Hatua muhimu kuhusu kura ya maoni kwa kurejea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba [Sura ya 83 Toleo la mwaka 2012]
(1) "kura ya maoni" maana yake ni kura iliyopigwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii kwa madhumuni ya kuridhia Katiba inayopendekezwa;
(2) Kwa madhumuni ya kuyapatia uhalali masharti yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa, kutakuwa na kura ya maoni itakayoandaliwa, kuendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
(3) Ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa Katiba inayopendekezwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar itatayarisha na kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali swali litakaloamuliwa kwa kura ya maoni.
(4) Ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapishwa kwa swali katika Gazeti la Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar itatangaza taarifa inayoainisha: (a) siku ambayo kura ya maoni itafanyika;
(b) muda wa upigaji kura ya maoni; na
(c) muda wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupiga kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa.
(5) Kwa madhumuni ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura ya maoni Katiba inayopendekezwa, Tume italazimika, na vyama vya siasa na vyama vya kijamii vinaweza kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.
(6) Ndani ya siku ishirini na moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza taarifa, msimamizi wa uchaguzi wa kila jimbo la uchaguzi atawataaarifu wananchi wa eneo analohusika nalo kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa kura za maoni.
(7) Mtu yeyote ambaye jina lake limeingizwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanzishwa chini ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984, atakuwa na haki ya kupiga kura, isipokuwa kama mtu huyo atakuwa amezuiwa kupiga kura na sheria nyingine yoyote.