Hasira na makwazo huondoa vilemba vya wema na busara feki tunazojivika

Hasira na makwazo huondoa vilemba vya wema na busara feki tunazojivika

Kipangaspecial

JF-Expert Member
Joined
Mar 30, 2020
Posts
20,778
Reaction score
28,722
Unapomhitaji mtu awezeshe jambo lako, mtu unayemwona ni raslimali ya ufumbuzi wa tatizo lako, unaweza kulazimika kuwa na sura ya uungwana bandia. Mshunuzi Carl Jung aliuita uungwana huu persona—tabia tunazojitambulisha nazo mbele ya watu tunaowahitaji kama nyenzo ya mahusiano—mfano tabasamu, ucheshi, ushika dini, sadaka zinazotangazwa, uungwana kwa bosi, kumwachia nyumba mtu unayejua atakusaidia kufikia malengo yako na kadhalika.

Persona huficha tabia fulani fulani tunazojua hazikubaliki katika jamii zinazoweza kutuharibia heshima mbele za watu tukadharaulika na kuonekana ‘watu wa hovyo’—mfano ubinafsi, kiburi, dharau, ulaghai, ubazazi, uchu wa madaraka, upendeleo wa kikabila na kadhalika. Carl Jung aliziita tabia hizi shadow, kwa vile huwa hatuzijui kama unazo na hata tukizijua tunazidhibiti mithili ya zimwi tunalolificha kwenye chupa lisituponyoke tukadhalilika.

Hata hivyo, kuna mazingira hufunua tabia hizi tusizotaka kujitambulisha nazo. Mfano, unapokuwa umekasirika, ule unyama ukiojificha ndani yako unakuponyoka. Unapokutana na mtu unayefikiri humhitaji, hana hadhi wala nafasi ya kukusaidia, mtu mliyetofautiana na unahisi huhitaji tena heshima yake, nguvu unayotumia kulidhibiti zimwi lako inapungua. Ule uhalisia unaonekana kirahisi.

Uungwana wako, wema wako, utu wako huonekana vizuri ukikasirika au ukishajua mtu hana msaada wowote na wewe. Maneno unayochagua kumsema mtu aliyekukatisha tamaa, uliyegombana naye, maneno unayosema unapokuwa na hasira, unapomjibu mhudumu wa mgahawa, mlinzi wa geti, yanakutambulisha vizuri zaidi kuliko vile unavyomtendea mtu mnayeheshimiana, unayempenda na kumhitaji. Ukitaka kuchagua kiongozi mwadilifu, mchumba mwenye utu au rafiki mwuungwana, chunguza anapokasirika, anavyowasema wabaya wake au anavyowatendea watu asiowahitaji.

Na Bwaya wa X
 
Back
Top Bottom