Makinda agusia ndoa ya Nassari, Halima Mdee
SUALA la ndoa kati ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) leo limeibukia bungeni baada ya Spika Anne Makinda kuwatania na kusababisha washangiliwe walipoinuka wakati mmoja wakitaka kuuliza maswali.
Mdee na Nassari walitaka kuuliza maswali ya nyongeza katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM) kuhusu mikataba isiyokuwa na tija iliyoingiwa kati ya wawekezaji wa mashamba 41 ya kahawa mkoani Kilimanjaro na Vyama vya Ushirika.
Baada ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe kulijibu akikiri kuwepo upungufu mkubwa katika uwekezaji huo, Mdee, Nassari pamoja na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe walisimama wakitaka kuuliza swali la nyongeza.
"Nassari na Mdee, lakini kwa kuwa hawajafunga ndoa, namuita Kiongozi wa Upinzani," alitania Spika Makinda na kusababisha kicheko na kushangilia kutoka kwa wabunge.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Halima alisema, sasa yupo tayari kufunga ndoa na Mbunge wa chama hicho wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
"Nafurahi kwamba Nassari hatimaye ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo," alisema Mdee wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha na Meru katika viwanja vya Leganga kusherehekea ushindi wa Chadema.
Alisema, yeye na chama chake walikuwa wamebanwa na kampeni za kuhakikisha Chadema inatwaa jimbo hilo ndiyo sababu hakujibu mara moja maombi ya Nassari ya kumwoa aliyoyatoa katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
"Naondoka kwenda Dar es Salaam kujiandaa kwa Mkutano ujao wa Bunge, kisha nitakwenda Dodoma ambako nitamsubiri Nassari na kwa pamoja tutafanya maandalizi," alisema Mdee huku akishangiliwa na hadhira hiyo huku wakiimba na kucheza katikati ya mvua iliyokuwa ikinyesha.
Mdee alisema ndoa kati ya wabunge hao wawili wa Chadema ni wazo zuri na itatangazwa sana na kuandika historia.
Alipoona anashambuliwa sana na wapinzani wake kuhusu useja wake katika kampeni hizo, Nassari hatimaye alitangaza kumwoa Mdee ambaye pia hajaolewa. Na katika moja ya mikutano ya hadhara, alisimama naye jukwaani kukampeni.
"Kuna viongozi wengi wa kidini Dodoma, ikiwa ni pamoja na ndani ya Bunge ambao watatushauri jinsi ya kulitimiza hili," alisema Mdee na kuongeza kwamba baba yake Joshua, Mchungaji Samuel Nassari alipata kusema, ‘mwanamke mzuri ni zawadi kutoka kwa Mungu'.
Hivi karibuni, Halima alikaririwa akisema kuwa, suala la yeye kuolewa na Nassari halipo, na kwamba, alizungumzia jambo hilo hadharani kwa utani tu wa kisiasa.