maana wananchi wote tumeambiwa na Rais Jakaya Kikwete tutoe maoni kwa uhuru bila kushurutishwa.
Basi tukiwa tukiyatafakari hayo tuungane pamoja pia katika kuona kwamba demokrasia inashamiri na kufikia kilele chake kwa kuandika katiba bora yenye kuweka misingi madhubuti katika Muungano wetu, haki za kiraia na masuala mengine.
Tuache tabia ya kukabana makoo, ya kushupaliana kwa sababu ya tofauti ya mawazo kwani itikadi na vyama vya siasa ni kama njia inayotumiwa na wanasiasa kutulaza usingizi wakitubembeleza kwa wimbo wa maslahi ya vyama kabla ya nchi.
Mwandishi wa makala haya ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu(PhD) katika siasa za kimataifa,Chuo Kikuu cha Central China Normal University.
CHANZO: NIPASHE