SoC02 Hatuwezi kufundisha kila kitu

SoC02 Hatuwezi kufundisha kila kitu

Stories of Change - 2022 Competition

Jade_

Senior Member
Joined
Apr 19, 2015
Posts
122
Reaction score
214
Maoni lukuki yanaendelea kutolewa na wadau (ikiwemo mimi) kuhusu mtaala mpya wa elimu unaolenga kuboresha watoto wanachojifunza shuleni. Wapo wanaosema watoto waanze kusoma masomo yenye mlengo wa umahiri tangia shule ya msingi. Mfano mtoto asome masomo ya sayansi na teknolojia tu tangia anapoanza shule na asisome mengine.

Kama ni ya ufundi au sanaa ni hayo tu. Kusudi kuu la shule ya msingi ni kumkadimishia mtoto dunia na dunia siyo maarifa ya somo moja. Hii ni pupa ya mzazi kutaka mtoto wake apate gawio la kipawa ambacho pengine hana. Watoto wachache mno mno ndiyo wanaweza kuwekwa kwenye mpango maalum wa masomo ya umahiri, wengi ni akili za kawaida tu.

Mtoto katika umri mdogo ataonekana anajua sana kuhesabu au kucheza mpira lakini je huko mbeleni ataendelea kubobea? Ataendelea kuwa bora kuliko wenzake? Na kama akibadilisha mawazo na asitake tena kufanya kile alichokuwa anasema anapenda itakuwaje?

Kuna wanaopendekeza masomo mbalimbali yaanzishwe kama ya kujifunza kusimba, uzalendo, maadili, ujasiriamali, nakadhalika. Tutafundisha nini na tutaacha nini? Nia ni nzuri lakini haiwezekani kufundisha watoto kila kitu hata wakikaa shuleni maisha yao yote.

Untitled226_20220815004206.png

Picha: Mzigo wa masomo mengi

Elimu yetu kwa sasa inalaumiwa haikutayarisha vijana kujitegemea na badala yake iliwaandaa kutegemea ajira kutoka serikalini. Ni kweli, wakati mtaala wa sasa unaandaliwa, kazi za serikalini na sekta binafsi za kiutawala zilikuwa bado hazijaelemewa na wingi wa wasomi wanaotabahari kuzifanya. Mambo yamebadilika na kupelekea somo sadikika la ujasiriamali livume.

Sawa basi. Somo la ujasiriamali limeanzishwa. Je mtaala wake utakuwaje? Watoto watafundishwa kusajili jina au alama za biashara? Kutengeneza sabuni? Batiki? Kupika keki? Je tuna uhakika wa nini kitakachohitajika huko mbeleni? Mambo yanabadilika sana na kadiri siku zinavyoenda kasi ya mabadiliko inaongezeka. Hatujui mambo yatakuwaje na kuhisi kwamba mambo yalivyo hivi sasa ndiyo yatakavyokuwa ni wendawazimu.

Hatuwezi kutabiri na ikitokea tukabahatisha aguzi mambo yatabadilika papo hapo. Tukifahamu dunia itakuwaje huko mbeleni kila mtu atafuata huo mwelekeo na kupelekea tatizo kama la sasa la wasomi wengi ajira chache. Mbadala bora ni mtoto kufahamu namna ya kutumia ubongo na kupanua mawazo ili awaze kukabiliana na changamoto yeyote. Sijasema mtoto afundishwe matatizo atakayokutana nayo na namna ya kuyatatua kama fomula ya hesabu bali nimesema mtoto afundishwe namna ya kutumia ubongo wake. Ajifunze kufanya hivi kwa matendo.

Binadamu anapata maarifa mapya kwa kuvumbua. Sayansi inayopigiwa debe kila kukicha ni uvumbuzi. Uvumbuzi ni kaida kuu ya maendeleo ya binadamu. Ni sawa na vinasaba vyetu. Ikiwa binadamu anajifunza kwa kuvumbua kwa nini isiwe mtoto? Mtoto akishika kitu kikamdhuru atavumbua sharti la kutogusa hicho kitu. Tunatakiwa tuwawezeshe watoto wajifunze kwa kuwaacha wavumbue kama alivyofanya na anavyoendelea kufanya binadamu. Mtoto akiweza kufanya hivyo yale anayojifunza hatasahau na ataweza kugundua mapya.

Elimu wanayoipata watoto shuleni imegawanyika kwenye mafunzo ya aina mbili.
1. Mafunzo yenye kutoa maelezo ya namna jambo lilivyo.
2. Mafunzo ya namna jambo linavyofanywa.

