Hekaya: hadithi ya njia ya kukamata mwizi

Hekaya: hadithi ya njia ya kukamata mwizi

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
HADITHI YA NJIA YA KUKAMATA MWIZI​

ZAMANI za kale alikuwako mtu mmoja aliyekuwa na rasilmali yake, rupia elfu akazitia ndani ya mfuko akazifungia ndani ya sanduku lake. Hapana mtu aliyejua habari hii ila yeye na mkewe. Siku moja huyu mwenye nyumba ikampata safari ya kuondoka kwenda mbali; akamwacha mkewe nyumbani. Baada ya siku kupita akaja mwizi kule nyumbani, akavunja nyumba akavunja sanduku, akachukua ule mfuko, bibi hana habari. Alipoamka asubuhi aliona sanduku limevunjwa, na mfuko umechukuliwa.

Mwanamke asiseme neno mpaka alipokuja mumewe, akampa habari yote. Yule bwana mwenye nyumba akasikitika sana kuibiwa rasilmali yake, akainama, akawaza, akanena, “Najua fedha yangu haikwenda mbali imeibiwa na jirani, ila simjui; lakini haidhuru.” Akanyamaa kimya. Hakusema neno.

Siku moja alimwambia mkewe atengeneze vyakula maana ana karamu anataka kuwakaribisha jirani zake. Vikatengenezwa vyakula vingi akawaalika jirani zake wote kuja karamuni, wakaja wote.

Basi wakati walipokuwa wamehudhuria wote, aliwaambia “Waungwana niwieni radhi sana, nimekuiteni kwa maana mbili. Naliweka nadhiri nilipokuwa katika safari yangu ya kuwa pindi nirudipo salama nitafanya chakula kidogo nitajamali na jirani zangu. Basi nimerudi salama ndipo nikakuiteni kuja kwangu. Sasa kuleni, nikuambieni maana ya kwanza.”

Walipokwisha kula aliwaambia: “Sasa sikilizeni niwaambieni na maana ya pili; Mimi niliposafiri niliacha ndani ya nyumba yangu rupia elfu ndani ya sanduku. Nyuma yangu amekuja mtu amevunja sanduku amekwiba, na hii ndiyo rasilmali yangu. Na mimi nimepiga bao nimemjua mwizi wangu. Naye yupo hapa. Basi nimekuiteni mshuhudie, kwa kuwa mimi sitaki kufanya neno kando, nataka kumwua mbele yenu ili kulipa kisasi cha fedha zangu,” Aliposema hivi alifuta upanga wake, akasogea kule walikoketi watu kama ataka kumkata mtu. Mara lile jizi likaruka likatoka mbio, Ikawa watu kupiga kelele Hilo! Hilo! wakalifukuza hata wakalikaniata.

Yule mwenye nyumba akanena, “Haja yangu siyo kumwua, mimi nataka fedha zangu tu.” Wakamwuliza alikoweka zile fedha, akawachukua kwenda kuwaonyesha alipozifukia, akazifukua na zote zilikuwa kamili. Mwenye nyumba akashukuru Mungu, akaenda nyumbani kwake, wala hakushughulika na habari ya kumshtaki tena. Akasema haja yangu ilikuwa ni fedha, nimezipata, basi.
 
Back
Top Bottom