Haya yatakusaidia uwapo mikononi mwa polisi

Gasy wa Ukweli

JF-Expert Member
Joined
Nov 7, 2010
Posts
397
Reaction score
201
[h=3]Posted by Bashir Yakub at Tuesday, November 24, 2015[/h]



NA BASHIR YAKUB -


1.JE KITU GANI KIFANYKE ASKARI ANAPOKUNYIMA DHAMANA.


Kwanza ieleweke kuwa dhamana ni haki yako. Haki ni jambo la lazima. Haki ya dhamana inaruhusiwa kunyimwa katika makosa machache sana kwa mfano uhaini, wizi wa silaha, mauaji n.k. Makosa mengine madogo madogo hasa haya ya kila siku ya kutukana, kudhalilisha, kupigana, ajali ndogo, wizi usio wa silaha, na mengine dhamana ni lazima. Hata hivyo makosa ambayo hayaruhusiuwi kwa dhamana ni lazima askari anapokunyima dhamana aandike sababu za kukunyima dhamana.


Na hapohapo yatakiwa ahakikishe anakufikisha mahakamani haraka sana iwezekanavyo hasa ndani ya saa 24 ili mahakama ikatizame shauri lako na haki unazostahili. Ni makosa makubwa askari kumnyima raia dhamana pale anapostahili na ni makosa makubwa askari kutomfikisha mtuhumiwa mahakamani haraka bila sababu za msingi. Unayo haki ya kumtaka askari akufikishe mbele ya hakimu/jaji haraka ili ukaombe dhamana huko na haki zako nyingine. Katika hili hautaomba ila utamtaka askari kufanya hivyo.


2. JE DHAMANA NI LAZIMA UWEKE(DEPOSIT) YA KIASI CHA FEDHA.


Hapana dhamana si lazima uache pesa. Unaweza ukapewa dhamana kwa ahadi ya maandishi tu. Ahadi ya maandishi ni masharti ambayo utayasaini na kuahidi kuyatekeleza utapokuwa umeachiwa kwa dhamana. Moja ya masharti hayo ni kuahidi kufika tena kituo cha polisi au mahakamani katika muda utakaopangwa. Dhamana ya kuweka kiasi cha fedha huwa inaamriwa iwapo kuna makosa makubwa yaliyotendeka. Hata hivyo fedha hizo hutakiwa kurudishwa ama baada ya upelelezi kukamilika na kuonekana mtuhumiwa hana kosa au baada ya kuwa huru kutokana na amri ya mahakama.


3 JE INARUHUSIWA KUMKAMATA MWINGINE BAADA YA KUMKOSA MTUHUMIWA HALISI.


Ni kosa kubwa askari kumkamata mtu mwingine baada ya kumkosa mtuhumiwa. Mara kadhaa hutokea askari kuondoka na ndugu , mtoto au mke wa mtuhumiwa baada ya kumkosa mtuhumiwa nyumbani. Hii hairuhusiwi kabisa. Sheria iko wazi kuwa aliyetenda kosa ndiye anayewajibika kwakosa.

Kama hayupo na hawezi kupatikana hilo haliwahusu ndugu, watoto, mke au mme wa mtuhumiwa.

Kosa ni kwa aliyetenda kosa basi na si vinginevyo.

4. KUWEZESHWA KUWATAARIFU NDUGU UNAPOKAMATWA.

Inapotokea umekamatwa bila ndugu zako kuwa na taarifa na ukawa unashikiliwa kituo cha polisi basi unayo haki ya kuwezeshwa na askari waliokukamata kuwataarifu ndugu, jamaa na mwanasheria iwapo unaye ili waweze kufika kituoni kwa hatua .

Kama huna mawasiliano ya simu ni wajibu wa askari waliokushikilia kukuwezesha kupata mawasiliano hayo ili uwasiliane na ndugu hao.

5. JE INARUHUSIWA KUKAMATWA BILA KUAMBIWA SABABU.

Hapana hairuhusiwi. Unapokamatwa ni lazima kuambiwa sababu za kukamatwa huko.

Ikiwa umekamatwa katika mazingira ambayo sio ya vurugu basi inatakiwa kabla hujakamatwa askari ajitambulishe na akwambie kuwa anatakiwa kukukamata kwasababu hii na hii.

Ikiwa katika mazingira ya vurugu kwa mfano ulikuwa unagombana, kwenye maandamano haramu , mapambano ya askari na wafanya fujo basi sababu ya kukamatwa utaambiwa baada ya kuwa umekamatwa na sio kabla.

6. JE UFANYE NINI IWAPO UMETOA LALAMIKO NA ASKARI WAMELIPUUZA.

Wapo baadhi ya watu wametoa malalamiko ya msingi kuhusu kuonewa au kutendewa jinai lakini askari polisi wamekataa kusajili malalamiko hayo wala kufungua kesi.

Hii inaweza kuwa imesababishwa na uzembe au rushwa aliyotoa mtenda kosa ili asifunguliwe mashitaka. Ikiwa litakutokea hilo basi waweza kutoa taarifa kwa askari wa cheo cha juu zaidi ya yule uliyeripoti kwake na hasa mkuu wa kituo.

Ikiwa na huko hakuna msaada basi waweza kutoa taarifa kwa hakimu wa mahakama iliyo karibu ambaye atatoa amri ya kusajiliwa shitaka hilo.

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
 

Tunashukuru sana kwa msaada wako kwani niwengi tulikuwa hatufaham hizi haki.
 
Shukrani mkuu! Ila kisaikolojia askari wa majeshi meengi wana kitu kinaitwa kisaikolojia tunaita superiority complex ukimaster na kuikontrol hii kwao basi hawana tena jipya na wanaweza hata kukusindikiza mpaka nyumbani kwako.

You need to understand them and their mental process, maafande hawanisumbui maana najua nguvu yao inachochewa wapi!?

Inagwaje, elimu murua saana hii, muhimu watu waipatae.
 
Vipi suala la Polisi kukukagua Gari lako utakuta wako barabarani wameweka kizuizi wanataka kukagua Gari lako..vile vile vipi iwapo Polisi kakupiga unaweza mshtaki wapi?
 
Mbona mleta mada ameileta kisiasa zaidi, iweje uongelee upande Moja wa shilingi.
Nashukuru ametanabaisha ya kuwa ni mwanasheria, shaka na hofu ni adithi aliyoandika, mbona haina "vielelezo"?
Zaidi hivi kweli mleta mada anaishi Tanzania Kweli, au aliishawahi hata siku moja kuangukia mikononi mwa polisi wa Tanzania? Mbali na shahiri lote hilo mbona hajatueleza hatua stahiki ya mwisho kuchukua iwapo yote hayo aliyoadithia kushindikana au ni nini "outcome" yake?
 

Mkuu mimi ni msomaji tu wa hizi makala, nimeamua kushare na Wana JF siko kisiasa kabsa. Elimu ya uraia Tanzania iko chini sana ndo maana polisi wana amua wanavyotaka. Ila tunapoelekea tutakuja kuwa vizur

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
 
Vipi suala la Polisi kukukagua Gari lako utakuta wako barabarani wameweka kizuizi wanataka kukagua Gari lako..vile vile vipi iwapo Polisi kakupiga unaweza mshtaki wapi?

Mkuu ngoja niwasiliane na huyo Mwanasheria ntaleta tena makala nyingine: Watanzania tujitahidi kujua haki zetu za msingi.
 
Hayo yanawezekana sehemu nyingine yoyote ila siyo Tanzania.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…