Shida kwenye elimu yetu inatokea pale mafunzo ya namna ya kufanya jambo (mafunzo ya vitendo) kutotiliwa mkazo kama yale mafunzo ya maelezo. Mafunzo ya vitendo ndipo mtoto atakapoweza kufanya vumbuzi. Uvumbuzi unatokea baada ya kuishi maisha ya kila siku. Madarasa yageuzwe mfano wa maisha ya kila siku ili mtoto aweze kutumia ubongo wake katika kutatua matatizo mbalimbali atakayokutana nayo.

Tusianzishe masomo ya kusimba, ujasiriamali nakadhalika badala yake tuweke vilabu za hizi shughuli kama sehemu ya elimu ya ziada. Itasaidia kumshughulisha mtoto apate uzoefu wa pande tofauti za maisha na shida anazoweza kukutana nazo. Mtoto akijaribu na akaweza kutatua shida ataongeza kujiamini na hataogopa atakachokutana nacho maishani. Ataelewa anaweza kukabiliana na chochote na hakuna shida isiyo na suluhisho.

Michezo mbalimbali iendelee kuwepo na iongezwe mashuleni. Shughuli nyingine za kisanaa, stadi za kazi ziwepo na muda wa kuandika “notes” na kukaa darasani upunguzwe. Namna ya kufanya elimu yetu iwe bora ni kuwapa watoto nafasi ya kuvumbua. Wavumbue wanachopenda, wanachoweza na nini wanachoona kinahitaji kuboreshwa na sio kuelezwa tu cha kufanya.

Mazoezi ya kusoma kuandika (kwa Kiswahili na Kiingereza) na kuhesabu yaongezeke maradufu. Najua wanafunzi wanafanyia mazoezi haya masomo lakini bado haitoshi, bahati mbaya kuna ripoti za wanafunzi kumaliza la saba hawajui kusoma wala kuandika. Muktadha wa kujifunza ubadilishwe na wanafunzi wapate uzoefu wa duniani kwa kutembelea na hata kufanya majaribio ya kupima uelewa wao kwenye maktaba za mikoa, masoko, stendi, viwanja vya ndege, makumbusho nakadhalika. Kujua kusoma na kuandika siyo kuzifahamu tu herufi bali ni namna ya kuweza kufahamu maana ya herufi na lugha kwa ujumla. Kujua kuhesabu siyo tu tarakimu, jumlisha na kutoa lakini je hesabu inatueleza nini? Hesabu inatabiri nini? Tutilie mkazo haya masomo, hata dunia ikibadilika bado itakuwepo katika msingi wa haya masomo. Kusoma kuandika na kuhesabu ni ujuzi wa nyakati.

Shule za sekondari zinazofundisha masomo tusiyoyazoea (mfano Moshi Technical iliyopo mkoani Kilimanjaro) ziongezwe na ziwepo za umahiri katika sanaa na michezo pia. Hapa nchini Tanzania tuna shida ya wahitimu wengi wa aina moja na kutokuwa na tofauti inayojitosheleza ili kukidhi sekta nyingine. Tusizoee tu masomo ya uzoefu tuweke na ya ujuzi. Tutapata watu wenye uwezo wa aina nyingi na si tu wahitimu wengi wa aina moja.

Mabadiliko ya kielimu hayatatokea kwa mara moja, yatachukua muda mrefu. Yakifanyika hayatakamilika na inabidi tuendelee kuboresha kidogokidogo kadiri dunia na binadamu anavyoendelea kubadilika na anavyogundua na kupata maarifa mapya. Kiufupi mtaala wetu hautakaa uwe timamu na tusipende kujilaumu sana kwa mapungufu tutakayoyaona.


Viambatisho:
MTAALA WA ELIMU YA MSINGI DARASA LA I–VII
MWONGOZO WA MWALIMU WA KUFUNDISHIA ELIMU YA AWALI
MIHTASARI YA MASOMO YA ELIMU YA SEKONDARI-KIDATO CHA I-IV
 
Upvote 2
Karibuni kwa tafakuri, maswali au kutoa maoni ili tusaidie elimu yetu isonge mbele.
 
Somo ninaloona liwe la lazima tangia shule ya msingi ni namna ya kutumia kompyuta. Kompyuta ni kama penseli au kalamu, matumizi yake hayakwepeki.
 
Naendelea na tafakuri. Hapo kwenye kutafuta njia nyingine ya kufanya mitihani na kupima uwajibikaji wa walimu. Kwani lazima mitihani ifanywe darasani au kwa kuandika tu? Tukipata namna mbadala itasaidia kuboresha elimu yetu na kuwekeza nguvu zaidi katika kufanikisha uvumbuzi kwa watoto. Namna mbadala itaondoa shinikizo la kukariri kwa ajili ya mitihani.
 
Kama ukipenda andiko langu usiache kulipigia kura na kutoa maoni au maswali.
 
Back
Top Bottom