Hawa ndio 'wagalatia' waliologwa! Tena, tuone jinsi wanavyologwa. (gal 3:1)

Hawa ndio 'wagalatia' waliologwa! Tena, tuone jinsi wanavyologwa. (gal 3:1)

Raphael Mtui

Member
Joined
Nov 26, 2024
Posts
78
Reaction score
204
Katika dunia ya leo, tuna swali kubwa kuhusu watu wanavyodanganywa KIRAHISI na manabii wa uongo ambao hapahitajiki akili yoyote kubwa katika kuwatambua.

Manabii wa uongo ndio wamekuwa kirusi kilichoupaka wokovu matope.

Ujue, watu wa dini huwa hawajui kutofautisha kati ya vituo vya maombezi na kanisa. Wao kila wanaposikia mahali watu wakisema 'kwa jina la yesu' wanaamini ni kanisa la waliookoka (walokole).

Katika mitandao mbalimbali, huwa tunaona picha za kutisha sana!

Tunaona manabii hao wakiwacharaza watu viboko, wakiwavua wadada nguo za ndani ili ziombewe, wakiwalisha waumini wao majani, wakiwashika wadada sehemu za siri tena hadharani, wakiwapulizia waumini wao vimiminika vya sumu, wakiwabusu wadada mdomoni na kuwatemea mate yao, wakiwakumbatia wadada kimapenzi kabisa, na mambo mengi ya kutisha kama hayo!

Lakini hawa wafuasi bado wanamwamini mtumishi wao, wanamwimbia, wanampigia magoti, wanampa heshima zenye utata, na mambo kama hayo!

Hivi hawa watu waliologwa namna hii ni akina nani?

Na wanalogwaje hadi wanaingia 'kingi' namna hiyo?


Mbona wamekuwa 'madwanzi' namna hiyo?

Tuongee ukweli, kama mtu ameokoka, anamjua Mungu vizuri huku akiabudu katika kanisa la waliookoka, hakika hawezi kudanganywa kirahisi namna hiyo!

Kama mtu hajaokoka, na hajui maana ya wokovu, huyu anaweza kulogwa na hawa manabii. Ndio maana wanaoenda kwenye vituo vya manabii na mitume hawa sio Wapentekoste, ingawa hutakosa huko Wapentekoste wachache wasiojielewa.

Wasaka miujiza wengi hutoka katika dini zinazo-hold kwamba hakuna kuokoka duniani. Hawa hutoka makanisani mwao na kutembelea kwa 'mtumishi' anayewaalika akisema 'watu wote wa dini zote mnakaribishwa.

Ziko njia mbalimbali zinazotumika kuloga watu hawa:

Kwanza ni kuwafanya watu wawe tegemezi kwenye kuomba, wasiombe bali waombewe, kwamba wao hawana nguvu bali mtumishi fulani ndio ana upako sana, wao hawasikilizwi na Mungu bali mtumishi ndio ana kibali mbele za Mungu, kwa hiyo tegemeo lao liwe kwa mtumishi, na hakuna namna ya kumfikia Mungu na kupata mahitaji yao pasipo kumtegemea mtumishi na upako wake na mafuta yake, na maji yake, na unabii wake, na sabuni yake, na vitambaa vyake, na mafunuo yake, na fruto zake, nk.

Ukishatengenezewa fikra hizi tegemezi, hapo ujue umeshalogwa vizuri.

Kama nilivyosema, asilimia kubwa ya wanaologwa hawatoki kwenye makanisa ya waliookoka. Ni wachache tu wasiojielewa.

Wengi wao hutoka katika dini zisizoamini wokovu na kuuhubiri.

