Hatua hii ya Chuo cha Polisi inapaswa kuungwa mkono

Hatua hii ya Chuo cha Polisi inapaswa kuungwa mkono

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Katika toleo letu la leo ukurasa wa kwanza , tumechapisha habari yenye kichwa cha habari askari 117 wametimuliwa Polisi . Katika habari hiyo, imeelezwa kuwa, Chuo cha Taaluma na Mafunzo ya Polisi (MPA), kilichopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kimewatimua wanafunzi hao kwa kukosa sifa za kuendelea na mafunzo ya kijeshi baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu, utoro na matatizo ya kiafya.

Askari wanafunzi hao walikuwa waungane na wenzao wanaotarajiwa kuhitimu mafunzo ya awali ya polisi na uhamiaji, Julai 26, mwaka huu.

Kufukuzwa kwa wanafunzi hao wa Polisi, kunaashiria moja kwa moja namna menejimenti ya chuo hicho ilivyojipanga upya kupunguza wimbi la baadhi ya askari walioko kazini ambao wanalipaka matope jeshi hilo kutokana na kupotoka kimaadili kwa kutaka kujinufaisha kimaslahi.

Mkuu wa Chuo hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Matanga Mbushi, aliiambia NIPASHE katika mahojiano maalum kwamba, waliotimuliwa chuoni ni kati ya askari wanafunzi 3,189 waliokuwa wamesajiliwa kuanza mafunzo ya kijeshi chuoni hapo Oktoba 25, mwaka jana.

Kati yao askari hao, 115 ni wale wa Polisi na askari wawili wanatoka katika Idara ya Uhamiaji iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa dhati kabisa, tunapenda kuchukua nafasi hii kupongeza na kuunga mkono hatua hizo zilizochukuliwa na chuo hicho za kuwabaini wanafunzi hao hususan waliopatikana na makosa ya utovu wa nidhamu na utoro kabla ya kuhitimu mafunzo yao na kuingia kwenye ajira.

Kwa wale wanafunzi walioondolewa katika mafunzo hayo kutokana na matatizo ya kiafya, tunawapa pole kwa sababu hilo liko juu ya uwezo wao.

Tunapongeza na kuunga mkono hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba kama mchujo huo usingewabaini na wakaachwa kupenya katika ajira, kwa hakika wangeleta `majanga' na kulichafua Jeshi la Polisi nchini.
Sote tu mashuhuda namna baadhi ya walinzi hawa wa amani wamekuwa wakitajwa kuhusika katika matukio kadha wa kadha ya uhalifu.

Mathalani, inataka kuwa ni kawaida kusikia polisi wakishirikiana na wahalifu mbalimbali, kuwabambikia wananchi wasio na hatia kesi, kufichua taarifa za siri kwa watuhumiwa walizopewa na raia wema, kuiba vitu mbalimbali vya kidhibiti mahakamani na hata wengine kufanya vitendo vya uhalifu moja kwa moja, kutaja matukio machache.

Hatua iliyochukuliwa na chuo hicho kama ingekuwa inafanywa hivyo kila kundi la wanafunzi wanapoingia kuanza mafunzo ya upolisi, kwa hakika Jeshi letu la Polisi lisingekuwa linakumbwa na kashfa kama hizo.
Sisi tunaamini kwamba askari polisi wanaofanya vitendo hivyo, ni wale ambao tabia zao tangu walikotoka, zilikuwa mbaya na kwa sababu hawakuchujwa vyema wakati wa usaili wanapojiunga na jeshi hilo pamoja na wanapofanya mafunzo chuoni.

Kutokana na kutochujwa vyema vijana wanaofaa kufanya kazi hiyo nyeti, ndipo wale wenye tabia kama hiyo huendeleza kufanya maovu hata pale wanapokuwa tayari wameajiriwa ndani ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, pamoja na kukipongeza chuo hicho kwa hatua hiyo, tunalishauri pia Jeshi la Polisi liweke utaratibu wa kudumu wa kuwachuja askari wake wenye ajira wanaojihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu ikiwamo uhalifu.

Kwa kufanya hivyo, Jeshi letu la Polisi litabakiwa na askari waadilifu na wenye moyo wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yao.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom