SoC03 Hatujarithi mazingira kutoka kwa wazee wetu, tumeyaazima kutoka kwa watoto wetu

SoC03 Hatujarithi mazingira kutoka kwa wazee wetu, tumeyaazima kutoka kwa watoto wetu

Stories of Change - 2023 Competition

Missandei

Member
Joined
Apr 21, 2023
Posts
58
Reaction score
87
Mazingira ni jumla ya vitu vyote vinavyotuzunguka. Yanahusisha ardhi, misitu, vyanzo vya maji kama mito,maziwa na bahari, hewa na majengo. Hatuna budi kuhifadhi mazingira yetu kwa ustawi wetu na viumbe hai wengine, lakini pia kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kuhifadhi mazingira kunahusisha kuilinda misitu, ardhi, hewa na vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi.

Kuchagua bidhaa au huduma zilizojikita katika kutoa matumizi endelevu kunapunguza uchafuzi wa mazingira yetu.

Kuchagua bidhaa na huduma za aina hiyo ni muhimu hasa kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana kuuthibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na takataka za plastiki.

Takataka za plastiki zina sifa ya kutokuoza, badala yake hujirundika na baada ya muda mrefu huanza kujivunja vunja na kutengeneza vipande vipande vinavyosambaa katika hewa, ardhi na vyanzo vya maji na kufanya uchafuzi.

Chembe chembe ndogo kabisa za plastiki hizi husambaa katika hewa na kuingia katika miili ya binadamu kupitia hewa tunayovuta, maji au chakula na kusababisha matatizo kama kansa, mvurugiko wa homoni, ugumba nk.

Viumbe hai kama ndege na samaki hula vipande vya plastiki wakidhani ni chakula na mwisho huwasababishia vifo.

Takwimu za Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa zinasema zaidi ya tani milioni 380 za plastiki zinazalishwa kila mwaka duniani na chini ya 9% ya plastiki hizo ndizo zinazorejezwa, na baadhi ya ripoti zinasema 50% ya plastiki zinazotengenezwa ni kwa ajili ya matumizi ya mara moja tu.

Pia zaidi ya tani milioni 10 za plastiki zinatupwa baharini kila siku na kuhatarisha maisha ya viumbe hai waishio majini. Inakadiriwa kufikia mwaka 2050 bahari zetu zitakuwa na uzito mkubwa wa takataka za plastiki kuliko uzito wa samaki.

Mapendekezo
Kupunguza na kuacha kabisa kutumia bidhaa za plastiki zenye matumizi ya mara moja mfano vinywaji vya kwenye vyupa vya plastiki, vifungashio vya vyakula, mirija ya vinywaji nk.

Serikali kuhamasisha wananchi kujikita katika utumiaji wa bidhaa zinazopunguza uchafuzi wa mazingira mfano matumizi ya vichuja maji kwa ajili ya maji ya kunywa,

Pia matumizi ya nepi za kufua baada ya matumizi kwa ajili ya watoto wadogo badala ya zile za kutupa baada ya matumizi. Tunaweza kutumia hizi za kutupa pale inapobidi. Hatua hii itapunguza uchafuzu wa mazingira unaofanywa na takataka hizi.

Kutumia tena plastiki kwa matumizi mengine mara baada ya matumizi ya awali. Plastiki zisizofaa kwa matumizi mengine zitupwe panapostahili kwa ajili ya urejelezaji.

Ingawa urejelezaji wa plastiki siyo suluhisho kwa kuwa si taka zote za plastiki zinazoweza kurejezwa, bali ni baadhi. Pia kipande kimoja cha plastiki kinaweza kurejelezwa mara 2 hadi 3 kabla ya kuwa hakifai tena.

Na kadri plastiki inavyorejelezwa ndivyo ubora wake unavyopungua na kiwango cha sumu kinavyoongezeka hivyo kuhatarisha afya za watumiaji.

Si hivyo tu, urejelezaji wa plastiki unahitaji plastiki mpya kuchanganywa ili kutoa plastiki yenye viwango vinavyohitajika.

