Harakati za Waingereza kukuza Kiswahili

Harakati za Waingereza kukuza Kiswahili

Mphamvu

JF-Expert Member
Joined
Jan 28, 2011
Posts
10,702
Reaction score
3,319
Waingereza walipochukua koloni la Tanganyika kutoka kwa Wajerumani, walikuta Kiswahili kimeimarika na kutumika katika utawala na maeneo mengine.

Kwa kuwa nao walihitaji kutawala hivyo hawakupuuzia matumizi ya Kiswahili, japo hawakutumia Kiswahili kwa lengo la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila ya wao kukusudia.

Shuguli za kiuchumi

Shuguli za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa kilimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua hao walijulikana kama manamba.

Katika mkusanyiko wa vibarua hawa waliokuwa wanatoka katika makabila tofautitofauti, lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha ni Kiswahili ambacho tayari kilikuwa kimeteuliwa kuwa lugha rasmi katika mawasiliano ya kiutawala.

Shuguli za kiutamaduni

Shughuli hizi ni kama vile uigizaji wa tamthiliya za kigeni, uchezaji wa muziki wa kigeni hususan twisti. Nyimbo hizo zilitungwa kwa lugha ya Kiswahili nchini Kenya na Tanzania. Pia tamthiliya za kigeni zilikuwa zikiigizwa majukwaani kwa lugha ya Kiswahili na hivyo ikasaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili.

Shughuli za kidini

Wakati wa utawala wa Mwingereza pia kuliambatana na ujio wa wamisionari waliokuwa na lengo la kueneza dini ya Kikristo. Kupitia mafundisho hayo yaliyokuwa yanatolewa kwa lugha ya Kiswahili kulisababisha kukua na kuenea lugha ya Kiswahili katika maeneo mengi ya nchi waliyolenga kueneza dini ya Ukristo.

Pia shughuli za kidini zilichangia kutafsiriwa kwa vitabu mbalimbali vya kidini kama vile Biblia na vitabu vingine. Tafsiri ya vitabu hivi ilikuwa ni kutoka katika lugha ya Kiingereza kwenda katika lugha ya Kiswahili.

Kwa kufanya hivvyo Kiswahili kiliweza kuongeza misamiati mingi zaidi na hivyo kuwezesha kukuza lugha ya Kiswahili.
Wamisionari walilazimika kujifunza Kiswahili hukohuko kwao ili wanapokuja huku Afrika Mashariki wasipate shida kujifunza Kiswahili.
Kwa sababu hiyo wamisionari waliokuwa wamejifunza lugha ya Kiswahili walitunga kamusi za Kiswahili – Kiingereza ili kuwasaidia wenzao pia kujifunza Kiswahili; kwa njia hii waliweza kukikuza Kiswahili.

Shughuli za kisiasa

Pia kutokana na uanzishwaji wa vyombo mbalimbali vya kiutawala, jeshi, polisi na mahakama. Kufuatia uanzishwaji wa vyombo hivi misamiati ya Kiswahili iliongezeka hivyo kukuza Kiswahili.
Vilevile kampuni za uchapishaji zilianzishwa kama vile East African literature Bureau na kuundwa kwa kamati ya lugha (Interterritorian language committee). Hatua hii iliimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili hatua iliyosaidia kukua kwa lugha ya Kiswahili.

Shuguli za ujenzi

Waingereza walishughulika na ujenzi wa barabara na reli kama nyenzo zilizowasaidia kuunganisha miji ambayo walifanya shughuli zao hasa kilimo. Shughuli hizi pia zilisaidia kuibuka kwa msamiati mpya kama vile, reli, stesheni, tiketi.

Mwananchi
 
Back
Top Bottom