Ghazwat
JF-Expert Member
- Oct 4, 2015
- 23,718
- 66,267
Omog amekuwa katika mjadala huku wengi wakiamini ana nafasi ndogo ya kubaki Simba baada ya kuwa na taarifa kuwa uongozi unaonekana kutoridhishwa naye, na umeanza kusaka kocha mpya kimyakimya.
Katika mahojiano na Championi Jumatano, Hans Poppe amesema kwa kuwa alikuwa nje ya nchi, hakuwa ameshiriki mambo mengi ya Simba lakini haoni kama kuna ubaya Simba ikiamua kubadili kocha.
"Kama inawezekana kubadili kocha kwa ajili ya kupata matokeo sioni vibaya. Kocha anaajiriwa kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa matokeo bora.
"Kama kocha atakuwa ana matokeo mabaya au yasiyoridhisha, sioni kama kuna ubaya kumbadilisha eti kwa sababu ya hofu", alisema.
Alisema uongozi unapaswa kupima na kuangalia kwa kuwa suala hilo si katika kitengo chake na kama unaona inawezekana kubaki naye, au kubadilisha mambo kwa nia njema, yote ni mambo sahihi.
Kuhusiana na kikosi cha Simba kinavyocheza hadi kilipo sasa, Hans Poppe ambaye hapendi kumung'unya maneno amesema;
"Hatuna mwendelezo mzuri katika kikosi chetu. Leo unashinda saba kesho sare, nafikiri kuna tatizo la kufanyiwa kazi. Bado timu haijawa na muunganiko mzuri.
"Sasa hili ni jukumu la bechi la ufundi kutengeneza kikosi ambacho kinafanya vizuri katika kila idara".
Simba inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano na kushinda tatu huku ikiwa imetoa sare mbili.
Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na Omog kubaki au kuendelea huku baadhi ya mashabiki wa Simba wakitaka aondolewe.
Lakini wajuzi wa mambo ya soka wamekuwa wakisisitiza kuwa bado mapema kwa kocha mwenye kikosi kipana kupata uhakika wa mambo na Simba wanapaswa kuwa wavumilivu angalau kwa mechi tano zijazo.
Tayari imepachika mabao 14 na kuruhusu matatu katika mechi hizo tano.
Chanzo: Championi