Walimu wa shule za sekondari tulioajiriwa mwaka 2025 na 2026 na tunaotumia Benki ya CRDB kupokea stahiki zetu, hususan fedha za kujikimu, tunakabiliwa na changamoto ya kucheleweshewa malipo yetu.
Katika orodha ya walimu tuliostahili kulipwa fedha hizo, walimu wanaotumia Benki ya NMB pekee ndio waliolipwa. Hadi sasa, zimepita wiki nne bila sisi tunaotumia CRDB kupokea fedha zetu. Tunapofuatilia suala hili kwa wahusika, badala ya kupata ufafanuzi wa kuridhisha, tumekuwa tukipokea majibu ya dharau.
Tulipowasilisha malalamiko yetu kwa Mwenyekiti wa CWT wa wilaya, tulipata majibu kwamba walimu wanaotumia NMB wamelipwa mapema kwa sababu benki hiyo ni ya serikali. Jambo hili linazua maswali: Je, kutumia benki nyingine kama CRDB ni kosa? Ikiwa walimu wanapaswa kutumia NMB pekee, kwa nini hilo lisielezwe wazi tangu mwanzo?
Tunaomba mamlaka husika zitoe ufafanuzi kuhusu sababu za kucheleweshwa kwa malipo yetu na kuhakikisha kuwa walimu wote wanaostahili wanapata fedha zao bila ubaguzi wa aina yoyote unaotokana na benki wanayotumia.
Vilevile, tunawaomba viongozi na watumishi wanaosimamia masuala ya malipo ya walimu watimize majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na heshima. Walimu wanapofuatilia stahiki zao, wanastahili kupata majibu yenye ufafanuzi na yanayoheshimu haki zao, badala ya kudharauliwa.
Tunaamini kuwa stahiki za walimu zinapaswa kulipwa kwa wakati na kwa haki, bila kujali benki wanayotumia kupokea fedha zao.