Wakishalogwa wanaanza kupewa ratiba:

Utasikia wiki hii ni sadaka ya 30,000 kutoa jini mahaba, wiki hii ni 50,000 ya kukomboa ardhi, wiki hii ni ya kukomboa kichwa, wiki hii ni ya kufungua mikono ili kila unachogusa kifanikiwe, wiki hii ni ya kukomboa kiuno na uzao wako, wiki hii ni ya kukomboa miguu, wiki hii ni ya kukomboa mdomo, wiki hii ni ya kukomboa jina, wiki hii ni ya kukomboa kitovu, wiki hii ni ya kukomboa nyota yako,

Wiki hii ni ya kujipatanisha na ardhi yako, wiki hii ni ya kupokea nyumba, wiki hii ni ya kupokea magari, wiki hii ni ya kupokea mafuta ya biashara, wiki hii ni ya kufungua anga lako, wiki hii ni ya kumfukuza Babeli wako, wiki hii ni ya kumfukuza Ashuru, wiki hii ni ya kumfukuza Delila wako, wiki hii ya kuvunja laana na mikosi, wiki hii ni ya kudili na ndoto, wiki hii ni ya kukomboa maziwa ya kina mama, wiki hii kumwondoa mfalme wa Uajemi, listi hii ya kuloga haitaisha!

Kumbuka, kila hitaji lazima liambatanishwe na sadaka inayotangulia kutangazwa (promotiwa).

Ukitaka kujua aliyelogwa, jaribu kukutana na mtu wa namna hii umwambie; "Ninatafuta kazi sijapata."

Utajibiwa: "Unatakiwa ukomboe miguu yako ili ukienda kuomba kazi upewe. Inatakiwa ulete vyeti vyako kwa mtumishi fulani viombewe utapata kazi."

Au jaribu kuandika kwenye mitandao hivi; "Jamani naumwa kichwa niombeeni"

Utasikia: "Omba toba kwa ajili ya ardhi, usiku saa tisa kemea mti wa ukoo, utapona mtumishi."

Hiyo ni dalili tosha ya mtu ambaye hajaokoka, na ameshalogwa tayari.

Lakini kuna mbinu nyingine ya pili matata sana hutumika kuloga, ni hii;

Walogaji hufundisha habari za nguvu za giza na si habari njema za wokovu kwa undani, bali watafundisha habari zote za shetani.

Wokovu utaguswa kwa mbaali tena mara moja moja.

Watu hawatahubiriwa toba, wala ubatizo wala umuhimu wa kujiunga na ushirika wa kanisa la waliookoka kama kweli umeokoka. Huo utaitwa ni udini.

Badala ya kufundishwa habari za wokovu, watu watafundishwa na kujaa maarifa yote ya nguvu za giza;

Watu watajua aina zote za majini, harufu zao na tabia zao, aina za mapepo na tabia zao.

Watu watajua jinsi wachawi huloga, watapewa habari za watu wanaosadikiwa kwenda kuzimu na kurudi, nk.

Watu watalogwa kwa kufundishwa sana habari za giza, ILI WAJAE HOFU!

Wakijaa hofu, watajiona hawawezi bila kuombewa na mtumishi, simu itapigwa usiku, mtumishi nimeota hiki mara nimeoneshwa kile, mtumishi atapigilia msumari kwamba unazungukwa na wachawi sana, mume wako anakuendea kwa waganga, mama yako anataka kumloga mwanao, mwenye nyumba wako ni mchawi nk.

Kuanzia hapo ni vita mtaani, kwenye ndoa na kwenye familia, watu wamelogwa na wamegombanishwa hatari!

Mtu akishalogwa kisawasawa, utajua tu.

Akiona panya ndani anaamini ni mapepo, akiona mende atakemea kwa mishipa yote, akiona siafu ndani anaamini ni roho chafu ataanza kupiga makombora ya moto, akiona popo basi hapo ujue ni simu kwa mtumishi, na hapo atalogwa zaidi.

Mtu aliyelogwa hivi akisikia neno maombi mara moja anaanza kuwaza vita na shetani tu na mambo ya kukemea tu.