Hivyo basi ni wazi kuwa njia sahihi ya kumaliza tatizo la uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki ni kupunguza matumizi ya bidhaa za plastiki.

Takataka zinazooza kama mabaki ya chakula tunaweza kuzitengenezea mbolea hivyo kupunguza kiasi cha taka zinazohitaji kutupwa. Mbinu hii itazalisha mbolea ambayo itaongeza rutuba kwenye udongo.

Kupunguza matumizi ya vyombo vya moto kama magari na pikipiki kwa kuwa vinachafua mazingira kwa kutoa moshi, lakini pia tairi za vyombo hivi zinapojivunja vunja kutokana na msuguano kati yake na barabara, hutoa chembe chembe zinazochafua hewa.

Kuvuna maji ya mvua na kuyatumia kwa shughuli mbalimbali kama kilimo, matumizi ya nyumbani nk. Hili litapunguza madhara yaletwayo na mvua kubwa mfano mmomonyoko wa udongo na mafuriko. Tunaweza kuvuna maji ya mvua kwa kufunga mifumo ya kukusanya maji ya mvua wakati tunapojenga nyumba zetu.

Pia tutumie bidhaa zinazozalishwa katika mazingira yetu. Kama tukitumia bidhaa zilizozalishwa katika mazingira yetu tunakuwa tumetunza mazingira kuliko tunaponunua bidhaa zinazotoka mbali zilizofungashwa kwa vifungashio na kutumia usafiri kutufikia.

Vilevile kununua bidhaa iliyokwisha kutumika (mtumba) ni chaguo zuri kimazingira. Hivyo tuzipe bidhaa hizi vipaumbele kwakuwa zinatupa nafasi ya kutunza mazingira.

Pia tuepuke vitendo vya uchomaji wa mashamba na takataka visivyo vya lazima kwa kuwa vinachafua hewa kwa kutoa kemikali zenye sumu ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na mimea. Si hivyo tu kuchoma mashamba hupoteza rutuba ya udongo na kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Mwisho kabisa tuache kutupa takataka hovyo na kila mmoja awajibike kuweka mazingira yanayomzunguka katika hali nzuri.

Ni vyema tukatanguliza ustawi wa mazingira yetu katika kila tunachokifanya. Vilevile tuwafundishe watoto wetu kuishi kwa kufuata misingi hii. Napendekeza serikali kuanzisha programu za utunzaji mazingira katika shule zote za msingi hapa nchini ili kuongeza ufahamu na uwajibikaji katika kutunza mazingira.

Pia halmashauri za miji na majiji kote nchini kutoa elimu ya utunzaji mazingira sambamba na kuweka vihifadhi takataka vya aina tofauti sehemu za mikusanyiko vitakavyowezesha takataka kutupwa kulingana na asili yake.

Yaani, Takataka zenye asili ya kuoza na zilizolowana zitupwe kwenye kihifadhi takataka cha peke yake, Takataka zisizooza na kavu zitupwe kwenye kihifadhi takataka cha peke ake, Pia takataka hatari zihifadhiwe kwenye kihifadhi takataka cha peke yake. Utaratibu huo utarahisisha uchakataji wa takataka na kuokoa muda na nguvu kazi.

Heri ya Siku ya Mazingira!
 
Upvote 3
Nimefurahi kuwa wakwanza kupiga kura kwenye chapisho lako

Watu wanakwenda na sayansi na teknolojia mwishowe wanajikuta wako nje ya mstari wa asili/nature tizama watu wanakata miti wanaotesha ukuta, miti inapandwa ni ile miti mseto urefu futi tano
Kuna miti ya matunda inapotea taratibu achilia mbali miti mingine mbalimbali
 
Nimefurahi kuwa wakwanza kupiga kura kwenye chapisho lako

Watu wanakwenda na sayansi na teknolojia mwishowe wanajikuta wako nje ya mstari wa asili/nature tizama watu wanakata miti wanaotesha ukuta, miti inapandwa ni ile miti mseto urefu futi tano
Kuna miti ya matunda inapotea taratibu achilia mbali miti mingine mbalimbali
Ni wachache sana wanafikiri kama wewe
 
Back
Top Bottom