Maombi yake yote ni kukemea na kuona mashetani tu!

Mtu aliyelogwa huwaza maadui tu, hana rafiki, anaishi kwa umakini uliopitiliza hadi unamnyima raha na uhuru, anaogopa kukamatwa na 'maadui' zake.

Mtu aliyelogwa humwona shetani tuu kwenye kila kitu.

Anamjua sana shetani, kila saa kukemea, kila mahali ni kuwaza mapepo na majini tu.

Anatembea na chumvi ya kumlinda, amejirashia maji ya upako ya kumlinda, amejipaka mafuta ya upako ya kumlinda!


Akisimamishwa na trafiki ni pepo, akiambiwa alipe kodi ni pepo, hapigi kura anasema ni ufreemasoni, hata akiteleza tu utasikia ni shetani ameinuka!!

Ndio maana wanazidi kujaa mapepo maana wao humtafakari shetani na mapepo tu kuliko Mungu.


Kitu kibaya zaidi kuhusu watu hawa, wakishalogwa hawaongozwi tena na Neno la Mungu. Wao ni mafunuo na ndoto na maono tu!

Kila jawabu la mambo yao lazima lipatikane kwa njia ya ndoto na maono si kwenye Neno!

Mtu akishalogwa vizuri, Neno kwake huwa si kitu.

Anaweza kufanya kitu cha ajabu kabisa na akasema ni Roho Mtakatifu amemwongoza!

Haijalishi anaenda kinyume na Neno, wao wanachoamini zaidi ni maono na ndoto zao, bila kujali kama zinaivana na Neno au la!

Njia nyingine bora ya kuwaloga watu ni kwa maneno laini na kutumia Maandiko yanayoahidi baraka tu, na si Maandiko yanayomtaka mtu abadilike, atubu na aokoke.

Walogaji hawagusi Maandiko ya kukemea dhambi, ya kuonya na kusahihisha.

Wanataka 'bless-me-verses' tu, na si 'correct-me-verses.'

Yaani, wanapenda na kutaka yale Maandiko ya NIBARIKI na si yale ya NISAHIHISHE NIBADILIKE.

Ukishasikia mtu anakwambia mimi naabudu kwa mtumishi fulani, halafu anaanza kumsifia tena sana kwa jinsi huyo mtumishi alivyo na upako, ooh mtumishi ni fire, ooh mtumishi wetu akikupa saa yake huwezi kuibeba hapo chini, akikusogelea unaangukia kule bila kukugusa, akivua kiatu akasema mtu akivae wote wanashindwa kukivaa wanaanguka tu, ukiona mtu anajisifia mtumishi wake hivyo, ujue tayari mtu ameshalogwa hapo!

Mtu akishalogwa huwa haendi kanisani, huwa anajiunga na vituo mbalimbali vya maombezi kutafuta 'kufunguliwa'.

Ukishaona mtu hapendi kuwa chini ya mchungaji na ushirika wa kanisa la waliookoka, anapenda kuhudhuria maombezi huku na kule, tayari ameshalogwa vizuri!

Utasikia "yule mtumishi akikuombea lazima upate kazi, lazima upone..nk!"

Nyumbani kwa aliyelogwa ni kule wanakosema "pokea gari! Pokea milioni mia wiki hii! Pokea miujiza yako leo!"

Huko toba wala utakatifu sio ajenda!

Kwao Mungu ni kama 'entity' fulani anayetakiwa kuwapa kila wanachoona wanastahili kukipata.

Basi watu wanaohudhuria huko hulogwa weee mpaka wanaanza kudhani wameokoka, wakidhani wokovu ni njia hiyo.

Inafika wakati hawawezi kutofautisha kanisa na vituo vya maombezi.

Watu waliologwa hivi huwa hawamwamini mtumishi mwingine, wanawadharau wachungaji wakidai hawana upako, wanamwamini mtumishi wao tu.
 
Back
Top Bottom